1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Chanjo zinatoa kinga asilimia ngapi mwilini?

21 Julai 2021

Watu 259 wamefariki dunia nchini Uingereza kutokana na aina mpya ya kirusi cha delta. Watu 116 kati ya waliofariki walikuwa wamepata chanjo kamili. Swali ni je chanjo bado inatoa kinga dhidi ya kirusi cha delta?

England London | Massenimpfung im London Stadium
Picha: Maciek Musialek/NurPhoto/imago images

Utafiti umeonesha kuwa kufikia sasa, hakuna chanjo iliyoidhinishwa kutoa kinga ya asilimia 100 dhidi ya maambukizo ya virusi vya corona tangu kuanzishwa kwa chanjo hizo.

Watu waliopata chanjo hasa wale wanaougua maradhi mengine bado wanakabiliwa na athari ya maambukizo na katika hali mbaya zaidi vifo. Hata hivyo kiwango cha sasa cha vifo nchini Uingereza bado ni kidogo licha ya kuongezeka kwa viwango vya maambukizo.

Katika maelezo ya video aliyotoa mnamo mwezi Juni, Christian Drosten mmoja wa wataalamu wakuu wa virusi nchini Ujerumani, amesema kuwa kuna visa ambapo watu waliopata chanjo mara mbili pia walikufa. Amependekeza kwamba wataalamu waangalie kwa makini chanzo cha vifo hivyo na jinsi utambuzi ulivyofanywa.

Idadi kubwa ya watu waliopata chanjo miongoni mwa waliokufa huenda ikawa ilitokana na hali kwamba takriban nusu ya idadi ya watu sasa wamepata chanjo ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba idadi jumla ya vifo inapungua.

Zoezi la utoaji chanjo ya covid-19Picha: Edy Susanto/ZUMAPRESS/picture alliance

Kwa kuongezea, takwimu za shirika la PHE zinaonesha kuwa watu 116 kati ya 118 waliokufa walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 50.

Peggy Riese, mwanasayansi katika kituo cha utafiti wa maambukizo cha Helmholtz, alielezea hali hiyo kwa usaidizi wa mfano mwafaka. Amesema kuwa iwapo asilimia 100 ya idadi ya watu imepata chanjo, basi idadi ndogo ya watu waliopata chanjo pia wanakufa. Riese ameimbia DW kwamba hii haimaanishi kuwa chanjo hiyo sio salama lakini haitoi kinga ya asilimia 100.

George Behrens, profesa katika kitengo cha magonjwa ya viungo na misuli katika chuo cha mafunzo ya matibabu cha Hannover, ameiambia DW kwamba idadi ndogo ya watu waliopata chanjo huenda wakafariki iwapo chanjo zao zitakosa kufanya kazi kutokana na uwepo wa vizuizi vya kinga kama wale waliopandikizwa katika sehemu moja ama nyingine ya mwili.

Behren amesema kuwa athari ya chanjo hizo pia hupungua baada ya miezi kadhaa huku baadhi ya watu bado wakiathirika vibaya.

Chanjo hizo zinatoa kinga nzuri lakini Behren pia ameonya kuwa hakuna chanjo inayoweza kutoa kinga ya asilimia 100.

Utafiti uliofanywa na kitengo cha takwimu za biologia cha baraza la utafiti wa matibabu nchini Uingereza katika chuo kikuu cha Cambridge, unapendekeza kuwa chanjo zimezuia takriban maambukizo milioni 7.2 na vifo elfu 27 nchini Uingereza pekee.

Chanjo ya coronaPicha: Giorgos Kontarinis/ANE Edition/imago images

Wataalamu wote waliohojiwa na DW walielezea matumaini katika ufanisi wa chanjo hizo dhidi ya kirusi cha delta.

Friedmann Weber, mtaalamu wa virusi katika chuo kikuu cha Giessen ameeleza kuwa chanjo hizo ni nzuri na kinga mwili ya watu waliopokea chanjo zote mbili na kusubiri kwa muda ni ya kiwango cha juu cha wastan ama cha juu kwa watu ambao wamepata kinga mwili baada ya maambukizo.

Aina mpya ya virusi hutokea wakati virusi vinapobadilisha mfumo wake . Weber amesema kuwa aina mpya ya virusi huenda ikatokea kwa muda na kuongeza kuwa aina hiyo mpya ya virusi itandelea kutokea hadi idadi kubwa ya watu itakapopata chanjo. Lakini hata baada ya hilo, wataalamu hao wa virusi hawachukulii kuwa chanjo zitaacha kufanya kazi mara moja.

Kufikia sasa, chanjo zimethibitisha kufanya kazi dhidi ya aina mpya za virusi zilizojitokeza na kuibua wasiwasi. Riese amesema kuwa itabidi chanjo hizo zifanyiwe marekebisho zinapopoteza ufanisi wake. Hata hivyo ameonya kuwa hakupaswa kuwa na haraka  na kwamba chanjo haitengenezwi kwa haraka. Iwapo aina mpya itajitokeza kila baada ya miezi minne, utengenezaji wa chanjo utakabiliwa na changamoto kubwa.