Je Bayern munich itateleza tena leo ?
10 Aprili 2009Katika Bundesliga-macho yakodolewa mpambano wa leo kati ya mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich na Einrtrach Frankfurt-je, Munich itavumilia pigo jengine baada ya lile la mabao 4 iliopata huko Barcelona ?FC Liverpool, yaweza kuparamia leo kileleni mwa ngazi ya Ligi ya Uingererza, ikitamba mbele ya Blackburn Rovers.Katika Kombe la Ulaya ya la UEFA, nusu-finali itakuwa kati ya timu 2 pekee za Ujerumani na 2 pekee za Ukraine.
Mabingwa wa Afrika Misri ,wakijiandaa kwa Kombe la mashirikisho linalofungua pazia la Kombe lijalo la dunia huko Afrika Kusini, 2010,wamepanga kucheza na mabingwa wa Asia-Iraq kabla kuanza kwa kombe hilo.
Bundesliga na Premier League:
Hii haikuwa wiki ya kufurahisha kwa mabingwa wa Ujerumani: Bayern Munich na kocha wao Jurgen Klinsmann.Baada ya kuzabwa mabao 5-1 na Wolfsburg, Jumamosi iliopita, Munich walifedhehshwa kati ya wiki na viongozi wa Ligi wa Spain ,FC Barcelona pale akina Lionel Messi wa Argentina na Samuel Eto -o wa Kamerun waliponguruma katika lango lao na kuwakatisha tamaa ya taji jengine la Ulaya: Ni kwa jicho hilo changamoto uwanjani Olympic Arena mjini Munich inaangaliwa.Je, Munich itateleza mbele ya Frankfurt ?:
Tukiorejea mkasa wa kuaibishswa kati ya wiki hii mabingwa wa Ujerumani ,Bayern Munich na FC Barcelona:Tumu hii ikiongozwa na kocha Jurgen Klinsmann ilifunga safari hadi Barcelona ,mji mkuu wa Catalonia ikitumai kufuta madhambi ya mabao 5-1 waliozabwa na viongozi wapya wa Ligi ya Ujerumani Wolfsburg jumamosi iliopita.LKakini baada ya kupita dakika 9 tu, mkamerun Samuel Eto-o alimtupia pasi maridadi muargentina Lionel Messi kuvunja tumbuu ya lango la mabingwa hao wa Ujerumani.
Messi hakuonesha ni mwizi wa fadhila, kwani dakika 3 baadae nae alirudisha shukurani kwa Samuel Eto-o alipomtengezea nafasi ya kutia nae bao la pili.Halafu Barcelona ilibidi kungoja hadi dakika 7 kabla kipindi cha mapumziko kupiga misumari mengine 2 katika jeneza la mabingwa wa ujerumani msimu huu wa champions league.Watatu ulipigwa na Lio nel Messi kabla mfaransa Thierry Henry,kuizika Munich kabisa katika kaburi iliochimbiwsa mjini Barcelona.
Kama Barca, kocha wa Chelsea ,mdachi Guus Hiddink alikuwa na sababu ya kufurahia,kwani kikosi chake -Chelsea kiliambia Liverpool iliotia bao la kwanza, "kutangulia jamani si kufika."
Chelsea iliikomea Liverpool mabao 3-1 na sasa wana nafasi ya kuiacha Liverpool nyuma katika champions League.Kwa kweli, muivory Coast didier drogba angesawazisha haraka bao la Liverpool baada ya mwenzake Salomon Kalou kumchenga Fabio Aurelio na halafu kumtupia yeye dimba. Drogba alipoteza nafasi nyengine wazi katika dakika ya 28,lakini pale Ivanovic alipoutia kichwa mpira hadi wavuni mwa Liverpool, kila kitu kilirudi kuwa sawa kwa Chelsea.
Na kama wasemavyo: "Mramba asali,harambi mara moja". Ivanovic , akalifumania tena lango la Liverpool kwa bao jengine lililofananay sana kama lile lake la kwanza.
Msumari wa mwisho katika jeneza la Liverpool alikuja nao Drogba akifuta madhambi aliofanya awali.Kwa ushindi wa mabao 3-1 ,Chelsea, imetoa salamau kwa Liverpool na Manchester United kwamba, wasiisahau bado ihayi-licha ya kuwa ipo pointi 4 nyuma ya viongozi wa Ligi- Manu.
Iwapo Liverpool,itafuta mabao hayo 3 ya Chelsea katika duru ya pili, ni swali la kusubiri kuona.Wazi ni kwamba,Chelsea imeshatia mguu moja katika nusu-finali ya Champions League.
Katika kinyanganyiro cha kombe la ulaya la UEFA-kombe la shirikisho la dimba la ulaya, nusu-finali ya kombe hilo kufuatia changamoto za kati ya wiki hii,yamkini ikawa kati ya timu 2 pekee za Ujerumani na za Ukraine:
Timu 2 za Bundesliga-Hamburg na Bremen zilitamba kati ya wiki: Hamburg iliikomea Manchester City mabao 3-1 wakati Bremen iliitimua nje Udinese ya Itali pia kwa mabao 3-1.Sasa timu hizo mbili zimeweka miadi ya kupambana katika nusu-finali ikiwa zitasonga mbele.
Kwa upande wapili Shakhtar Donetsk ya Ukraine ilishinda kwa mabao 2-0 nyumbani ilipopambana na Olympique Marseille ya Ufaransa huku wenzao Dynamo Kiev wakifaulu kutoka sare 0:0 na Paris St.Germain.Pia timu hizi mbili zitaonana pia katika nusu-finali.
Muandishi:Ramadhan Ali
Mhariri: Mohammed Abdulrahman