1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la corona lazidi kuibua sintofahamu

12 Machi 2020

Makamu wa kwanza wa rais nchini Iran pamoja na mawaziri wawili ni miongoni mwa walioambukizwa virusi vya corona, wakati vifo vitokanavyo na homa hiyo vikizidi kuongezeka kutoka 62 hadi 354 nchini humo.

Iran Teheran Coronavirus
Picha: picture-alliance/AA/F. Bahrami

Nchini Iran, shirika la habari la FARS limeripoti maambukizi ya viongozi hao waandamizi katika wakati ambapo kunasambaa minong'ono kuhusu hali ya kiafya ya makamu wa rais Eshaq Jahangiri. Jahangiri hakuonekana kwenye picha za mikutano ya ngazi za juu ya hivi karibuni hali inayoibua wasiwasi kuhusu kiongozi huyo.

FARS, limesema wengine wanaoumwa ni waziri wa utamaduni, utalii na shughuli za mikono Ali Asghar Mounesan na waziri wa viwanda, madini na biashara, Reza Rahman.

Katika hatua nyingine, Kuwait imetangaza kusitishwa kwa shughuli zote nchini humo kwa muda wa wiki mbili, wakati visa vya corona vilivyothibitishwa vikipanda kuanzia 24 hadi 262. Wengi wa wanaoambukizwa katika visa vipya hupata dalili kama kikohozi na homa ya wastani. Lakini kwa baadhi ambao ni pamoja na wazee na watu wenye afya dhaifu hukabiliwa na dalili kama ya homa kali ya mapafu. Na wengi pia hivi sasa wanapona homa hiyo ya corona.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu atangaza kuongeza fedha za kunusuru biashara zilizoathirika na CoronaPicha: Reuters/A. Awad

Soma zaidi: Iran yathibitisha vifo vya kwanza vya virusi vya Corona

Nchini Israel, waziri mkuu Benjamin Netanyahu ametangaza kiasi cha dola bilioni 2.8 za kuokoa uchumi katika wakati ambapo inapambana na virusi hivyo vya corona. Fedha hizo ni mara mbili ya zile zilizotangazwa awali kwa ajili ya kusaidia biashara zilizoathiriwa pakubwa na mzozo huo.

''Uchumi wa Israel uko katika hali nzuri sana. Tunaingia kwenye mzozo wa corona, lakini mazingira yetu ni bora zaidi ya mataifa mengine ulimwenguni. Tumechukua hatua kama ufadhili wa dola bilioni 1.13 ili kusaidia biashara zilizoathiriwa na virusi hivyo. Na wakati huu tunaangazia kuongeza fedha za ziada,'' amesema Netanyahu.

Israel imethibitisha wagonjwa 77 waliambukiwa virusi hivyo. Netanyahu amewahakikishia raia wake kwamba hakutakuwa na tatizo la upatikanaji wa bidhaa kwa kuwa zinaendelea kuingia kupitia baharini, na kwa hivyo hakuna sababu ya watu kuwa na wasiwasi.

Rais wa Halmashauri kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen, atarajiwa kutangaza ufadhili zaidi wa vita dhidi ya Corona.Picha: Reuters/F. Lenoir

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula Von der-Leyen baadae hii leo anatarajiwa kutangaza mpango wa dharura wa kupambana na virusi vya corona barani Ulaya. Kusambaa kwa virusi hivyo, tayari kumeathiri masoko na kuibua wasiwasi mkubwa wa mdororo wa kiuchumi katika wakati ambapo pia kunaongezeka miito ya kuongezwa kwa ufadhili.

Baada ya mkutano na viongozi wa Ulaya juzi Jumanne, Von der Leyen alisema Umoja wa Ulaya utatoa hadi Euro bilioni 25 kusaidia nchi wanachama zilizoathiriwa na mzozo huo, na msemaji wa umoja huo amesema fedha hizo zitatoka kwenye bajeti iliyopo.

Taarifa zilizotolewa muda mfupi uliopita zinasema, corona ambayo hapo jana ilitangazwa kama janga la kimataifa na Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO huenda likamalizika ifikapo mwezi Juni, hii ikiwa ni kulingana na mshauri mwandamizi wa afya nchini China, Zhong Nanshan.

Nanshan aliyepata umaarufu kwa kusaidia kukabiliana na mripuko wa homa kali ya mapafu ya SARS mwaka 2003, amewaambia waandishi wa habari kwamba hata kiwango cha wagonjwa wanaorudiwa na maambukizi ya homa hiyo hivi sasa kimeshuka nchini China.

Mashirika: APE/AFPE/RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW