1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jamii ya wafugaji kupokea chanjo ya COVID 19 Kenya

3 Februari 2022

Serikali ya Kenya imeongeza juhudi za utoaji chanjo ya COVID 19 kwa jamii za wafugaji zilizoathirika na kipindi cha kiangazi na kuamua kuzihamisha jamii hizo huku ikiendelea na mgao wa chakula kwa wahanga wa baa la njaa.

Coronavirus | Booster | Stiko
Picha: agrarmotive/imago images

Tangu serikali ianze kutoa chanjo dhidi ya covid 19 kwa raia, idadi kubwa ya wakaazi katika majimbo kame nchini wamekuwa wakikwepa kupokea chanjo hiyo kutokana na udhaifu wao wa mwili unaosababishwa na ukosefu wa lishe. Katika jimbo hili la Marsabit, raia wengi hawajapata chanjo ya corona kwa kile baadhi yao wanasema hawana nguvu ya kustahimili dawa ya chanjo hiyo mwilini.

Japo wengi hawakutaka kurekodiwa kuhusu msimamo wao, serikali imeonekana kubaini changamoto hiyo na sasa, imekuwa ikiwashauri wananchi hao kupata chanjo hiyo wakati wa ugavi wa chakula cha msaada. Kamishna wa jimbo la Marsabit Paul Rotich, amewaeleza wananchi kwamba,chanjo hiyo ni salama na haiwezi kuwaathiri kivyovyote.

"Wananchi vile wameona kamishna akichanjwa,wengi pia wamjitokeza kuchanjwa.Hapa marsabit tuko katika asili mia sita pekee,” alisema Rotich

soma zaidi: Ukame waleta athari jimboni Marsabit nchini Kenya

Kijana wa Afrika akipokea chanjo ya COVID 19Picha: Cyril Ndegeya/ Xinhua News Agency/picture alliance

Wakati huohuo, waziri wa afya wa jimbo la Marsabit Daktari Jama Wolde amebaini kuwa,idadi kubwa ya raia hawajapata chanjo ya covid 19 akiwasisitizia haja ya kufanya hivyo kabla ya kupatwa na homa hiyo ya mapafu. Waziri Wolde amepuuzilia mbali uvumi wa kwamba chanjo hiyo ina madhara katika baadhi ya viungo vya mwili,akieleza kuwa,hakuna mkaazi aliyeripoti kuathirika baada ya kupokea chanjo hiyo.

"Kwa sasa wakaazi wana ufahamu kuliko isipokuwa kuna baadhi ambao bado wanatashuishi wapate hii chanjo, alisema Waziri Wolde”

Wizara ya afya imekuwa na shaka kuhusu idadi ya waliopokea chanjo hiyo kote nchini,serikali ikitishia kusitisha huduma muhimu kwa watakaokosa kupata chanjo hiyo katika miezi michache ijayo.

Jimbo la Marsabit limesalia nyuma katika idadi ya watu wanaojitokeza kupokea chanjo hiyo kutokana na makali ya njaa inayowakabili pamoja na utamaduni potofu kuhusu chanjo yenyewe.

Mwandishi: Michael Kwena, DW Marsabit

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW