1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Janga la virusi vya corona kitisho kwa usalama wa chakula

15 Oktoba 2020

Kwa miaka kadhaa faharasi ya njaa duniani imeonesha maendeleo ya dunia katika kukabiliana na tatizo la utapiamlo. Lakini janga la virusi vya corona linaweza kurejesha nyuma mafanikio hayo

Welthungerhilfe - Sierra Leone 2012
Picha: Desmarowitz/Welthungerhilfe

Miaka mitano iliyopita, Umoja wa Mataifa ulilifanya kuwa moja ya malengo yake, kuondoa njaa ulimwenguni ifikapo mwaka 2030. Hii ilimaanisha kwamba kila mwanadamu, hata kutoka katika nchi masikini kabisa angekuwa na chakula cha kutosha.

Lakini hali ikoje sasa hivi ulimwenguni? na je ulimwengu upo katika njia sahihi ya kufanikisha lengo hilo la Umoja wa Mataifa? Mwaka 2015 lilionekana lenye makuu la linaloweza kutekelezeka. Matumaini haya yalitiwa msukumo na ukweli kwamba  hali ya chakula duniani ilikuwa imeimarika katika muda wa miaka michache tu.

Mwaka 2000, Faharasi ya Njaa Duniani (GHI) iliipa Dunia nzima alama 28.2, ikimaanisha kuwa hali ilionekana kuwa mbaya, lakini leo, ulimwengu ukiwa na alama ya 18.2, njaa inakadiriwa tu kuwa ya wastani. Sifuri ingemaanisha hakuna njaa kabisaa, wakati 100 itakuwa alama mbaya zaidi.

GHI inatumia vipengele vinne muhimu kuainisha viwango vya njaa duniani ambavyo ni Utapiamlo, Watoto chini ya miaka 5 ambao wanauzito mdogo kulinganisha na umri wao, kudumaa  na vifo vya watoto chini ya umri wa miaka 5.

Licha ya maendeleo hayo, takwimu za hivi karibuni bado zinaogofya, Karibu watu milioni 690 ulimwenguni wanaugua utapiamlo, watoto milioni 144 wamedumaa, watoto milioni 47 wanauzito chini ya umri wao na mnamo 2018, watoto milioni 5.3 walifariki kabla ya kufikisha miaka mitano ya kuzaliwa, hasa hasa kutokana na utapiamlo.

Utapiamlo kwa watoto bado ni changamoto katika mataifa kadhaPicha: Roberto Schmidt/AFP/Getty Images

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, shirika la misaada la Ujerumani Welthungerhilfe linaitaja njaa duniani kama "kushindwa vibaya kwa kimaadili kwa kizazi chetu."

Hata kama wastani wa ulimwengu umeimarika, tofauti kati ya kanda mmoja mmoja na nchi ni kubwa mno. Kanda ya Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara yenye alama 27.8 na Asia Kusini yenye alama 26.0 ndio kanda zenye alama mbaya zaidi za njaa duniani.

Simone Pott, msemaji wa shirika la Welthungerhilfe, alisema "migogoro,umasikini, ukosefu wa usawa, afya mbaya na athari za mabadiliko ya tabianchi" ndio masuala makuu hapa.

Pott anatoa mfano wa Madagaska, ambako alama ya GHI hivi sasa iko juu ​kuliko mwaka 2012. Matatizo nchini humo yanajumuisha kuongezaka kwa umaskini, kukosekana kwa utulivu wa kisiasa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati zinashika mkia katika ripoti hiyo, ambapo mizozo ya vurugu na hali mbaya ya hali ya hewa vinapunguza maendeleo mazuri.

App ya kufuatilia lishe na ukuaji wa mtotoPicha: Welthungerhilfe

Lakini pia kuna mifano mizuri, Mnamo mwaka 2000, hali katika nchi mbili, Cameroon na Nepal, ilizingatiwa kuwa katika kiwango cha "kutisha", lakini leo hii ni miongoni mwa mataifa yenye idadi ya wastani ya njaa.

Nchini Cameroon pato la uchumi wa kila mtu liliongezeka zaidi ya mara mbili, kutoka dola 650 hadi dola 1,534 kati ya mwaka 2000 na 2018, kulingana na takwimu za Benki ya Dunia.

Angola, Ethiopia na Sierra Leone pia zimefanya maboresho makubwa tangu 2000, na alama zao za GHI zimepungua kwa chini ya alama 25.

Mnamo 2000, mataifa hayo bado yalikuwa yameainishwa katika kiwango cha "kutisha sana", haswa kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo ni miongoni mwa sababu kuu za njaa na utapiamlo.

Simone Pott alielezea sababu za maendeleo huko Nepal, kuwa ni uwekezaji katika maendeleo ya uchumi hali ambayo imepunguza umasikini katika eneo hilo. Kuimarika katika sekta ya afya ulisababisha kiwango cha chini cha vifo kwa watoto na afya bora kwa ujumla. Uwekezaji zaidi katika kilimo umesababisha usalama zaidi wa chakula.

Lakini sasa jambo kubwa lisilojulikana limeingia kwenye hesabu, nalo ni janga la covid-19 na madhara yake, ambavyo havikuzingatiwa na ripoti hiyo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW