1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamii ya Batwa washambuliwa mbuga ya Kahuzi-Biega

6 Aprili 2022

Walinzi wa mbuga ya Kahuzi-Biega na wanajeshi wa Kongo wanashutumiwa kuwabaka na kuwauwa wakaazi asilia wa eneo hilo, kama mbinu ya kuwalazimisha kuhama kwenye ardhi yao, kwa mujibu wa mashirika ya haki za binaadamu.

Demokratische Republik Kongo, Angriffe auf die Batwa-Bevölkerung
Picha: Mariel Müller/DW

Nyaraka zilizowekwa hadharani na shirika linalopigania haki za wachache, Minority Rights Group (MRG), zinaeleza kuwa mashambulizi dhidi ya watu jamii ya Batwa, ambao ndio wenye asili ya mbuga hiyo, yamekuwa yakitendeka tangu mwaka 1976.

Lakini rikodi za karibuni zinataja matukio yanayofuatana kuanzia mwaka 2019, ambapo nyumba zao zimekuwa zikichomwa moto, wanawake na wasichana wao kubakwa na watoto wao kuuawa.

Kwa mujibu wa mashahidi, wanaotenda uhalifu huo ni walinzi wa mbuga hiyo pamoja na wanajeshi wa Kongo.

Kibibi Kaloba ni miongoni mwa watu 200 wajamii ya Batwa ambao wamekuwa wakiishi kwenye kambi isiyo rasmi ya wakimbizi kwa miezi kadhaa sasa.

Nyumba yake ilivamiwa na kuchomwa moto mwezi Novemba 2021, ambapo watoto wake wawili waliteketea kabisa. 

Ushahidi wa Kibibi

Kibibi Kaloba, ambaye watoto wake wawili waliteketezwa kwa moto na walinzi wa mbuga.Picha: Mariel Müller/DW

"Nilikuwa shambani kwangu nalima siku hiyo. Nikasikia kijiji chetu cha Bugamende kimevamiwa. Nikakimbilia kuwaokowa watoto wangu watano. Lakini nilipofika, nikakuta nyumba yangu imeshateketezwa kwa moto. Pamebakia moshi na majivu tu. Nilitumia jiti kuchakuwa kwenye majivu hayo na nikakuta vufu la mmoja wa watoto wangu," anasema Kibibi kwenye ripoti ya MRG.

Kibibi aliwakusanya watatu wake waliobakia hai na kukimbia nao. Wawili walioteketezwa kwa moto walikuwa na umri wa miaka minne na mitano.

Mashahidi wanasema wavamizi waliufunga mlango kwa nje kabla ya kuichoma moto nyumba hiyo.

Wanavijiji wanasema kuwa washambuliaji hao walikuwa walinzi wa mbuga na wanajeshi kutoka Jeshi la Kongo.

Mpango wa kuwaangamiza Watwa

Mkuu wa kabila la Batwa, Chifu Mbuwa BachimarendePicha: Mariel Müller/DW

Chifu wa kabila la Batwa, Mbuwa Kalimba Bachirembera, ameliambia shirika la haki za binaadamu la MRG kwamba ni wazi kuwa utawala wa mbuga umedhamiria kuwafukuza watu wa kabila lake kutoka kwenye mbuga hiyo, licha ya kwamba hiyo ni ardhi yao ya asili.

Kwa mujibu wa kauli yake, tangu mwaka 2019, wavamizi wamekuwawakija mara kwa mara "kuwashambulia watu wake, kuwauwa, kuwakata mikono na kisha kuwaonesha wengine wakiwatishia kwamba kama wasipoondoka, nao yatawafika hayo hayo."

Hata kwenye kambi ya muda waliyojishikiza kukaa, katika jengo la hospitali isiyomaliza kujengwa karibu na mbuga ya Kahuzi-Biega napo si salama.

Mbali ya kukosa chakula, maji na msaada wa kitabibu, wakimbizi hao wa jamii ya Batwa huvamiwa mara kwa mara kambini hapo.

Chifu Bachirembera anasema wiki chache zilizopita walivamiwa na kundi moja lenye silaha, ingawa kwa bahati nzuri hawakuwauwa.

Ghasia zinazodhaminiwa na dola

Vijiji vya jamii ya Batwa baada ya kuteketezwa kwa moto.Picha: Mariel Müller/DW

Shirika la haki za binaadamu la MRG limechunguza matukio haya kwa miaka mitatu sasa.

Kwenye ripoti yake yenye kurasa 100, linahitimisha kwamba walinzi wa mbuga hiyo na wanajeshi wa Kongo waliwauwa watu 20 wajamii ya Batwa, kubaka wanawake 15 na kuwalazimisha mamia kuyakimbia makaazi yao baada ya kuviteketeza vijiji vyao kwa moto. 

Msimamizi wa shirika hilo kanda ya Afrika, Agnes Kabajuni, anasema kinachoshuhudiwa sasa ni "sera ya machafuko yanayotendwa na dola kwa lengo la kuwatisha watu wa jamii ambayo tayari walishatengwa ili wayahame makaazi yao ya asili."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW