1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Japan yaadhimisha miaka 78 ya shambulio la Atomiki Hiroshima

Angela Mdungu
6 Agosti 2023

Japan leo inakumbuka miaka 78 tangu shambulizi la bomu la atomiki lilipoutikisa mji wa Hiroshima. Watu waliohudhuria hafla maalumu ya maadhimisho hayo ni pamoja na waliosalimika kwenye shambulio hilo na ndugu zao.

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida (Wakwanza kulia)
Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida (Wakwanza kulia)Picha: AP/Kyodo News/picture alliance

Wahudhuriaji, wengi wakiwa wamevalia nguo nyeusi, walitumia dakika moja kukaa kimya kama ishara ya kukumbuka tukio hilo katika uwanja wa Peace Memorial. Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia na wawakilishi wa takribani mataifa 111.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida, amelaani vitisho vya Urusi vya kutaka kutumia silaha za Nyuklia akisema kwamba, nchi yake ni taifa pekee lililoathiriwa na matumizi ya silaha za aina hiyo katika vita na kwamba itaendeleza juhudi za kutaka dunia isiyo na silaha za nyuklia.

Soma zaidi: Japan yalaani yalaani vitisho vya Urusi vya nyuklia katika kumbukumbu ya Hiroshima

Kishida hata hivyo amesema, juhudi hizo zinazidi kuwa ngumu kutokana na kuendelea kuwepo kwa mgawanyiko katika Jumuiya ya Kimataifa kuhusu kuachana na silaha za nyuklia na kitisho cha Urusi cha kutumia silaha hizo. Waziri Mkuu huyo wa Japan amesema uharibifu uliotokana na silaha za nyuklia huko Hiroshima na Nagasaki haupaswi kujirudia.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyetoa kauli yake kuhusu kumbukumbu ya Hiroshima amesema kuwa, jumuiya ya kimataifa haina budi kuzungumza kwa sauti moja kuwa matumizi yoyote ya silaha za nyuklia hayakubaliki.   

Maadhimisho miaka 78 ya bomu la Atomiki lililodondoshwa HiroshimaPicha: Keita Iijima/Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Mapema mwaka huu, zaidi ya majarida 100 ya kitabibu duniani kote yalitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka ili kuziangamiza silaha za nyuklia na kutahadharisha kuwa kitisho cha janga la nyuklia ni kikubwa na kinaendelea kuongezeka.

Shambulio hilo la bomu la Atomiki lililodondoshwa na Marekani mwaka 1945 liliwaua maelfu ya wakaazi wa Hiroshima ndani ya sekunde chache, na kufikia mwishoni mwa mwaka huo takribani watu 140,000 walikuwa wamekufa kutokana na mlipuko huo.

Marekani ilifanya shambulizi la pili la bomu la Atomiki siku tatu baadaye katika mji wa Nagasaki kwenye kisiwa cha Kyushu.  Watu wasiopungua 74,000 walikufa katika tukio hilo. Agosti 15, Japan ilijisalimisha na kusababisha vita hivyo vya pili vya dunia kufikia tamati.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW