1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJapan

Japan yaadhimisha miaka 81 ya Hiroshima

6 Agosti 2026

Japan imeadhimisha miaka 81 tangu shambulio la bomu la nyuklia lililouteketeza mji wa Hiroshima wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Manusura wakionya hatua za kuimarisha jeshi zinaweza kuhatarisha amani.

Japan Hiroshima 2026 |
Mwanamke akiwa ameshikilia maua huku akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu wakati wa maadhimisho ya miaka 81 tangu shambulio la bomu la atomiki, katika Bustani ya Kumbukumbu ya Amani ya Hiroshima, mjini Hiroshima.Picha: Issei Kato/REUTERS

Takribani watu elfu 50 kutoka nchi na maeneo 123, wakiwemo manusura wa mabomu ya atomiki, walikusanyika katika Bustani ya Kumbukumbu ya Amani ya Hiroshima, ambapo walikaa kimya kwa dakika moja, saa 2:15 asubuhi kwa saa za Japan, muda halisi ambao Marekani iliangusha bomu la atomiki siku ya tarehe 6 Agosti mwaka 1945.

Katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi, alisisitiza kuwa serikali yake itaendelea kushikilia sera ya kutomiliki, kutotengeneza wala kuruhusu kuingizwa kwa silaha za nyuklia nchini humo. Pia aliahidi kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika juhudi za kuwa na dunia isiyo na silaha za nyuklia na yenye amani ya kudumu.

"Uharibifu uliosababishwa na mabomu ya atomiki ya Hiroshima na Nagasaki, pamoja na mateso yasiyoelezeka waliyoyapitia watu wengi, hayapaswi kamwe kujirudia. Japan inaendelea kushikilia kwa dhati Kanuni zake Tatu za Kutokuwa na Silaha za Nyuklia."

"Kama taifa pekee kuwahi kushambuliwa kwa mabomu ya atomiki wakati wa vita, lina wajibu wa kuendelea bila kuchoka kuongoza juhudi za kufanikisha dunia isiyo na silaha za nyuklia."

Sera ya ulinzi ya Japan

Meya wa Hiroshima, Kazumi Matsui, amewataka viongozi wa dunia kuharakisha juhudi za kutokomeza silaha za nyuklia, akionya kuwa matumizi ya nguvu na kulipiza kisasi yanaweza kuirudisha dunia katika mazingira yaliyosababisha Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Ndege za kivita aina ya F-15 za Kikosi cha Sita cha Jeshi la Kujilinda la Anga la Japan likifanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na ndege ya kimkakati ya Marekani aina ya B-52 katika Bahari ya Japan.Picha: Defense Ministry of Japan/REUTERS

Hata hivyo, kumbukumbu ya mwaka huu imeambatana na mjadala kuhusu sera ya ulinzi ya Japan. Baadhi ya manusura wa mabomu ya atomiki wameeleza wasiwasi wao kuhusu hatua za serikali za kuongeza matumizi ya kijeshi na kuruhusu usafirishaji wa silaha, wakisema zinaweza kuondoa misingi ya katiba ya amani ya Japan iliyojengwa baada ya vita.

Serikali ya Japan inasema hatua hizo ni muhimu ili kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazotokana na China, Korea Kaskazini na Urusi, huku ikisisitiza kuwa sera yake itaendelea kuwa ya kujilinda pekee.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW