Jammeh afungia redio inayomkosoa
2 Januari 2017Chama cha waandishi habari nchini humo kimeonya kwamba kufungwa kwa kituo hicho cha redio kunaashiria mwanzo wa ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari vya watu binafsi, hasa vile ambavyo vinatoa nafasi ya mawazo yanayopingana na serikali.
Redio Taranga FM kinaonekana kuwa kinamkosoa Rais Jammeh, ambaye alishindwa uchaguzi Disemba a mpinzani wake, Adama Barrow, aliyesimama kwa niaba ya muungano wa upinzani.
Awali, Jammeh alikuwa amekubali kushindwa na akampongeza Barrow, lakini wiki moja baadaye alilitangazia taifa hilo la Afrika Magharibi kwamba hakubaliani na matokeo ya uchaguzi, akidai kuwapo na mapungufu makubwa na chama chake kiliwasilisha pingamizi katika Mahakama ya Juu kutengua matokeo hayo.
Hatua hiyo ya Jammeh ililaaniwa ndani na nje ya nchi yake, huku Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi (ECOWAS) ikiapa kumuondoa kwa nguvu kama atakataa kuondoka kwa hiyari baadaye mwezi huu.