Maambukizo ya virusi vya Corona vinaongezeka kila siku
9 Oktoba 2020Idadi ya watu waliokufa hadi sasa kutokana na ugonjwa huo wa mapafu imepindukia 200,000 nchini Marekani pekee.
Utabiri huo umetolewa wakati ambapo maambukizo na pia idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitali ikizidi kuongezeka kote Marekani.
Idadi kubwa ya wagonjwa waliolazwa baada ya kukutikana na virusi vya corona imeripotiwa katika katika maeneo ya Montana, North Dakota, South Dakota na Wyoming.
Marekani ndio taifa lililoathirika zaidi na virusi vya Corona duniani, kwa kurekodi zaidi ya maambukizo milioni 7.5.
Wakati hayo yanaarifiwa, Rais Donald Trump alisema hapo jana kuwa anajisikia yuko vizuri, ikiwa ni wiki moja baada ya kulazwa hospitalini kwa kuugua ugonjwa wa Covid-19.
Daktari wa Trump, Sean Conley, amesema rais huyo amemaliza matibabu na huenda akaendelea tena na kampeni za uchaguzi siku ya Jumamosi.
Na hapa Ujerumani, idadi ya maambukizo ya virusi vya Corona inaendelea kuongezeka kila siku. Kwa mujibu wa takwimu za taasisi ya Robert Koch, idadi ya maambukizi mapya ilikuwa 4,058 jana Alhamisi na 2,828 siku ya Jumatano. Kwa ujumla watu 314,660 wameambukizwa virusi hivyo huku watu 9,589 wakifariki dunia hadi kufikia sasa, wakiwemo watu 11 waliokufa katika saa 24 zilizopita.
Mkuu wa taasisi ya Robert Koch Lothar Wieler amesema : "Tangu mwanzoni mwa Septemba, idadi ya maambukizo imekuwa ikiongezeka kutoka wiki hadi wiki. Katika siku chache zilizopita, leo kumekuwa na zaidi ya maambukizi 4,000 ambayo yameripotiwa katika taasisi hii katika muda wa saa 24 zilizopita. Katika muda wa siku saba zilizopita, yaani kuanzia mapema mwezi huu wa Oktoba, idadi ya maambukizi imeongezeka mara mbili zaidi tofauti na mwezi Septemba."
Miji kadhaa ya Ufaransa yawekwa chini ya tahadhari
Nchini Ufaransa, miji ya Lyon, Lille, Grenoble na Saint-Etienne imewekwa chini ya tahadhari kufuatia ongezeko la idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
Baa zitafungwa na sheria kali za afya zitawekwa kwenye mikahawa ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo. Hata hivyo, hakuna vizuizi vya usafiri vilivyotangazwa.
Wizara ya Afya ya Ufaransa ilitangaza hapo jana maambukizo mapya 18,000 kwa siku ya pili mfululizo. Maambukizo hayo yanatokea wakati ambapo serikali inajaribu kuzuia kurudisha tena vizuizi.
Na barani Asia, China imesema itajiunga rasmi na mpango wa shirika la afya duniani wa chanjo dhidi ya Covid 19, Covax. Mpango huo unanuia kutoa dozi bilioni 2 za chanjo kufikia mwisho wa mwaka 2021.
Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje ya China haikuweza wazi kiwango cha msaada ambacho Beijing itatoa katika mpango huo wa chanjo japo Rais Xi Jinping mnamo mwezi Mei aliahidi kutoa msaada wa dola za kimarekani bilioni 2 kusaidia katika mapambano dhidi ya janga la Covid-19.
China itakuwa taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani kujiunga katika mpango huo wa COVAX, ambao unasaidia kufadhili chanjo kwa mataifa yanayoendelea.