1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la kitaifa Afrika Kusini kufuatia ukosefu wa umeme

10 Februari 2023

Wanaomkosoa rais Cyril Ramaphosa kwa kutangaza janga la kitaifa kufuatia ukosefu wa umeme wadai serikali ya ANC ndiyo hasa janga la kitaifa

Südafrika Ramaphosa | Lage der Nation
Picha: GCIS/AP Photo/picture alliance

Nchini Afrika Kusini rais Cyril Ramaphosa ametangaza janga la kitaifa kufuatia kadhia kubwa ya ukosefu wa umeme nchi nzima.

Katika hotuba yake kuhusu hali ya taifa,Rais huyo wa Afrika Kusini alitangaza hatua hiyo kama juhudi za kukabiliana na tatizo hilo ambalo limeuweka pabaya ukuaji wa kiuchumi nchini humo.

 Kwenye hotuba yake iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na waafrika Kusini rais Cyril Ramaphosa alikiri kwamba nchi inakabiliwa na tatizo kubwa na kinachoshuhudiwa ni mgogoro mkubwa wa nishati na kwahivyo hana budi bali kutangaza janga la kitaifa ili kutoa nafasi ya kukabiliana na tatizo hilo pamoja na athari zake.

Rais Ramaphosa aliongeza kwa kusema nchi haiwezi kuendeleza shughuli za kimsingi za kila siku kutokana na ukosefu mkubwa wa umeme.

Tunafahamu kwamba bila ya  huduma ya kuaminika ya usambazaji umeme  biashara haziwezi kukua,shughuli za kiusafiri haziwezi kuendeshwa,mimea haiwezi kumwagiliwa maji na huduma nyingine za msingi zinatatizwa''

Katika kipindi cha miezi ya karibuni Afrika Kusini imejikuta imetumbukia kwenye matatizo makubwa ya mgogoro wa nishati ambao haujawahi kuonekana nchini humo kwa  miaka chungunzima, mgogoro unaosababisha kila uchao kushuhudiwa umeme kukatika kwa saa chungunzima.

Picha: DW

Mgao wa umeme

Na mgao huo wa umeme unafanyika hasa kusaidia kuunusuru mfumo wa usambazaji umeme unaoendeshwa na makaa ya mawe ambao unakabiliwa na kishindo kikubwa kutokana na kulemewa na mahitaji yaliyopo katika taifa hilo. 

Mtandao wa usambazaji umeme nchini humo unaendeshwa na shirika linalosimamiwa na serikali la Eskom ambalo kimsingi  vile vile limezongwa na madeni na kwahivyo limepoteza uwezo wa kukimu mahitaji ya umeme ya waafrika Kusini.

Rais Ramaphosa amekosolewa kwa kiasi kikubwa baada ya kutangaza janga la kitaifa kufuatia mgogoro huo.Mzwanele Nyhontso ni kiongozi wa chama cha Pan African Congress.

Unawezaje kutangaza janga la kitaifa kwa sababu wizara moja inakabiliwa na matatizo?Nini kitatokea na  shirika la ndege la  Afrika kusini SAA? atatangaza janga jingine la kitaifa kutokana na kinachoendelea kwenye shirika hilo la ndege,na kwenye kampuni inayoendeshwa na serikali ya Denel na mengineyo. Ukweli hapa ni kwamba, ambacho ni janga la kitaifa ni serikali yenyewe ya ANC''

Picha: Eskom/dpa/picture alliance

Eskom limekuwa likihangaika kuendeleza miundo mbinu yake inayoendeshwa kwa nguvu za makaa ya mawe wakati ikiandamwa na athari za rushwa zilizofuatia  kipindi cha uongozi wa Jacob Zuma, na kuiacha ikiwa na madeni chungunzima.

Hatua ya Ramaphosa ya kutangaza janga la kitaifa maana yake ni kwamba hatua hiyo itatoa nafasi ya kutolewa fedha za ziada kuharakisha utekelezaji wa miradi ya nishati bila ya kufuatwa baadhi ya sheria na miongozo iliyopo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW