1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Felix Tshisekedi ni nani na ana mwelekeo upi?

10 Januari 2019

Tume ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imemtangaza kiongozi wa upinziani Felix Tshisekedi mshindi wa uchaguzi wa rais. Je Tshisekedi ni nani ? Ufuatao ni wasifu wake.

DR Kongo Politiker Felix Tshisekedi
Picha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Yeye ni mtoto wa aliyekuwa kiongozi mahiri wa upinzani Etienne Tshisekedi aliyefariki dunia hivi karibuni. Je mtoto huyo anacho kifua cha kutuliza ghasia katika nchi yenye wakaazi Milioni 80?. Akizungumza na waandishi habari siku ya Alhamis(10.01.2019) Felix Tshisekedi alisema, "hakuna aliyeweza kuwaza kwamba ushindi wa,mgombea wa upande wa upinzani ungeliweza kuthibitika." Tshisekedi amesema wapiga kura wametamka ukweli na ameahidi kuwa rais wa wote katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Mwanasiasa huyo alizaliwa mjini Kinshasa mnamo mwaka 1963. Ana mke na watoto watano. Baba yake Etienne alijaribu kuwapa changamoto marais watatu lakini hakufanikiwa, bila ya mafanikio. Mara ya mwisho baba Etienne alishindwa na rais Joseph Kabila kwa madai kwamba aliibiwa kura.

Harakati za kisiasa

Felix Tshisekedi, mshindi wa uchaguzi wa Congo, kwa mujibu wa matokeo ya awali Picha: Getty Images/AFP/V. lefour

Harakati za akina Tshisekedi dhidi ya udikteta nchini Congo zilianza mnamo mwaka1982. EtienneTshisekedi alianzisha chama cha kidemokrasia na maendeleo ya kijamii katika mji wa Kinshasha,(UDPS). Lengo lake kuu wakati huo lilikuwa kupambana na udikteta wa jenerali Mobutu Sese Seko. Na mpaka leo wachambuzi wanakiona chama hicho kuwa jeshi la kupambana na udikteta.

Kutokana na harakati zake za kisiasa za kupambana na udikteta Etienne Tshisekedi alikamatwa mara kwa mara. Mara tu baada ya Etienne kuzindua chama chake cha UDPS, dikteta Mobutu alimhamishia kwa nguvu kwenye kijiji kimoja katika jimbo la Kasai mbali na mji mkuu Kinshasa na mwanawe ambae wakati huo alikuwa na umri wa miaka 19 alilazimika kukatisha masomo mjini Kinshasha ili kumfuata baba yake. Lakini hiyo ilikuwa hatua muhimu katika maisha ya Felix Tshisekedi.

Akliwa na umri wa miaka 22 Felix Tshisekedi alikimbilia uhamishoni nchini Ubelgiji pamoja na mama yake na ndugu zake. Huku akifanya kazi za vibarua aliendelea na masomo ya biashara na mawasiliano. Hata alipokuwa nchini Ubelgiji tayari alianza kuwa mwanaharakati wa kisiasa. Na mara kwa mara alikabiliana na wafuasi wa watawala wa nchini Congo. Kuna taarifa kuwa aliwahi kupambana na polisi wa Ubelgiji waliojaribu kumzuia baba yake kupanda ndege ili kwenda Kinshasa.

Umaarufu wake 

Felix Tshisekedi huenda akawa rais wa kwanza wa DRC kutoka upinzaniPicha: Getty Images/AFP/L. Tato

Umaarufu wa Felix Tshisekedi bado unaendelea kuwamo kando kando ya chama cha UDPS. Analaumiwa kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa anakataa kubeba jumuku la kukiongoza chama hicho. Lakini baada ya muda mfupi Felix aliingia ulingoni na kuchukua  uongozzi wa chama.

Mwaka uliopita Felix Tshisekedi alichaguliwa kuwa rais wa chama na mgombea wa rais kwenye mkutano mkuu wa chama hicho  uliofanyika kwenye makao makuu katika mji wa Limete ambapoTshisekedi na Vital Kamerhe waliamua kuwa Tshisekedi agombee urais na Kamerhe ataendesha kampeni yake ya uchaguzi na kisha baadae atachaguliwa kuwa waziri mkuu baada ya kushinda uchaguzi huo.

Felix Tshisekedi ameshinda uchaguzi kwa zaidi ya kura milioni saba kati ya kura milioni 18 zilizopigwa ikiwa ni asilimia (38.6%). Mgombea wa pili wa upinzani, Martin Fayulu ameshika nafasi ya pili, kwa kupata kura zaidi ya milioni sita wa tatu ni mgombea wa chama tawala aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Emmanuel Ramazani Shadary, ambaye amepata kura milioni nne tu.

Tshisekedi anatarajiwa kuapishwa rasmi tarehe 18 Januari. Jukumu lake la kwanza litakuwa kuandaa mazishi ya kitaifa ya baba yake, ambaye mwili wake bado umehifadhiwa nchini Ubelgiji.

   

Mwandishi: Antonio Cascais/Zainab Aziz

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW