1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

DRC yataka vikwazo vya wazi dhidi ya Rwanda

21 Juni 2023

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inataka vikwazo vya wazi vitangazwe dhidi ya Rwanda, ambayo Umoja wa Mataifa inadai kuwa na ushahidi kwamba inaunga mkono waasi wa M23

Kombibild Felix Tshisekedi und Paul Kagame

Madai hayo yamejiri baada ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuwasilisha Jumatatu iliyopita, ripoti yao ya mwisho kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakithibitisha wazi kuhusika kwa jeshi la Rwanda katika mapambano baina ya M23 na jeshi la Kongo. 

Wataalamu wanadai kuwa na ushahidi wa ziada dhidi ya Rwanda

Ripoti hii mpya ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imejiri baada ya zile zilizotangulia, hasa ile ya Desemba. Wakati Rwanda ikiendelea kukanusha kuwaunga mkono waasi wa M23, wataalamu wanadai kuwa wamekusanya ushahidi wa ziada kuhusu jeshi la Rwanda kuhusika mkoani Kivu Kaskazini.

DRC yasema matamshi ya kulaani hayatoshi

Wapiganaji wa kundi la waasi la M23Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Kwa hivyo mamlaka nchini Kongo inadai sasa kuwe na vikwazo dhidi ya Rwanda kwani matamshi ya kulaani bado hayajatosha. Solange Masumbuko Nyenyezi, mbunge kutoka muungano wa vyama vilivyo madarakani amesema kuwa hatua za kweli, sahihi na zinazoonekana zinahitajika kwani Kongo imeshambuliwa na Rwanda bila haki na hayo yamefanywa chini ya uangalizi wa jumuiya ya kimataifa.

Wakazi wa Magharibi mwa Kongo wakumbwa na ukosefu wa usalama

Hayo yamejiri huku wakazi wa Magharibi mwa Kongo pia wakikumbwa na ukosefu wa usalama. Wanamgambo wa Mobondo waliokuwa wakivuruga usalama katika eneo la Kwamouth mkoani Mai-Ndombe sasa wanaendesha hali hiyo hiyo katika mikoa ya Kwango na Kwilu. Lucien Lufutu, mratibu wa mashirika ya kiraia mkoani Kwango anasema sasa wanataka mazungumzo ya amani na serikali.

Lufutu ameongeza kusema kuwa kiongozi wa Mobondo aiitwaye Lusifa aliwahakikishia wawakilishi wa mashirika ya kiraia waliokutana naye kwamba wao hawataki kupigana na wanajeshi ila wanachokitaka ni mazungumzo. 

Usajili wa wapiga kura watarajiwa kuanza Jumapili Kwamouth

Wakati hayo yakijiri, usajili wa wapigakura unatarajiwa kuanza Jumapili ijayo huko Kwamouth ambapo miezi iliyopita, tume huru ya uchaguzi haikufaulu kuwasajili wapigakura kutokana na hali ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo la mkoa wa Mai-Ndombe.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW