1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jammeh apinga matokeo mahakamani

Isaac Gamba
14 Desemba 2016

Rais wa Gambia Yahya Jammeh amewasilisha pingamizi katika mahakama kuu nchini humo kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika hivi kabuni licha ya awali kukubali kushindwa.

Gambia Wahlen Yahya Jammeh
Picha: Reuters/C. Garcia Ralins

Pingamizi hilo lililosainiwa na katibu mkuu wa chama cha Rais Yahya Jammeh linataka kuitishwa upya kwa uchaguzi na kupitiwa upya kwa daftari la watu waliosajiliwa kupiga kura.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press pingamizi hilo linadai kuwa uchaguzi huo haukufanyika katika mazingira yaliyo huru na haki na hivyo kutaka matokeo yake yabatilishwe.

Hapo kabla Rais Jammeh aliyakubali matokeo hayo na kumpigia simu kumpongeza mgombea wa chama cha upinzani Adama Barrow, lakini wiki iliyopita alitangaza kuyakataa matokeo ya uchaguzi huo.

Miongoni mwa mapungufu yaliyoorodheshwa katika waraka wa pingamizi hilo dhidi ya tume huru ya uchaguzi nchini humo ni pamoja na matokeo tofauti yaliyotangazwa siku moja baada ya uchaguzi na pia yale yaliyotangazwa tarehe 5, Disemba huku pia wakihoji ni kwa nini wapiga kura 360,000 hawakupiga kura.

Hata hivyo, tume ya uchaguzi nchini humo imedai kuwa uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira yaliyo huru na haki na kuongeza kuwa matokeo ya  kura zilizohesabiwa baadaye hayabadilishi matokeo ya uchaguzi huo na kuwa mgombea wa upinzani Adama Barrow bado anabakia kuwa mshindi.

Jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha pingamizi la kupinga matokeo ya uchaguzi huo. Hata hivyo kwa hivi sasa kisheria mahakama kuu ya Gambia haina majaji wa kusikiliza shauri hilo hivyo haifahamiki pingamizi hilo limewasilishwa kwa nani.

Viongozi wa ECOWAS wamtaka Rais Jammeh kuheshimu matokeo.

Rais wa Liberia Ellen Johnson SirleafPicha: Reuters/A. Sotunde

Hapo jana vyombo vya usalama nchini Gambia viliweka kizuizi katika lango la tume ya uchaguzi nchini humo kuwazuia wafanyakazi wa tume hiyo kuingia katika ofisi za tume wakati viongozi kadhaa wa mataifa ya Afrika Magharibi wakiwasili nchini humo kwa ajili ya kutoa mwito kwa Rais Jammeh kuheshimu matokeo na kuruhusu kuendelea kufanyika mchakato wa kubadilishana madaraka kwa njia ya amani.

Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf aliyeongoza ujumbe wa viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi wa nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS amesema Rais wa Gambia Yahya Jammeh amewahakikishia kuwa nchi hiyo itaendelea kuwa katika mazingira ya amani wakati pingamizi lililowasilishwa na chama chake likifanyiwa kazi.

Viongozi wengine walioko kwenye ujumbe huo ni pamoja na  Rais wa Nigeria Mohammadu Buhari, Rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma na Rais wa Ghana John Mahama ambaye pia tayari ameshindwa katika uchaguzi uliofanyika nchini mwake hivi karibuni.

Rais Sirleaf amesema viongozi hao wanatarajia kukutana na viongozi wengine katika eneo hilo la Afrika Magharibi siku ya Jumamosi mjini Abuja, Nigeria.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/EAP/DW

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW