1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, demokrasia ya Tanzania inakua au imedumaa?

24 Agosti 2020

Je, demokrasia ya Tanzania inakua au imedumaa? Ndilo swali analoliuliza mchambuzi wetu Anaclet Rwegayura katika Barua kutoka Dar.

Tansania Sansibar Wahlen
Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Mikutano ya kampeni za uchaguzi inawapeleka Watanzania katika uwanja wa kufurahisha kisiasa, wakati washindani wapya wakipanda majukwaani wiki hii kujinadi kama wasemaji wenye mvuto wakati wazoefu wa mchezo huu wakijidai kuwa wao ndio majembe halisi Kama pambano lililoandaliwa na vilabu vya michezo, mikutano hii imepangwa na vyama vya siasa kuuza wagombea wao wa urais na ubunge kwa umma kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020. 

Mikutano ya kampeni inayoanza wiki hii, kama michezo ya kawaida, imeandaliwa kuvutia umati mkubwa wa mashabiki wa vyama tofauti vya siasa. Mashabiki hao wana shauku ya kujua udhaifu na nguvu ya pande zinazopambana katika uchaguzi. Wakati taifa linajiandaa kwa zoezi la kila miaka mitano, wapiga kura wanatarajia vyama vyote vinavyogombea na wagombea wao kujipanga vizuri na kuonyesha ukomavu wao wa kisiasa kuliko chaguzi zilizopita.

Serikali ya Tanzania yagharamia uchaguzi kwa shilingi bilioni 331

Kama raia wenye dhamira ya kuimarisha misingi ya demokrasia nchini, hatuna budi kuipongeza serikalini kwa kuthibitisha uwezo wake kulipa gharama zote za kazi hii muhimu itakayogharimu Shilingi bilioni 331 kutoka katika hazina yake badala ya kutafuta msaada wa kigeni. Hivi ndivyo uchaguzi wa kidemokrasia ya viongozi wa umma unapaswa kufanyika ikiwa lengo lake ni kuwezesha mchakato wa utawala, diplomasia na maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika taifa huru.

Ni wazi kwamba nchi nyingi hivi sasa zinapambana na changamoto mpya na gharama zinazotokana na janga la maradhi ya Korona zikiwa pamoja na kijiweka katika karantini zisizo za kawaida. Kwa bahati Tanzania imeepuka janga hilo. Haijalishi ni nini au ni nani aliyewashawishi wagombea wa chama chochote kuwania  uchaguzi, Rais John Pombe Magufuli sasa anakubaliwa na viongozi wa dini kwa kuiongoza Tanzania kwa mafanikio katika  msingi wa kimungu. Daima anahimiza taifa kumtanguliza Mungu katika kila jambo, ikiwa pamoja na masuala ya kibinadamu ambayo yanawakabili wananchi.

Je, demokrasia ya Tanzania inakua au imedumaa?

Katika harakati za kuwania uchaguzi, Rais Magufuli amesisitiza kwa watekelezaji wa sheria na maafisa wa uchaguzi kuhakikisha haki kwa watu wote pamoja na vyama vyao vya siasa. Karibu tunatimiza miaka 60 kama taifa. Miongoni mwa mataifa, Tanzania bado inachukuliwa kama changa, lakini ukweli ni kwamba imekomaa kiasi cha kutosha kushawishi mataifa mengine katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na utawala na uongozi. Katika kipindi hiki cha uchaguzi, tujiulize: Je, demokrasia ya Tanzania inakua au imedumaa?
Jibu lisitolewe haraka haraka bila ufafanuzi.

Ningetarajia watu watafakari swali hili na kutoa majibu yaliyofikiriwa vizuri, baada ya majadiliano ya kweli na dhahiri kuhusu jamii yetu inavyoondoa ubaguzi wa kila aina, ufisadi na kuimarisha haki kwa wote. Jambo hili linapaswa kuwa mjadala wa kitaifa unaoendelea hata baada ya uchaguzi ikiwa lengo ni kuondoa ufisadi na kuimarisha utawala wa kiraia. Hatuwezi kuruhusu mfumo wetu wa demokrasia uanguke.

Hali ya kisisa ya Tanzania na Afrika kwa Ujumla

Leo tunaona baadhi ya mataifa ambayo yanajiita yameendelea na ambayo yanadai kuwa ya kidemokrasia huku watu wao wakilumbana juu ya uhusiano wa rangi zao, kizazi chao au urithi wao kabla ya kuamua nani achaguliwe kama mwakilishi wao wa kweli. Barani Afrika, ubaguzi wa kisiasa bado uko kwenye migongo  ya ukabila na imani za watu, ukichochewa na ufisadi ili kuzima mwanga wa demokrasia na kuiondoa kabisa mikononi mwa wapigakura.

Soma zaidi: Miaka mingine mitano kwa Magufuli?

Tanzania imejitahidi kushinda vizuizi hivi, lakini mafanikio kamili bado hayajafikiwa. Matukio katika maeneo fulani fulani, kulingana na maelezo ya mashuhuda, yanachukiza sana. Tanzania tunahitaji wagombea waaminifu, wakweli na wenye nia safi washinde uchaguzi. Washindi kama hao ndio watajali maono ya taifa hili na mipango iliyowekwa tayari ya kufika hapo. Juu ya hilo, ni washindi hawa ambao taifa linatarajia kuandika historia yake halisi ya demokrasia na kuirithisha kwa vizazi vijavyo. Utamaduni huo lazima uanze sasa ambapo mpira uko katika uwanja wa kila mtu.

Matokeo ya kura za 2020 lazima yaakisi utashi wa wananchi kuanzia serikali za mitaa kwenda mpaka Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi huko Zanzibar na pia kwa urais wa Muungano na Visiwani.
 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW