1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jammeh anusurika kupinduliwa

Mohammed Khelef30 Desemba 2014

Jeshi nchini Gambia limevunja jaribio la kumpindua Rais Yahya Jammeh wakati kiongozi huyo anayetambuliwa kwa misimamo yake yenye utataakiwa nchini Ufaransa.

Rais Yahya Jammeh wa Gambia.
Rais Yahya Jammeh wa Gambia.Picha: AP

Taarifa za kibalozi zinasema kwamba usiku wa kuamkia leo, wafuasi wa kiongozi wa zamani wa jeshi Lamin Sanneh wakiwa na silaha waliivamia ikulu kwenye mji mkuu Banjul na kituo kimoja cha jeshi kilicho karibu na makaazi hayo ya rais.

Baadaye mapigano makali ya risasi yalitokea yaliyoendelea hadi alfajiri, ambapo wapiganaji wanne wa Sanneh waliuawa na wengine wanne kukamatwa. Inaripotiwa kuwa wapiganaji hao walikuwa wamevuka mpaka wakitokea Senegal, nchi ambayo inaizunguka Gambia kutokea kaskazini hadi kusini.

Vituo vya redio na televisheni za serikali vilizimwa kwa sehemu kubwa ya alfajiri ya leo, huku Mkuu wa Usalama wa Taifa, Louis Gomez, akikataa kuzungumzia ripoti za jaribio hilo la mapinduzi.

Si mara ya kwanza

Hii si mara ya kwanza kufanyika kwa jaribio la mapinduzi kwenye nchi hiyo ndogo magharibi mwa Afrika, ambayo iliwahi kutawaliwa na Uingereza. Mwenyewe Jammeh aliingia madarakani kwa mapinduzi yasiyo umwagaji damu mwaka 1994 akiwa na miaka 29, na tangu hapo amesalia madarakani, akishutumiwa kutumia mbinu za kidikteta kutawala.

Wengi wanamchukulia Jammeh kuwa kiongozi asiyetabirika, na anafahamika kwa kutangaza mipango na mawazo yenye utata bila kutoa tahadhari. Mwaka 2012, alitumia hotuba yake kwa taifa kwenye sikukuu ya Kiislamu kutangaza mipango ya kuwanyonga wafungwa waliokuwa wakisubiri kupewa adhabu yao.

Wafuasi wa Rais Yahya Jammeh wa Gambia.Picha: AP

Uamuzi huo ulilaaniwa vikali na makundi ya haki za binaadamu na jamii ya kimataifa, ikiwemo serikali ya Uingereza. Miaka mitano kabla ya hapo, Jammeh alidai kwamba alikuwa anaweza kutibu virusi vya Ukimwi na ugonjwa huo, kupitia tiba ya mitishamba ambayo inawataka wagonjwa kuacha kutumia vidonge vya kupunguza makali ya Ukimwi.

Wanaharakati wa haki za binaadamu wanamlaumu pia Rais Jammeh kwa msimamo wake dhidi ya ushoga, na namna anavyowashughulikia wapinzani wake wa kisiasa na waandishi wa habari wanaomkosoa. Jammeh ni mmoja wa viongozi wa Kiafrika wanaouzungumza vibaya ushoga na hivi karibuni amewahi kutishia hata kuwakata vichwa watu wenye mahusiano ya jinsia moja.

Marekani iliindosha Gambia hivi karibuni kutoka kwenye mkataba wa kibiashara, ikiwa ni hatua ya kuiadhibu nchi hiyo kwa rikodi yake ya haki za binaadamu, ikiwemo sheria iliyosainiwa mwezi Oktoba, ambayo inatoa adhabu ya kifungo cha maisha kwa mashoga.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga