1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

A return to whaling?

Josephat Nyiro Charo13 Juni 2014

Makundi ya wanamazingira wamekasirishwa na nia ya Japan kupuuzilia mbali uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, na kutumia mpango wake wa utafiti wa kisayansi kuhalalisha uvuvi wa nyangumi.

Walfang Japan
Picha: picture-alliance/dpa

Migahawa kote nchini Japan inashiriki kwenye kampeni ya "Wiki ya Nyangumi" kuunga mkono ulaji wa nyama ya nyangumi, huku waandaaji wa kampeni hiyo iliyoanza Jumatatu wiki hii, na viongozi wa serikali wakisisitiza kwamba kula bidhaa zinazotokana na uvuvi wa nyangumi kwa ajili ya utafiti wa kisayansi ni halali na ni sehemu muhimu ya utamaduni wa kitaifa wa nchi hiyo. Wanamazingira wamekasirishwa na mpango wa Japan kutafuta mbinu mpya za kuhalalisha uvuvi wa nyangumi kwa ajili ya biashara.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amekwenda mbali kusema uvuvi wa nyangumi ni muhimu mno kwa Japan kiasi kwamba anapanga kuimarisha kampeni kuwashawishi wapinzani wa kimataifa na kuanza tena uvuvi wa nyangumi kwa ajili ya biashara katika bahari ya Antarctic.

Tangazo hilo limemuweka waziri mkuu huyo wa Japan katika mkwaruzano na mashirika ya kuyalinda mazingira, ambayo yamekuwa haraka kumtaka aheshimu uamuzi wa mwezi Machi mwaka huu uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, mjini The Hague, Uholanzi. Katika uamuzi huo Japan ilitakiwa sharti ikomeshe kuwaua nyangumi katika bahari ya Antarctic, kwa sehemu kwa sababu uwindaji huo unawezesha kupatikana data zinazoweza kupatikana kupitia njia nyingine za utafiti zisizo hatari kwa maisha ya nyangumi.

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo AbePicha: Reuters

Kesi ya muda mrefu

Kesi hiyo iliyodumu miaka minne iliwasilishwa na serikali za Australia na New Zealand kwa misingi kwamba hatua ya Japan kuwaua mamia ya nyangumi kila mwaka zaidi inaonekana kama uvuvi wa nyangumi kwa ajili ya biashara uliojificha, kwa kuwa bidhaa zinazotokana na utafiti huo huishia kuuzwa katika maduka makubwa na katika migahawa ya Japan.

Australia na New Zealand zilighadhabishwa pia na hatua ya Japan kukataa katakata kulitambua eneo la kimataifa la hifadhi ya nyangumi katika bahari ya Antarctic. Hata hivyo waziri mkuu Abe anaonekana kutotingishika kabisa na uamuzi wa mahakama ya ICJ, upinzani wa serikali nyingine na ghadhabu ya mashirika ya kuyalinda mazingira.

Akizungumza mbele ya tume ya bunge mjini Tokyo mnamo Juni 9 Abe alisema, "Huku tikiheshimu sheria ya kimataifa na taarifa sahihi za kisayansi, ni muhimu kuendelea na uvuvi wa nyangumi kwa ajili ya utafiti wa kisayansi ili kupata data zinazohitajika kuhusu idadi ya nyangumi ili kuweza kusimamia kiurahisi raslimali za mamalia ili kuweza kuangalia upya uwezekano wa kuanza tena uvuvi wa nyangumi kwa ajili ya biashara."

Waziri mkuu Abe aidha alisema raia wa kigeni mara kwa mara wanakosa kuuelewa utamaduni wa Wajapani na kusisitiza kwamba wavuvi wa nyangumi huonyesha heshima yao kwa viumbe wanaowaua kwa kufanya ibada ya kidini kila mwaka.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa New Zealand, Murray McCully, amesema kauli ya Shinzo Abe inatia wasiwasi, huku waziri wa mazingia wa Australia, Greg Hunt, akisisitiza upinzani wa nchi yake dhidi ya uvuvi wa nyangumi kwa ajili ya biashara na utafiti hatari wa kisayansi.

Maandamano ya wanaharakati kupinga uvuvi wa nyangumi mjini TokyoPicha: Toshifumi Kitamura/AFP/Getty Images

Uvuvi kuanza tena mwakani?

"Japan imeanzisha mchakato kupata ridhaa kutoka kwa kamati ya kimataifa ya uvuvi wa nyangumi, IWC, kuanza tena uvuvi wa nyangumi katika bahari ya Antartic, ikiwezeka mapema mwakani," amesema Joji Morishita, Kamishna wa shirika la IWC, wakati alipozungumza na DW.

"Nahisi uamuzi wa sasa wa mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, una manufaa kwa Japan. Mahakama inachukulia tu kwamba Japan pengine itauangalia upya mpango wake wa utafiti. Na hiyo ni sawa kwa Japan kupendekeza mpango mpya unaojumuisha uvuvi wa nyangumi ili mradi unakidhi au kuzingatia msingi na masharti ya uamuzi wa mahakama ya ICJ."

Kamishna Joji ameonya dhidi ya kuingiliwa utamaduni wa Wajapani. "Hata kama baadhi ya nchi zinafikiri kuwa nyangumi ni viumbe maalumu au watakatifu, ili mradi wanatumiwa kwa uangalifu ili wasitoweke, mtizamo huo haupaswi kulazimishwa kwa watu wengine wanaotaka kutumia raslimali ya nyangumi. Kwa mfano kama watu nchini India watajaribu kulazimisha jinsi wanavyowachukulia ng'ombe kwa nchi nyingize za dunia na kupigania marufuku ya kula bidhaa za McDonalds au mikate ya nyama - hambuger, kipi kitakachotokea?"

Joji amesema Japan itawasilisha mpango mpya wa utafiti mwaka ujao 2015. Joji pia amesema ingawa haikubaliani na uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, Japan ni nchi inayotii sheria.

Mwandishi: Josephat Charo/Dominguez, Gabriel

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman