1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SayansiKimataifa

Je 'GMO' ndio mfumo bora endelevu wa uzalishaji chakula?

31 Mei 2023

Vyakula vilivyozalishwa kwa kubadilishiwa vinasaba vingali vina utata hususan barani Ulaya. Je ndio mfumo bora endelevu wa uzalishaji chakula katikati ya majanga na hasara ya bayoanuwai huku idadi ya watu ikiongezeka?

China Chongqing Herbsternte und der Duft der Erntefelder
Picha: Zhouzhiyong/Sipa/Zuma/picture alliance

Uzalishaji chakula huathiri pakubwa mazingira. Kulingana na wataalam, kilimo huchangia robo ya hewa ukaa au kaboni na pia husababisha kuangamia kwa idadi kubwa ya viumbe hai ulimwenguni. Huku njia endelevu za uzalishaji chakula zikisakwa swali linaloulizwa ni je mfumo wa uzalishaji wa kubadilisha vinasaba maarufu kama GMO ndio suluhisho bora endelevu la uzalishaji chakula? Frederick Schwaller

Na japo shughuli za kilimo zinapungua, idadi ya watu inazidi kuongezeka. Umoja wa Mataifa unatabiri kuwa idadi ya watu itafikia bilioni 10 ifikapo mwaka 2057. Hali hii inaibua swali la ni vipi tunaweza kuongeza uzalishaji wa chakula kwa asilimia 50, huku pia tukidhibiti janga la mabadiliko ya tabia nchi na kuangamia kwa viumbe hai?

Matin Qaim, mtaalamu wa uchumi wa chakula ambaye pia ni mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo na Utafiti katika chuo kikuu cha Bonn Ujerumani amesema "tumegundua kwamba kutumia sehemu kubwa ya ardhi kwa shughuli za kilimo, ndilo kosa kubwa ukizingatia tabia nchi na bayoanuwai.” Ameongeza kuwa hii inamaanisha tunahitaji kuzalisha chakula kwa kutumia sehemu ndogo ya ardhi ili kuweza kulinda asili.

GMO yatishia kumuondosha waziri Kenya

Ni vipi watu bilioni 10 watalishwa?

Kuhusu swali la ni vipi hiyo itawezekana na kuwalisha watu bilioni 10, Qaim ameeleza kuwa kuna njia mbili. Kwanza tunahitaji mabadiliko ya lishe ili kufanya matumizi yetu kuwa endelevu zaidi. Akizungumza na DW amesema hiyo inamaanisha kuwa na upotezaji mdogo wa chakula na vilevile nyama kidogo yaani kupunguza kutegemea protini na vinginevyo kutokana na wanyama.

Mkulima akiwa kwenye eneo la kilimo cha mpunga Magharibi mwa Java, akivuna mchele ili zisiharibike kutokana na mafuriko.Picha: Timur Matahari/AFP/Getty Images

Njia ya pili ni kwamba tunahitaji teknolojia bora zaidi ili kuunda mbinu za kilimo ambazio ni rafiki kwa mazingira. Sawa na wataalamu wengine Qaim anafikiri teknolojia za jeni kukuza vyakula kisayansi ni mkakati muhimu kwa mfumo endelevu wa chakula.

Serikali ya Kenya yabatilisha uamuzi wa kupiga marufuku mbegu za GMO

Qaim amesema "kila mtu anataka kuzalisha chakula kingi kwenye ardhi ndogo na kutumia kemikali kidogo na vilevile mbolea kidogo. Ikiwa unaweza kutumia teknolojia za jeni kukuza mimea inayostahimili zaidi hali mbalimbali, basi ni jambo zuri."

Faida za vyakula vilivyobadilishiwa vinasaba

Kwa mujibu wa wanasayansi haswa wanaounga mkono teknolojia za jeni, vyakula vilivyokuzwa kwa kubadilishwa vinasaba maarufu kama GMO, huweza kuwa na mazao mazuri na hujikinga dhidi ya wadudu, baridi au ukame, na huongeza virutubisho. Pia vinaweza kurekebishwa ili kupunguza utoaji wa kaboni na kuimarisha uendelevu wa uzalishaji chakula. Wameongeza kuwa uzalishaji wa mazao ya GMO hutumia takriban 10% tu ya ardhi ambayo kilimo cha kawaida hutumia.

Wataalam wasema ili mfumo wa uzalishaji chakula kwa kubadilisha vinasaba vya mimea ukubalike, sharti vigezo vyote vinavyohitajika vitimizwe ndipo nchi au taasisi iruhusiwe.Picha: Renee C. Byer/Zumapress/picture alliance

David Spencer, mtaalamu wa magonjwa ya mwili na msemaji wa Replanet, muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea suluhu za kisayansi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na uharibifu wa viumbe hai, amesema GMO si chochote zaidi ya mbinu ya kuzalisha chakula, kama vile kuunganisha mimea ya matunda, kitu ambacho tumekuwa tukifanya kwa maelfu ya miaka. Lakini ni ya kisasa zaidi, kwa hivyo tunaweza kufanya mabadiliko sahihi kwa haraka.

Wasiwasi wa vyakula vya 'GMO'

Mfumo wa ukuzaji vyakula kwa kubadilisha vinasaba ulianza miaka 30 iliyopita. Wanasayansi walitaja wasiwasi mwingi kuhusu usalama wa mfumo huo.

James Rhodes, mchambuzi wa usalama wa viumbe katika nchini Afrika Kusini, ameeleza kuwa miaka thelathini ya tathmini ya data za usalama na ufahamu wa kisayansi yaonesha vyakula vya GMO ni salama kama vyakula vilivyokuzwa kwa njia ya kawaida.

Lakini si wote wanavikubali vyakula vilivyobadilishiwa vinasaba. Uchunguzi wa maoni uliofanywa mwaka 2020 katika nchi 20, ulibaini kuwa asilimia 50 ya watu huchukulia vyakula vya GMO kuwa si salama.

GMO na athari zake kimazingira

This browser does not support the audio element.

Mwandishi: Frederick Schwaller

Tafsiri: John Juma

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW