1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jammeh akataa kuachia madaraka

10 Desemba 2016

Asema hakubaliani na matokea akidai dosari kubwa zimetokea katika uchaguzi na kuwaonya wagambia wasithubutu kuingia mitaani kuandamana

Yahya Jammeh
Rais Yahya JammehPicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Rais Yahya Jammeh aliyeiongoza Gambia kwa kiasi miaka 22  ametangaza ijumaa usiku kwamba hakubaliani tena  na  matokeo yaliyompa ushindi mpinzani wake Adama Barrow na  kutaka uchaguzi mpya ufanyike.Jammeh ametoa onyo kali akiwataka wagambia wabakie majumbani mwao na kutothubutu kuingia mitaani kuandamana.Inaarifiwa wanajeshi walionekana wakiweka vizuizi vya magunia ya mchanga katika maeneo muhimu kote kwenye mji mkuu Banjul hali ambayo inatajwa kusababisha hali ya wasiwasi kote katika taifa hilo la Afrika Magharibi ambalo linaelekea kutumbukia katika mgogoro mpya Wa kisiasa.

Uchunguzi uliofanyika kuhusiana na matokeo ya uchaguzi wa Desemba Mosi yameonesha kutokea kwa dosari zisizokubalika upande wa tume ya uchaguzi alisema Jammeh katika hotuba yake iliyooneshwa kupitia Televisheni ya Taifa na kuonegeza kwamba hatokubali tena kuachia madaraka  kwa mgombea wa upinzani Adama Barrow.Zaidi rais huyo alisema'' kama nilivyokuyakubali matokeo ya uchaguzi kwa nia nzuri naamini kwamba tume huru ya uchaguzi ilikuwa huru na ya kweli na ya kutegemewa,Natangaza kwamba sikubaliani na matokeo kwa hali yoyote.

Rais mteule Adama BarrowPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

Jeshi limetawanywa katika mji mkuu  huku Marekani ikilitaka jeshi hilo kuendelea kuheshimu uatawala wa sheria na matokeo ya urais.Tayari upinzani umejibu hatua ya rais Jammeh kwa kumkosoa na kusema kupitia mitandao ya kijamii kwamba anakwenda kinyume na demokrasia lakini pia upinzani umewataka wananchi wagambia wabakie watulivu.Matokea ya hadi sasa yanaonesha Adama Barrow alishinda kwa asilimia 43.29 ya kura wakati Jammeh akipata asilimia 39.64 na idadi jumla ya waliojitokeza kupiga kura ni asilimia.Marekani kupitia balozi wake mjini Banjul imetowa mwito wa Utulivu na kulitaka jeshi liendelee kuheshimu utawala wa kisheria na matokeo ya uchaguzi wa rais.

Desemba 2 rais Jammeh alitoa hotuba iliyovuta hisia kubwa miongoni mwa wananchi wa Gambia baada ya kukubali kushindwa na kuahidi kumpokea madaraka mpinzani wake kwa njia ya amani tangazo ambalo lilizusha vifijo na nderemo katika nchi hiyo.

Lakini sasa Jammeh amegeuza msimamo na kusema kwamba uchaguzi wa Desemba Mosi ulikuwa ndio uchaguzi uliokabiliwa na udanganyifu mkubwa kabisa kuliko chaguzi zote katika historia ya Gambia.Nchi jirani ya Senegal imetoa tamko la kulaani kinachoendelea Gambia huku nchi hiyo ikilitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kukutana kulijadili suala hilo na pia kumtolea mwito Jammeh kuyakubali matokeo na kupisha kipindi cha mpito kwa njia ya amani na kuyakabidhi madaraka.

 

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Sylvia Mwehozi

     

   

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW