Japani kuipa Afrika msaada wa dola bilioni 32
1 Juni 2013Waziri Mkuu wa Japani Shinzo Abe ametoa ahadi ya masaada huo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa siku tatu kuhusu maendeleo ya Afrika unaofanyika katika mji wa Yokohama nchini Japani.
Msaada huo unajumuisha utowaji wa yeni bilioni 650 kwa ajili ya mikopo katika ujenzi wa miundo mbinu na mpango wa mafunzo kwa ajili ya vijana wa Afrika.Mpango huo utawapa fursa vijana 1,000 wa Kiafrika kujifunza katika vyuo vikuu vya Japani na kujifunza kazi katika makampuni ya Kijapani.
Abe amesema kuendeleza rasilmali ya nguvu kazi, huduma muhimu za matibabu na kukuza sekta ya kilimo ni mambo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Afrika.Amesema kile inachokihitaji Afrika ni uwekezaji katika sekta ya binafsi ambapo ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi utatoa fursa ya kufaidikia na uwekezaji huo. #
Shauku ya Japani kuwekeza Afrika
Tangazo lake hilo linaonyesha shauku ya Japani kuchuana na China katika masuala ya kuipatia msaada na kuwekeza Afrika bara lenye utajiri wa mali asili.
Licha ya uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Japani na Afrika,umuhimu wa Japani kwa bara hilo umekuwa ukipunguwa kulinganishwa na ule wa China ambapo kiwango chake cha biashara na Afrika ikilinganishwa na Japani ni mara tano zaidi na mara nane zaidi katika uwekezaji wa moja kwa moja.
China huwa haitangazi kiwango cha msaada wake wa maendeleo lakini repoti zinadokeza kwamba hutoa hadi dola bilioni mbili kila mwaka.Kiwango ilichotangaza Japani Jumamosi kimepita sana kiwango hicho cha China.Uhusiano wa Japani kwa Afrika unatofautiana na mataifa mengine kwa bara hilo amesema Abe katika kauli inayoonekana kuikusudia China.
Serikali ya China imekuwa ikishutumiwa na baadhi ya nchi kwa kile mara nyengine kinachoonekana kuwa inachofanya barani humo ni kunyakua ardhi na kutohusisha uwekezaji na masharti ya kuboresha haki za binaadamu au kuzitaka nchi zinazopokea misaada kuwa wazi zaidi.
Waziri Mkuu huyo wa Japani amesema mali asili ya Afrika inasababisha kuwepo kwa fursa muhimu za biashara kwa nchi yenye uhaba mkubwa wa mali ghafi kama Japani lakini nchi hiyo haitotafuta na kuchimba rasilmali hizo kwa sababu tu ya kuzileta Japani.
Msaada ukuze uchumi
Amesema wataisaidia Afrika ili kwamba mali asili za Afrika zisababishe ukuaji wa kiuchumi wa bara hilo.Abe pia ametoa wito wa kuanzishwa kwa kanuni za uwazi katika biashara na kuimarisha usalama kwa Wajapani wanaoishi na kufanya kazi barani Afrika.Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ameitaka Japani kuimarisha uwepo wake barani Afrika.
Akizungumza katika kikao cha ufunguzi wa mkutano huo wa Kimataita wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD), amesema ni jambo la kushangaza kwamba kuhusika kwa Japani katika fani ya uwekezaji barani humo kuko nyuma kabisa kuliko vile ingelipaswa iwe kwa hivi sasa kulinganisha na nchi mpya ambazo hivi sasa zimekuwa zikijihusisha katika harakati nyingi.
Afrika lazima ibadilike
Suala la uwekezaji katika sekta ya binafsi limekaribishwa na wajumbe ambapo Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema uchumi wa bara hilo hauna budi kuendelezwa. Amesema Afrika lazima ibadilike kutoka kuwa na uchumi unaotegemea usafirishaji nje wa bidhaa na kuwa na uchumi wenye kuongozwa na viwanda pamoja na kutanuwa njia mbali mbali za kiuchumi.Zuma amesema mambo matatu ni muhimu kufikia maendeleo nayo ni : kuunganisha masoko, kuendeleza viwanda na kuendeleza miundo mbinu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pia amehudhuria mkutano huo ambapo amesema malengo ya mkutano huo ni malengo ya Umoja wa Mataifa.Amesema wamejizatiti kuisaidia Afrika itimize Malengo ya Maendeleo ya Milenia yakiwemo kutokomeza umaskini na njaa ifikapo mwaka 2015.
Mkutano huo wa TICAD utaendelea kufanyika hadi Jumatatu ambapo wajumbe kutoka zaidi ya nchi 50 za Afrika watakuwa wanajadili na Japani jinsi ya kuhakikisha ukuaji wa uchumi endelevu barani Afrika.Mkutano huo unaandaliwa kwa ushirikiano wa mashirika ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa,Benki ya Dunia na kwa mara ya kwanza Umoja wa Afrika.Mkutano huo umekuwa ukifanyika kila baada ya miaka mitano nchini Japani tokea ulipoanzishwa hapo mwaka 1993.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP,dpa
Mhariri :Caro Robi.