1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan yamuaga Shinzo Abe

27 Septemba 2022

Maelfu ya raia nchini Japan wanamuaga aliyewahi kuwa waziri mkuu Shinzo Abe katika mazishi ya kitaifa yaliyokabiliwa na ukosoaji mkali juu ya fedha nyingi zilizotumika kwenye maandalizi ya mazishi yake ya kitaifa.

Japan | Staatsbegräbnis Shinzo Abe
Picha: Yuichi Yamazaki/AFP/Getty Images

Waziri Mkuu wa sasa wa Japan Fumio Kishida amemuaga mtangulizi wake, aliyemtaja kama mtu shujaa, mwaminifu na aliyekuwa na huruma. 

Mji mkuu Tokyo, umefurika waombolezaji karibu 4,300 kutoka ndani na nje ya Japan hii leo ili kumuaga Shinzo Abe katika mazishi ya kitaifa. Mjane wake bi, Akie Abe aliyevalia nguo nyeusi na mkono akiwa ameshikilia chungu kilichokuwa na majivu ya mwili wa mumewe, aliingia katika ukumbi wa Nippon Budokan uliokuwa umejaa waombolezaji, na mbele ya ukumbi huo kukiwa na picha kubwa ya Abe, aliyeuawa kwa risasi mapema mwezi Julai.

Pembezoni mwa ukumbi huo, pana bustani kubwa, ambako waombolezaji pia waliweka mashada ya maua na kufanya sala mbele ya meza mbili zilizoandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo tangu mapema asubuhi ya leo.

Soma Zaidi: Viongozi waomboleza kifo cha waziri Mkuu mstaafu Shinzo Abe

Waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida amemtaja mtangulizi wake kama mtu shujaa na aliyejwa na huruma.Picha: Kiyoshi Ota/REUTERS

Waziri mkuu wa sasa Fumio Kishida, alitoa heshima zake za mwisho kwa mtangulizi wake, aliyemuita mtu jasiri, mwaminifu na aliyejawa na huruma. Aliposoma wasifu wake, Kishida, pia alisema anaamini iwapo Abe, waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Japan, angekuwa mzima angeweza kuendelea kuwa dira ya Japan kwa hata miongo miwili ijayo.

"Ulikuwa mamlakani kwa muda mrefu zaidi katika historia ya katiba yetu. Lakini historia itakukumbuka zaidi kwa mafanikio yako, kuliko muda uliokaa madarakani." alisema Kishida.

Pamoja na Kishida, wawakilishi wengine wa serikali, bunge na mahakama walitoa heshima zao za mwisho. Aidha, mamia ya wawakilishi kutoka nje ya Japan pia walihudhuria mazishi hayo ikiwa ni pamoja na makamu wa rais wa Marekani Kamala Harris na waziri mkuu wa India, Narendra Modi.

Lakini kwa upande wingine, maombolezo ya kitaifa nchini humo yalichochea maandamano ya waliopinga vikali mazishi ya kitaifa ya Abe wakisema kwamba waziri mkuu wa sasa Fumio Kishida ambaye pia anatokea chama cha Abe cha Conservative hakuwa na haki ya kumzika Abe kwa heshima hiyo ya kitaifa.

Baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakipinga mazishi ya kitaifa ya Shinzo Abe wakidhibitiwa na polisiPicha: Minoru Iwasaki/Kyodo News/AP/dpa/piture alliance

Hata hivyo Kishida alidai kwamba Abe anastahili mazishi hayo ya kitaifa na hasa kwa kuzingatia kwamba ndiye kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi. Kiasi maafisa polisi 20,000 wamesambazwa kusimamia usalama wakati huu wa mazishi.

Na hata baadhi ya waombolezaji waliosimama kwenye mstari kwa muda mrefu wakisubiri kutoa heshima zao za mwisho, walimzungumzia kiongozi huyo kuwa alikuwa mtu aliyejishusha na kuona ni sawa kupewa mazishi kama hayo. Yoshiko Yokota, mmoja ya waombolezaji hao alisema alisikia mwili umekufa ganzi baada ya kusikia Abe amepigwa risasi. Akasema, hadhani kama Japan itakuja kupata kiongozi mwingine wa aina ya Abe.

Shinzo Abe, aliuawa kwa kupigwa risasi na mwanajeshi mstaafu, Julai 8 wakati akiwa kwenye kampeni katika jiji la Nara. Muuaji wake anasema hakumuua Abe kutokana na mtizamo wa kisiasa, ila ni kutokana na ghadhabu aliyonayo dhidi ya kiongozi wa kidini wa Kanisa la Umoja na lenye utata la Korea, mwenye mahusiano na Abe.

Soma Zaidi:Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe atangaza kujiuzulu 

Mashrika: DPAE/AFPE