Je China itaondolewa vikwazo vya silaha na Umoja wa Ulaya?
15 Aprili 2005Mawaziri wa mambo ya nje kutoka mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Luxembourg kuzungumzia masuala nyeti kadha wa kadha kuanzia ya Mashariki ya Kati hadi matatizo yanayoikabili jamhuri ya zamani ya Usovieti ya Russia.
Lakini masuala ya mataifa hayo 25 wanachama wa Umoja wa Ulaya juu ya mpango wa kuindolea serikali ya China vikwazo vya silaha vilivyowekwa kuanzia mwaka wa 1989 kufuatia mauaji ya halaiki yaliofanyika katika uwanja wa Tianamen nchini humo yanaelekea kuwasha moto katika mjadala.
Kwa mujibu wa mjumbe mmoja suala hilo haliwezi kuepukwa kuzungumziwa katika kikao hicho cha siku mbili kinachofanyika huko Senningen Chateau kaskazini mwa mji wa Luxembourg.
Lakini suala hilo hata hivyo limefanywa kuwa gumu zaidi baada ya China mwezi uliopita kupitisha sheria yake inayozuia kujitenga kwa jimbo lolote la nchi hiyo na inayokubali China kutumia nguvu dhidi ya Taiwan iwapo itajitenga.
Kwa upande wake Washington imeonya kwamba iwapo vikwazo vya silaha vitaondolewa dhidi ya serikali ya China basi huenda uamuzi huo ukachangia katika kutatiza suala la uwezo kati ya Beijing na Taipei.
Na iwapo suala hilo halitapatiwa suluhisho ifikiapo mwezi Juni basi huenda ikaongeza mtafaruku na huenda likasalia bila kutatuliwa hadi mwaka 2006 baada ya kumalizika kwa kipindi cha miezi sita ya Uingereza kuwa rais wa Umoja huo kuanzia mwezi July.
Hata na hivyo hakuna uamuzi wowote unaotarajiwa kufikiwa katika kikao hicho cha Luxembourg kufuatia kutokuwepo kwa waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jack Straw ambaye hatoweza kuhudhuria kikao hicho kufuatia wimbi la Kampeini ya uchaguzi mkuu unaokaribia nchini mwake.
Msemaji wa mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana amesema kabla ya mazungumzo hayo ya Luxembourg ambayo yanafikiriwa kuindolea China vikwazo, tayari sheria ya China ya inayozuia kujitenga kwa jimbo lolote lake pamoja na masuala mengine nchini humo imeathiri kwa kiasi fulani uamuzi huo.
Ufaransa pamoja na Ujerumani wameupigia debe sana uamuzi wa kutaka kuondolewa vikwazo vya silaha China zikipuzilia mbali lawama kwamba zinapuuza masuala muhimu kwa kuipendelea China.
Ikizungumzia wasiwasi wake Umoja wa Ulaya umesisitiza kwamba utaweka sheria yake juu ya uuzaji wa silaha huku pia ukisema utaisukuma China kuchukua hatua juu ya suala la haki za binadamu kabla ya kuondolewa vikwazo vya silaha.
Lakini hapo jana Kansella wa Ujerumani Gerhard Schroeder ameupinga vikali mpango huo akisema China imejirekebisha kwa kiasi kikubwa tangu kuwekewa vikwazo hivyo.
Mbali na sheria hiyo ya China inayozuia kujitenga kwa jimbo lolote lake, hofu imezuka kati ya China na Japan kufuatia mizozo juu ya kuhusika kwao wakati wa vita vya zamani na uamuzi wa Tokyo wa kuruhusu machimbo ya gesi na mafuta katika sehemu za maji wanazogombania.
Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Joska Ficher amesema hapo jana kwamba Umoja wa Ulaya hautaendelea na mipango yake ya kuindolea vikwazo China hadi watakapoona hatua madhubuti zimechukuliwa na Beijing juu ya Taiwan pamoja na kutelezwa kwa haki za binadamu.