1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan yailaza kameroun bao 1:0 wakati holland yatamba mbele ya Denmark 2:0

14 Juni 2010

Je, mabingwa wa dunia Itali wamepata salamu za Ujerumani jana usiku ?

Cacau -akishangiria bao lake langoni mwa Australia (4:0)Picha: AP

Japan, yailaza Kameroun bao 1:0 na Holland yaipiga kumbo Denmark 2:0.

Simba wa nyika-Kameroun, ambao walilenga shabaha alao kufikia pale walipoacha Itali,1990 walipocheza na mkongwe Roger Milla, (robo-finali), walikiona leo cha mtekakuni kutoka Japan,mjini Bloemfontein. Simba wa nyika hawakuwa na jibu mbele ya mabingwa hao wa Asia.Nahodha Samuel Eto-o hakufurukuta.dakika za mwisho,Kameroun ilikaribia kusawazisha,lakini bahati haikuwa yao leo.

HOLLAND NA DENMARK 2:0

Kabla ya Kameroun na Japan,kuteremka uwanjani,Holland, ikicheza bila stadi wa Bayern Munich,Arjen Robben,alieumia, iliitoa Denmark kwa mabao 2:0.Holland ilitangulia kwa bao lao wenyewe wadeni langoni mwao mara tu baada ya kipindi cha pili.

Wakitamba na Van der Vaart wa Real Madrid, van Persie wa Arsenal London na Sneider wa Inter Milan, Holland,walipania kufuta madhambi ya miaka ya nyuma ya kufika finali mara 2:1974 hapa Ujerumani na 1978 huko Argentina na kuondoka bila ya kombe.

Denmark, ilichachamaa kuzima vishindo vya Oranje,timu ya Taifa ya Holland bila mafanikio.Kwani, wadachi walikuwa na ngome imara ikiongozwa na van Bommel wa Bayern Munich. Holland ilizidi kuwa hatari katika lango la Denmark baada ya Illija anaechezea Hamburg katika Bundesliga,kuitwa uwanjani kuchukua nafasi ya Van der vaart.

Sneider aligonga mwamba wa juu wa lango la Denmark mnamo dakika ya 81 lakini hodi zake hazikuitikiwa.Haukupita muda,lakini, Illija aligonga nae mwamba wa lango la Denmark na uliporudi, Kyut akalifumania lango la Denmark kwa bao la pili na kukamilisha ushindi. Holland, inasubiri majibu ya simba wa nyika Kamerun na Japan ikiwa kileleni mwa Kundi hili:

ITALI NA PARAGUAY:

Leo usiku baada ya Kameroun na Japan ,kuondoka uwanjani, itakua zamu ya mabingwa wa dunia-Itali kutetea taji lao.Maadui zao jioni hii, ni Paraguay.hili litakuwa Kombe la mwisho la dunia kwa stadi wao Gennaro Gattuso katika kikosi cha waazzuri.Wakiongozwa tena na kocha Marcello Lippi aliewatawaza mabingwa wa dunia,miaka 4 iliopita hapa Ujerumani, waazzuri wanadi watarudi nalo tena nchini Itali.Kwani, "mramba asali,harambi mara moja".

UJERUMANI:

Ujerumani jana, ilianza Kuania Kombe hili la dunia 2010 huko Durban,kwa kishindo.Walicheza kwa ari,kasi na kutamba mbele ya Kangaroo wa Australia.

Kufuatia ushindi wao wao wa mabao 4:0 dhidi ya Australia, nahodha wa Ujerumani,Philipp Lahm, alisema :

"Muhimu ni kuwa, tumeshinda mpambano wetu wa kwanza .Kuwa tuna nafasi ya kutamba ,hayo tulijua kabla kuanza kwa Kombe hili la dunia na leo, timu yetu imethibitisha hayo.Lakini bado kuna safari ndefu ya kwenda.Sasa tujishughulishe na mechi ijayo dhidi ya Serbia."

Mazumari ya Vuvuzela,yanayohanikiza uwanja mzima hata kuwa taabu kwa wachezaji kuwasiliana na kuzika hata matangazo ya TV,ubishi umezuka, iwapo yapigwe marufuku au la:

"Wanataka tuache kuyapuliza.Kwanini ?

Hili ni Kombe la Dunia la Afrika.Kwahivyo, ni Kombe letu.Tunabidi kulipuliza tena na tena hadi mwisho wa mashindano."

Na huko Tanzania,mashabiki wa dimba huenda wakashindwa kuangalia baadhi ya mechi za Kombe la dunia.Kisasa nini ? kama kawaida:umeme.Kuna mpango wa kuanzisha mgao wa umeme.Lakini,wanauliza mashabiki:kwanini TANESCO inafanya wakati huu wa Kombe la dunia ?

George Njogopa ,mwandishi wetu mjini Dar-es-salaam,anaripoti kwamba, mashabiki wa dimba wamekasirishwa nchini tanzania kwa kusikia Kampuni la Umeme la TANESCO linapanga umeme wa mgao.Wanahofia watashindwa kujionea Kombe la Dunia linavyoendelea huko Afrika kusini.Kwanini,wauliza mashabiki,umeme wa mgao tena nyakati za usiku unapangwa wakati huu wa kombe la dunia ?

Eric Ponda,muandishi wetu huko Kenya, ametuarifu huko kuna tatizo jengine kabisa : Makampuni mengi yanalalamika kwamba, mashabiki wengi ama hawaendi makazini au wale wanaokwenda, huzungumza Kombe la dunia tu .Wengine, wanasinzia.Sababu ni Kombe la dunia.

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE/AFPE

Uhariri: Abdul-Rahman