1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgombea wa Ukansela wa CDU Armin Lachet atakiwa aachie ngazi

Zainab Aziz Mhariri: Mohammed Khelef
27 Agosti 2021

Wakati umebakia mwezi mmoja tu kufanyika uchaguzi mkuu nchini Ujerumani, kambi ya wahafidhina imeendelea kuanguka katika umaarufu. Anayebebeshwa lawama ni mgombea wake wa ukansela Armin Laschet.

Deutschland | Zentraler Wahlkampfauftakt von CDU und CSU
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Wanachama wengi wa chama cha Armin Laschet cha Christian Democratic Union CDU, sasa wanajiweka kando na mgombea wao na wengine wanataka ajiuzulu. Alipochaguliwa kuwa mgombea wa kambi hiyo ya wahafidhina, chama cha CDU kilikuwa kinaongoza katika kura za maoni lakini hali imebadilika na sasa chama hicho kinarudi nyuma. Kulingana na utafiti wa maoni, mgombea ukansela kwa tiketi ya chama cha Social Democratic SPD, Olaf Scholz ambye kwa sasa ni waziri wa fedha wa Ujerumani yupo kidedea akifuatiwa na mgombea wa chama cha kijani Annalena Baerbock.

Mgombea wa Ukansela wa chama cha CDU Armin LaschetPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Hata ikiwa chama cha CDU kitashika nafasi ya pili au ya tatu hayo yatakuwa maafa kwa kambi ya wahafidhina. Mambo sasa ni mabaya zaidi kwa Armin Laschet ambaye ni waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia lenye watu wengi zaidi kuliko jimbo jingine lolote la Ujerumani. Waliokuwa wanamuunga mkono wanamtaka aachie ngazi.

Mwenyekiti wa chama ndugu cha CSU katika wilaya ya Nuremberg kwenye jimbo la Bavaria Andre Freud amesema mambo hayaendi vizuri kwa kambi ya  wahafidhina na kwamba hakuna matumaini ya hali ya kambi hiyo kubadilika. Kampeni ya bwana Laschet imekuwa inaandamwa na mushkeli. Alinaswa kwenye camera akiwa anacheka kwenye eneo lililokumbwa na maafa ya mafuriko hivi karibuni. Na wala hakuwa la kujibu alipoulizwa juu ya mipango ya baadae. Na jimbo lake la North Rhine Westphalia linaongoza kwa maambukizi  ya virusi vya corona.

Mgombea wa Ukansela wa chama cha SPD Olaf Scholz Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Mwenyekiti wa CSU wa mji wa Nuremberg bwana Freud amesema mgombea ukansela huyo wa kambi ya wahafidhina anazingatiwa kuwa mtu asiyekuwa na hisia sahihi. Mwenyekiti huyo amefafanua kwa kueleza  kwamba hata ikiwa bwana Laschet hayuko hivyo, watu wengi wanamzingatia kuwa hivyo. Andre Freud  amemtaka bwana Armin Laschet aachie ngazi.

Baadhi ya wanahcma wa kambi ya wahafidhina wanataka nafasi ya Laschet ichukuliwe na mwenyekiti wa chama cha CSU, Markus Söder ambaye ni Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria la kusini mwa Ujerumani.

Vyanzo:/RTRE/https://p.dw.com/p/3zX9h

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW