1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan kutoa msaada wa dola bilioni 30 kwa Afrika

27 Agosti 2022

Serikali ya Japan imeahidi kutoa msaada wa dola bilioni 30 kwa ajili ya maendeleo ya Afrika, ikisema kwamba inataka kushirikiana kwa karibu zaidi na bara hilo.

Tunesien, Tunis | Japan - Afrika Gipfel
Picha: Fethi Belaid/POOL/AFP/Getty Images

Akihutubia siku ya Jumamosi katika mkutano wa nane wa kilele kuhusu maendeleo na uwekezaji kati ya Japan na Afrika, unaofanyika kwenye mji mkuu wa Tunisia, Tunis, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida, amesema nchi yake itafanya kazi kuhakikisha usafirishaji wa nafaka kwa njia ya meli kwenda Afrika unafanikiwa, licha ya uhaba wa chakula ulioko ulimwenguni, kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

"Iwapo tutakata tamaa kwa jamii inayozingatia sheria na kuruhusu mabadiliko ya moja kwa moja kwa hali iliyopo sasa kwa kutumia nguvu, madhara yake hayatoenea tu barani Afrika, bali ulimwenguni kote," alisisitiza Kishida.

Kuporomoka kwa uchumi kutokana na janga la virusi vya corona, mzozo wa chakula unaochangiwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa changamoto zinazolikumba nchi nyingi za bara la Afrika na ndiyo zinajadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili.

Fedha kutolewa ndani ya miaka mitatu

Kishida ambaye amehudhuria mkutano huo kwa njia ya video, baada ya kupata maambukizi ya COVID-19 siku chache kabla ya mkutano huo, amesema dola bilioni 30 zitatolewa katika kipindi cha miaka mitatu. Aidha, ameahidi kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya usalama wa chakula kwa uratibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Wakati huo huo, Japan imeipatia Tunisia msaada wa dola milioni 100 kwa ajili ya kupambana na athari za janga la COVID-19. Taarifa hizo zimeripotiwa Jumamosi na shirika la habari la Tunisia, TAP ambalo limemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Yoshimasa Hayashi anayehudhuria mkutano huo wa kilele katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Mkutano huo unafanyika wakati ambapo Urusi na China zikiwa na nia ya kuongeza ushawishi wao wa kiuchumi barani Afrika.

Rais wa Tunisia Kais Saied, akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Yoshimasa Hayashi Picha: Tunisian Presidency/REUTERS

Mkutano huo wa kilele unampa Rais wa Tunisia, Kais Saied jukwaa kubwa la kimataifa, tangu uchaguzi wa mwaka 2019 na unafanyika baada ya kiongozi huyo kulivunja bunge na kuimarisha mamlaka yake kamili yaliyowekwa rasmi kupitia kura ya maoni ya katiba, hatua ambayo wakosoaji wakei wameielezea kama mapinduzi.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika mkutano wa pamoja na waandishi habari na waziri mwenzake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia, Othman Jerandi amerudia kusisitiza kujitolea kwa Tunisia katika demokrasia, jambo ambalo limekuwa likitiliwa mashaka na wakosoaji wa Saied.

Mzozo kati ya Tunisia na Morocco

Mkutano huo wa kilele umeibua mzozo kati ya Tunisia na Morocco, ambayo ilikasirishwa na uamuzi wa Rais Saied kulialika vuguvugu la Polisario linalopigania uhuru wa Sahara Magharibi, eneo ambalo Morocco inalichukulia kama himaya yake.

Morocco na Tunisia zimewaita mabalozi wao kutoka kwenye nchi ya kila mmoja kwa ajili ya mazungumzo. Morocco imesema uamuzi wa kumualika kiongozi wa Polisario, Brahim Ghali umefanywa kinyume na matakwa ya Japan. Hata hivyo, Japan bado haijalizungumzia suala hilo.

Tunisia yenyewe inahitaji msaada wa kifedha wakati ambapo inakabiliwa na mzozo wa fedha za umma. Wiki hii foleni ndefu zilionekana katika vituo vya mafuta huku hukiwa na uhaba wa mafuta, na maduka kuanza kugawa baadhi ya bidhaa.

(AFP, AP, Reuters)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW