1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jnaga la corona lawashughulisha wahariri Ujerumani

20 Machi 2020

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii wamejishughulisha sana na janga la virusi vya corona ambalo limesababisha taharuki kubwa kote ulimwenguni.

Tansania | Julius Nyerere International Airport - Passagiere werden auf Corona Virus überprüft
Picha: Tanzania Airport Authorities/B. Mollel

Gazeti la die Tageszeitung limeandika juu ya janga la maambukizi ya virusi vya corona ambayo pia yameanza kulikumba bara la Afrika. Gazeti hilo linasema kwa mtazamo wa watu wengi barani Ulaya, Afrika ni sehemu ya magonjwa. Maradhi kama ukimwi na ebola yanatajwa kama ushahidi wa mawazo hayo! lakini gazeti linasema, sasa kibao kimegeuka kwani Ulaya sasa ndiyo imekumbwa zaidi na maambukizi a virusi vya corona.

Mpaka sasa ni idadi ndogo tu ya watu waliokumbwa na maambukizi hayo katika nchi za Afrika na waliokufa ni wachache!  Kutokana na idadi kubwa ya maambukizi na vifo barani Ulaya, wananchi wa kawaida katika nchi za Afrika wanasema, sasa mafisadi wa Afrika hawawezi kwenda kutibiwa Ulaya kama kawaida yao!

Hata hivyo gazeti lingine la Die Welt linaelezea wasiwasi juu ya mambukizi ya virusi vya corona barani Afrika na limemnukulu mhisani mkubwa duniani na mwanzilishi wa kampuni ya Microsoft Bill Gates akitahadharisha kwamba watu wengi wanaweza kukumbwa na maambukizi.

Gazeti la Die Welt linaeleza kwamba janga la Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lilionyesha jinsi ilivyokuwa vigumu kuyakabili maradhi yanayosababishwa na maambukizi, siyo tu kwa sababu mfumo wa afya haujawa imara bali pia kutokana na migogoro ya kivita, miundo mbinu hafifu na imani potofu.

Kutokana na miundombinu hafifu pia ilikuwa vigumu kupeleka dawa kwenye sehemu kadhaa za nchi. Kwa kuzingatia sababu hizo mambo yanaweza kuwa mabaya endapo maambukizi ya virusi vya corona yatalipuka katika nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tofauti na virusi vya Ebola, virusi vya corona vinasambaa kwa haraka kwa wakati mmoja.

Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Gazeti la Die Zeit, wiki hii linakumbusha yaliyotukia nchini Afrika kusini tarehe 21 mwezi Machi mwaka 1960. Siku hiyo polisi wa makaburu waliawua watu kwenye kitongoji cha Sharpeville. Katika muda wa sekunde chache watu 69 waliangamizwa. Huo ulikuwa mshutko mkubwa siyo tu nchini Afrika Kusini bali duniani kote.

Gazeti la Die Zeit linasema huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kumalizika kwa utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini. Baada ya mauaji hayo baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio juu ya kung`olewa kwa mfumo wa kibaguzi. Gazeti la Die Zeit linasema wakaazi wa kitongoji cha Sharpeville walioshuhudia mauaji hayo kama Selina Mnguni anasema aliyoyaona na kuyasikia siku hiyo ya tarehe 21 mwezi Machi mwaka 1960 yamefifia katika kumbukumbu, lakini amesema machungu bado yapo.

Kitongoji cha Sharpeville, sawa na vingine vya waafrika, havikufikiriwa na utawala wa kibaguzi kuwa sehemu za kuleta maendeleo. Hali hiyo imesababisha kufifia moyo wa ujasiriamari, na mpaka leo ,mabenki na hata serikali, inasita kuwekeza katika sehemu hiyo.

Matokeo yake ni kwamba asilimia 60 ya wakaazi 37,000 wa Sharpevielle hawana ajira. Vijana wengi wana matatizo kutokana na kutumia mihadarati. Wakaazi wa kitongoji cha Sharpeville wanasema wakati wote wametelekezwa, kwanza na utawala wa makaburu, na sasa wanapuuzwa na utawala wa chama cha ANC tangu mwaka 1994.

Hata hivyo mkaazi maarufu wa kitongoji cha Sharpeville Selina Mnguni aliyeshuhudia mauaji ya tarehe 21 mwezi Machi mwaka 1960, amesema ataendelela kuwa na matumaini, kwa sababu bila ya matumaini, historia ya Sharpevile haitakamilika ameeleza mama huyo.

Gazeti la Süddeutsche wiki hii linatupasha habari juu ya ng'ombe 1000 walioteremshwa kwenye bandari ya Luanda, mjini mkuu wa Angola. Kwa kawaida zinazoonekana kwenye bandari hiyo ni meli za kusafirishia mafuta na shehena za aina nyingine lakini safari hii shehena hiyo ilikuwa ya wanyama hao 1000.

Gazeti la Süddeutsche linatufahamisha kwamba Chad imewapeleka ng`ombe hao kama njia ya kulipa mkopo wa dola zaidi ya milioni 100 iliyochukua kutoka Angola. Ng'ombe hao ni sehemu tu ya deni, wengine watapelekwa karibuni. Chad itailipa Angola kwa njia hiyo kwa kupeleka jumla ya ngombe 7500 katika kipindi cha miaka 10.

(Tageszeitung, Die Welt, Süddeutsche)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW