1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJapan

Japan kuchukua Visiwa vya Kuril vinavyozozaniwa na Urusi?

1 Septemba 2023

Wakati vita vya Ukraine vikiendelea, Moscow imekuwa ikitawanya rasilimali zake za kijeshi kwenye mpaka wake wa magharibi. Hilo limezusha hofu ya kuchukuliwa visiwa vya Kuril vinavyozozaniwa kati ya Japan, China na Urusi.

Russland Kanu aus Holz vor dem Ilyinsky (Vulkan) und Kurile See
Visiwa vya KurilPicha: robertharding/picture alliance

Huko mjini Tokyo, misimamo ya kihafidhina inabaini kwamba vita vinavyoendelea vya Ukraine vinaweza kuipa Japan fursa ya kuchukua udhibiti wa kile ambacho Wajapani wanakiita "maeneo ya Kaskazini".

Visiwa vilivyokaa kimkakati na vinavyojulikana kama Visiwa vya Kuril nchini Urusi, vilitekwa na vikosi vya KiSoviet katika siku za mwisho za Vita vya Pili vya Dunia.

Kwa mara kadhaa, Moscow na Tokyo  zimekuwa na mazungumzo kuhusu visiwa vya Iturup, Kunashir, Shikotan na Visiwa vya Habomai lakini zilishindwa kufikia suluhisho na kupelekea pande hizo mbili kutowahi kusaini rasmi mkataba wa amani wa kumaliza vita.

Japan ya sasa haina mpango wa kutumia nguvu za kijeshi kuutatua mzozo huo. Lakini wapo wale wanaotumai kuwa serikali ya Vladimir Putin  inaweza kudhoofika kiasi kwamba mabadiliko fulani yanaweza kupatikana kwa msukumo wa kidiplomasia na kiuchumi.

Licha ya mzozo wa Ukraine kuendelea kiasi kwamba unahatarisha uwezo wa Kremlin wa kudhibiti maeneo hayo ya mbali, mshirika wake China  anaweza pia kuwa na malengo kuhusu visiwa hivyo.

Moscow yakabiliwa na vikwazo

Kunakopatikana visiwa hivyo vinavyozozaniwa vya Kuril

Jarida la kizalendo la Japan la "Sankei Shimbun" lilichapisha makala hivi majuzi zinazoashiria vita vya Ukraine na uasi mkubwa na wa muda mfupi wa mamluki wa Wagner kama viashiria vya kuporomoka kwa utawala wa Urusi.

Kwa mujibu wa jarida hilo, uasi huo ulionyesha kuwa kikosi kidogo cha ardhini kilicho na vifaru na silaha za kupambana na mashambulizi ya angani, kinaweza kusababisha wasiwasi mkubwa kwa ulinzi wa Moscow.

Sankei Shimbun ilihoji ikiwa ndivyo ilivyokuwa kwa mji mkuu Moscow, hii huenda inamaanisha kwamba mipaka ya Urusi kimsingi imesalia bila ulinzi.

Kulingana na tafsiri iliyotolewa na tovuti ya Japan Forward, ni kuwa Japan lazima sasa ijiandae iwapo tu itashuhudia kuanguka au kuporomoka kwa nchi ya Urusi.

Katika makala tofauti, jarida hilo linabaini kwamba uasi zaidi wa kijeshi au vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaweza kuuangusha utawala wa Putin na kusababisha vurugu kote nchini katika wakati ambapo jamhuri za shirikisho zilizopo maeneo ya mbali zina dhamira ya kujipatia uhuru wao kutoka kwa Moscow.

Katika hali hii,  Japan  inaweza kufikia makubaliano na serikali mpya inayosimamia visiwa vinavyozozaniwa, ikitoa usaidizi wa kiuchumi kwa kwa watawala wapya wa Moscow ili kurejesha eneo hilo.

Makala hiyo imeendelea kubaini kuwa, hata kama Putin hatoondolewa madarakani, anaweza kuwa tayari kubadilisha visiwa hivyo kwa msaada wa kiuchumi ikiwa vikwazo vya kimataifa vitasalia kwa miaka mingi.

Enzi za uongozi wa Yeltsin

Rais wa Urusi Boris Yeltsin (kulia) akionyesha ujuzi wake wa muziki pamoja na Waziri Mkuu wa Japan Ryutaro Hashimoto (kushoto) wakati wa mapumziko katika ufukwe wa bahari ya Japan ya Kawana mnamo Aprili 18, 1998.Picha: AFP Kazuhiro Nogi/dpa/picture-alliance

Yoichi Shimada, profesa wa mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Fukui amesema wakati Boris Yeltsin  alipokuwa kiongozi wa Urusi, Japan ilikaribia mno kufikia makubaliano ambayo yangeliwezesha angalau baadhi ya visiwa virejeshwe chini ya udhibiti wa Japan ili kupata msaada wa kiuchumi, lakini ilishindikana.

Shimada ameiambia DW kwamba mfano wa hali hiyo upo na kuongeza kuwa inafikirika kwamba, ikiwa Urusi itaingia kwenye machafuko, yeyote atakayechukua uongozi huko Moscow atarithi matatizo mengi ya kiuchumi na kidiplomasia na hivyo atakuwa tayari kujadili kwa mara nyingine tena maeneo visiwa hivyo vya Kaskazini.

Profesa huyo hata hivyo anaafiki kwamba mpango wowote wa kidiplomasia utakaoanzishwa na Tokyo unaweza kuambulia patupu iwapo China itaamua pia kutumia nguvu za kijeshi katika maeneo 16 ya "Mashariki ya Mbali ya Urusi", hatua isiyoweza kuchukuliwa na Japan.

Imeandaliwa na mwandishi wa DW mjini Tokyo, Julian Ryall

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW