Janga la COVID-19 laiweka Ulaya njiapanda
25 Oktoba 2020Jioni ya leo waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ametangaza hali ya dharura kwa taifa zima katika juhudi ya karibuni kabisa ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
Hali hiyo mpya ya dharura itadumu hadi mwezi Mei mwaka unaokuja.
"Hali tunayopitia sasa ni ngumu sana" amesema Sanchez katika hotuba yake kwa taifa baada ya kumaliza kwa kikao cha baraza la mawaziri kuamua hatua iliyofikiwa.
Hali hiyo ya dharura itazipa nguvu mamlaka za majimbo ambazo haumua masuala yake ya afya, kuweka marufuku kali ya kutembea ikiwa ni pamoja na zuio la kutoka nje usiku.
Kadhalika serikali za majimbo zinaweza kuweka vizuizi kadhaa kwenye biashara na kupunguza shughuli nyingine ikiwemo mikusanyiko kwenye makaazi ya watu na maeneo ya wazi.
Majimbo kadhaa ya Uhispania yamekuwa yakitoa wito kwa serikali kuu kutangaza hali ya dharura ili yaweze kuweka marufuku ya watu kutoka nje usiku.
Katika miezi ya mwanzo ya janga la virusi vya corona Uhispania iliweka vizuizi vikali sana kwa shughuli za kawaida lakini baadaye ilegeza masharti ya vizuizi kufuatia kupungua kwa idadi ya maambukizi ya COVID-19 majira ya kiangazi.
Italia na Ujerumani zachukua hatua
Kwengineko, serikali ya Italia imetoa amri itakahyoanza kufanya kazi kesho inayopiga marufuku mikusanyiko ya watu wanaopindukia 1,000 katika viwanja wa vya soka na michezo mingine.
Uamuzi huo ni sehemu ya mfululizo wa hatua chungunzima zilizotangazwa na serikali ya Italia tangu wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona kufukia idadi ya visa 20,000 kwa siku katika muda wa wiki mbili zilizopita.
Ligi ya kandanda ya Serie A ilimalizika bila kuwepo mashabiki uwanjani msimu uliopita kabla ya baadaye serikali kuruhusu angalau mashabiki 1,000 kuingia tena viwanjani.
Wakati hayo yakijiri, mji wa Frankfurt nchini Ujerumani umetangaza kufuta utamaduni uliozoeleka wa kuwa na soko la Krismasi mwishoni mwa mwaka katika wakati taifa hilo linapambana kudhbiti ongezeko linalotia wasiwasi la maambukizi ya virusi vya corona.
Hayo yameripotiwa na gazeti mashuhuri la Bild likinukuu maafisa wa mji wa Frankufurt waliofikia uamuzi huo Jumamosi jioni.
Soko la Krismasi la mjini Frankfurt ni moja ya masoko ya Krismasi yaliyo maarufu zaidi nchini Ujerumani na huvutia zaidi ya wageni milioni 2 wanaofika kununua vyakula, vinywaji na vitu vingine ambavyo huuzwa mahsusi kuelekea sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
Meya wa mji wa Frankurt Peter Feldmann amesema "lengo letu ni kuepuka awamu nyingine ya kuzifunga shughuli za umma"
Rais Steinmeier asema COVID-19 isiwe kisingizio katika ulinzi wa mazingira
Katika hatua nyingine rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema leo Jumapili kuwa janga la virusi vya corona linaloendelea kuiandama dunia halipaswi kuwa kisingizio cha kusahau ulinzi wa mazingira.
Akizungumza katika dhifa ya kukabidhi tuzo za mazingira nchini Ujerumani, Steinmeier amesema mapambano ya kuzuia mabadiliko ya tabia nchi hayapaswi kusisimama hata katikati ya juhudi za kupambana na virusi vya corona.
Nchini Uholanzi visa vya maambukizi ya virusi vya corona vimepindukia 10,000 katika muda wa saa 24 zilizopita, na kufanya hiyo kuwa rikodi ya juu kabisa ya maambukizi kurikodiwa nchini humo.
Wakati huo huo serikali ya Uingereza imesema inatafakari muda wa kukaa karantini kwa watu amabo wanaohisiwa kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi ya COVID-19.
Hayo yameelezwa na waziri wa Ireland Kaskazini Brandon Lewis alipozungumza na kituo cha televisheni cha Sky.