1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Japan, Korea Kusini zatangaza vikwazo vipya dhidi ya Urusi

24 Mei 2024

Japan na Korea Kusini zimetangaza vikwazo vipya dhidi ya kampuni, meli na watu binafsi wanaozipa silaha Korea Kaskazini na Urusi wakati Moscow ikiwa vitani dhidi ya Ukraine kinyume cha maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Korea Kaskazini, majaribio ya makombora
Roketi la Korea Kaskazini likirushwa kwa majaribio siku ya tarehe 17 Mei 2024.Picha: KCNA/AFP

Korea Kusini inaishutumu Pyongyang kwa kuipa Urusi maelfu ya makontena ya silaha.

Wataalamu wanasema mfululizo wa majaribio ya silaha yanayofanywa na Korea Kaskazini katika siku za hivi karibuni huenda ni silaha zinazokusudiwa kupelekwa katika uwanja wa mapambano nchini Ukraine.

Soma zaidi: Marekani yasaka njia mpya kutekeleza vikwazo kwa Pyonyang

Msemaji mkuu wa serikali ya Japan, Yoshimasa Hayashi, amesema nchi yake inalaani vikali mikataba hiyo na kwamba, kwa ushirikiano na washirika wao, wameweka vikwazo kwa makundi 11 na watu binafsi wanaohusika na msaada wa kijeshi kati ya Urusi na Korea Kaskazini kwa lengo la kufanikisha vita vya Moscow nchini Ukraine.

Soma zaidi: Marekani yapanga mkutano na Japan na Korea Kusini kando na mkutano wa kilele wa NATO

Mwezi Agosti, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo kama hivyo ikisema Urusi ilikuwa ikitumia silaha na kupoteza zana nzito katika vita vyake nchini Ukraine, hali inayoilazimisha kutegemea msaada kutoka kwa washirika wake wachache, ikiwa ni pamoja na Korea Kaskazini.