1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la Covid-19 limepora haki za wanawake na wasichana

Sylvia Mwehozi
8 Machi 2022

Leo ni siku ya kimataifa ya wanawake yenye kauli mbiu ya "usawa wa kijinsia leo kwa kesho endelevu". Janga la Covid-19 limeonekana kuwaathiri wanawake wengi waliopoteza kazi pamoja na wasichana kushindwa kwenda shuleni.

El Salvador Morena Herrera
Picha: Marvin Recinos/AFP/Getty Images

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake kwa kusema kuwa ulimwengu unahitaji viongozi zaidi wanawake wanaoweza kushinikiza nchi kushughulikia mgogoro wa mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na kujenga ulimwengu wa haki na endelevu. Ameongeza kuwa ulimwengu hauwezi kuondokana na janga la Covid-19 wakati ukipuuzia usawa wa kijinsia.Maelfu ya wasichana, wanawake walitekwa Msumbiji-Ripoti

"Katika siku ya kimataifa ya wanawake, tunawasherehekea wanawake na wasichana kila mahala. Tunasherehekea mchango wao katika kumaliza janga la Covid-19. Mawazo yao, ubunifu na harakati zinazobadili dunia yetu kuwa bora. Na uongozi wao katika kila nyanja ya maisha. Lakini pia tunatambua kwamba katika maeneo mengi, mshale wa haki za wanawake unarudi nyuma", alisema Guterres.

Wanafunzi wa kike wa AfghanistanPicha: Paula Bronstein/Getty Images

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Janga la Covid-19 limesababisha wanawake wengi kupoteza ajira zao na wasichana pia kukosa kwenda shule. Wanawake wanakabiliwa na umasikini na ongezeko la ukatili. Katika nchi zote, wanawake wana uwakilishi mdogo katika masuala ya utawala na taasisi za kibiashara.

Wanawake pia wanabeba mzigo mkubwa wa mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira. Guterres amehimiza kuwa umefika wakati wa kubadili fikra kwa ajili ya mwanamke na msichana. Kwa kuhakikisha usawa katika elimu, uwekezaji mkubwa katika mafunzo ya wanawake na kazi nzuri, kupitia hatua thabiti za kukomesha ukatili wa kijinsia, na mifumo thabiti ya ulinzi wa kijamii.

Nalo shirika la kimataifa la Amnesty International limesema kuwa haki za wanawake na wasichana zimekuwa chini ya mashambulizi kwa mwaka uliopita. Katibu mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard amesema hii leo kuwa "matukio ya mwaka 2021 na katika miezi ya mapema ya 2022 yamekandamiza haki na utu wa mamilioni ya wanawake na wasichana".

Mwanamke akiandamana mjini Manila, UfilipinoPicha: Ezra Acayan/Getty Images

Ameongeza kuwa migogoro ya ulimwengu imekuwa na athari zisizo sawa. Amelitaja janga la Covid-19 na kurudishwa nyuma kwa haki za wanawake nchini Afghanistan kuwa yalikuwa miongoni mwa matukio ambayo yaliathiri vibaya haki za wanawake na wasichana katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. " Kila moja ni mmomonyoko mkubwa kwa namna yake. Lazima tusimame na kutizama mashambulizi haya dhidi ya haki za wanawake na wasichana."

Pia ameorodhesha "unyanyasaji wa kijinsia ulioenea unaohusu mgogoro nchini Ethiopia, mashambulizi ya haki ya utoaji mimba nchini Marekani na Uturuki kujiondoa kwenye mkataba wa kihistoria wa Istanbul kuhusu jinsia, kuwa matukio mengine yaliyojitokeza na kutoa wito kwa serikali ambazo zimefanya hivyo kubatilisha maamuzi ambayo yalizidisha madhila kwa  wanawake na wasichana.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW