Janga la Virusi vya Corona bado kuzungumkuti
5 Januari 2021Hatua ya kurefusha muda wa kufunga shughuli mbali mbali ili kudhibiti janga la kusambaa virusi vya Corona nchini Ujerumani inatarajiwa kutangazwa rasmi leo Jumanne baada ya mkutano kati ya Kansela Angela Merkel na mawaziri wakuu wa majimbo yote 16 ya nchi hii.
Hata hivyo tayari baadhi ya vyombo vya habari vilitangaza juu ya kufikiwa makubaliano hayo hapo jana huku shirika la habari la Reuters likieleza kwamba viongozi wa majimbo yote wamekubaliana na fikra ya kufunga shughuli za kimaisha hadi mwishoni mwa januari,isipokuwa viongozi wa majimbo mawili.
Shirika hilo iimenukuu chanzo kutoka timu inayoshiriki mazungumzo hayo.
Imeelezwa kwamba suala kubwa linalosababisha mvutano kwenye mazungumzo hayo ya viongozi ni pendekezo la kutaka shule na chekechea ziendelee kufungwa.
Wizara ya utamaduni jana ilisema kwamba kufunguliwa shule kutafanyika tu ikiwa shughuli za kimaisha zitaruhusiwa kuanza.
Kufikia sasa hatua ya kufunga maduka,shule na huduma nyingine kote nchini Ujerumani tangu desemba 16,hazijasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi ya vorusi vya Corona.
Na kuendelea kusambaa kwa virusi hivyo pamoja na vifo kumewafanya viongozi wa nchi kulazimika kurefusha muda wa kufunga shughuli hizo.
Viongozi wa majimbo ambao hawaafiki hatua ya kuendelea kufunga shughuli za kimaisha wanahoji muda uliopndekezwa wa kufunga shughuli hizo kwa mujibu wa gazeti la Frankfurter Allgemeine.
Uingereza nayo yarefusha vizuizi kupambana na COBID-19
Ama tukiondoka Ujerumani,huko Uingereza waziri mkuu Boris Johnson ameagiza kwa mara nyingine kufungwa kwa shughuli za kimaisha nchini humo kudhibiti kusambaa kwa maambukizi ya aina mpya ya virusi vinavyosambaa kwa kasi.
Shughuli nchini humo zitaendelea kufungwa hadi katikati ya mwezi Februari,shule za msingi na sekondari pia zitafungwa kuanzia kesho Jumatano.
Chini ya hatua hizo mpya watu wataruhusiwa tu kutoka majumbani mwao kwenda madukani kwa ajili ya manunuzi ya vitu muhimu,mazoezini,au kwa shughuli za kimatibabu au kwenda kazini.
Wanafunzi wa vyuo vikuu pia watabaki nyumbani hadi katikati ya mwezi ujao wa Februari.Waziri mkuu Boris Johnson amesema Uingereza iko katika kipindi kigumu huku visa vya maambukizi yakiongezeka kila kona ya nchi.
Tangu Desemba 29 nchi hiyo imekuwa ikiripoti visa vipya 50,000 vya maambukizi kila siku.Jana Jumatatu nchi hiyo ilirikodi visa 58,784 vya maambukizi mapya kote nchini.
Tangazo la kufungwa shughuli mbali mbali nchini humo limekuja wakati maafisa wa afya wakianza kutoa chanjo ya Oxford-AstraZeneca ambapo ajuza wa miaka 82 alikuwa mtu wa kwanza kupata chanjo.
Scotland pia yachukua mkondo huo
Ama huko Scotland waziri kiongozi Nicola Sturgeon naye pia alitangaza hatua kali ya kufunga shughuli mbali mbali kuanzia Jumanne leo hadi mwishoni mwa Januari.
Na wataalamu wa shirika la afya duniani WHO wanajiandaa kuingia China kutafuta chanzo cha virusi vya Corona katika ziara ambayo imetawaliwa na mihemko ya kisiasa.
WHO imesema China imeruhusu hatimae ziara hiyo ya timu ya wataalamu 10 watakaokaa kwa wiki tano au sita nchini humo.
Ingawa mamlaka za China wiki hii zilikataa kuthibitisha juu tarehe kamili au maelezo juu ya ziara hiyo.
Kadhalika kuna mashaka ikiwa kweli ujumbe huo wa WHO utafanikiwa kupata ukweli wowote juu ya virusi hivyo kutoka na shinikizo linaloweza kuwakabili kutoka serikali ya China.