Japan yaikosoa sera ya uwekezaji ya China kuelekea Afrika
30 Agosti 2019Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe amewaeleza viongozi wa Afrika kujihadhari na wawekezaji wanaoyatwisha mzigo "mkubwa" mataifa hayo wakati akifunga mkutano wa maendeleo ya Afrika uliofanyika kwa siku tatu mjini Yokohama. Abe amesisitiza kwamba baadhi ya nchi katika kundi la nchi 20 zilizoendelea kiuchumi la G20 ikiwemo China zimejizatiti kuendeleza dhana ya "madeni endelevu".
''Tunapotoa usaidizi kwa mataifa ya Afrika tunahitaji kupanga hatua zetu ili zisiyaingize katika mzigo mkubwa wa madeni. Tunahitaji kufikiria usaidizi unaoweza kuyawezesha mataifa haya maskini kuendelea na kustawi. Tunahitaji kuhakikisha uwazi, uwepo wa uchumi na uendelevu pale tunapoendeleza misaada'', alisema Abe.
Hapo awali taarifa ya pamoja iliyochapishwa baada ya kumalizika mkutano huo wa siku tatu ilisema kuwa "tunaamini kuwa miundombinu bora ambayo inahakikisha upatikanaji wa gharama nafuu ya maisha ni muhimu kwa ajili ya mabadiliko endelevu ya uchumi".
Mkutano huo wa viongozi na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 50 wa nchi za kiafrika na taasisi za kimataifa umefanyika katika kivuli cha China, ambayo imewekeza pakubwa barani Afrika chini ya mradi wake wa ujenzi wa barabara na miundombinu.
Siku ya Alhamisi, Abe alionekana kuikosoa sera ya China akisema "ikiwa nchi washirika wako katika madeni makubwa, hiyo inazuia juhudi za kila mmoja kuingia katika soko". Kauli yake iliibua ukosoaji mkali kutoka kwa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Geng Shuang mjini Beijing aliyeelezea kama "uzushi usio na maana".
Katika mkutano huo, Japan ilijielekeza katika uwekezaji ulio na "ubora" badala ya uwekezaji mkubwa kama wa China ambayo ilitangaza kiasi ya dola bilioni 60 katika miradi ya maendeleo ya Afrika mwaka jana. Japan inapanga kuwapatia mafunzo wataalam katika jumla ya nchi 30 za Afrika ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo katika masuala ya mikopo ya umma na namna ya kukabiliana na majanga. Japan pia ilitilia mkazo uwekezaji katika sekta binafsi badala ya ufadhili wa maendeleo ya serikali.
Tangu mwaka 1993 Japan imeshirikiana na nchi kadhaa za afrika katika kuufanikisha mkutano huo wa TICAD juu ya maendeleo ya Afrika karibu kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kukuza misaada na fursa za kibiashara. Kwenye mkutano uliopita Japan ilitoa ahadi ya dola bilioni 30 kwa ajili ya maendeleo ya Afrika.
AFP