Japan, US, Ufilipino zajiimarisha Bahari ya Kusini mwa China
4 Novemba 2023Waziri Mkuu Kishida amyeyazungumza hayo akionesha dhamira yake ya kusaidia kuimarisha uwezo wa kiusalama wa Ufilipino. Mapema Ijumaa, Waziri Mkuu huyo wa Japan na rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Junior walikubaliana kuanzisha mazungumzo kuhusu mkataba wa wanajeshi wa pamoja kwa ajili ya kuongeza ushirikiano wa kijeshi wakati China ikiendelea pia kujiimarisha kwenye ukanda huo.
Soma zaidi: Manila yasema meli za China ziligonga kwa makusudi boti za Ufilipino
Manila na Tokyo ambazo ni washirika wa karibu wa Marekani zimekuwa na msimamo mkali dhidi ya kile zinachokiona kuwa ni tabia ya uchokozi ya meli za China katikati ya mvutano wa miaka mingi juu ya uhuru wa mipaka ya bahari. Beijing imekuwa ikidai kuwa na mamlaka juu ya karibu eneo zima la bahari ya Kusini mwa China yakiwemo maeneo muhimu ya kiuchumi ya Brunei, Indonesia, Malaysia, Ufilipino na Vietnam. Hata hivyo, mnamo mwaka 2016, mahakama ya kudumu ya usuluhishi ilisema kuwa, madai ya China hayana msingi wa kisheria.