1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, huu ndiyo mwisho wa Umoja wa Ulaya?

Admin.WagnerD19 Januari 2016

Shinikizo linaloongezeka dhidi ya Kansela Angela Merkel, kumtaka adhibiti mipaka ya Ujerumani, limezua hofu miongoni mwa wadadisi wa mambo, ambao wanahoji iwapo huu ndiyo mwanzo wa kusambaratika kwa Umoja wa Ulaya.

EU-Gipfel / Brüssel
Wakuu wa nchi na serikali za mataifa ya Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/dpa

Akikabiliwa na upinzani miongoni mwa wafuasi wake wa vyama vya kihafidhina na pia kutoka kwa mahasimu wa kisiasa, Merkel alisema Ulaya iko "hatarini" na kwamba hatma ya sarafu ya euro inahusishwa moja kwa moja na utatuzi wa mgogoro wa wakimbizi -- akiainisha hatari ya machafuko ya kiuchumi kama si kusambaratika kabisaa kwa taasisi za Umoja wa Ulaya.

Baadhi ya wanaliona hilo kama mbinu tu za kuwatishia raia wa Ulaya, zinazotumiwa na viongozi wanaohofia kupoteza zaidi kutokana na kuvunjika kwa Umoja wa Ulaya --- Wagiriki na Wataliana wameonekana kuburuta miguu juu ya suala la kudhibiti mpaka wa Mediterania wa kanda hiyo, na raia wa mataifa ya Ulaya Mashariki wanaonufaika na ruzuku za Ujerumani na ajira za viwandani zimepelekea madai ya hasira kuzitaka zisaidie kuchukuwa wakimbizi.

Wajerumani pia wanapata msaada kidogo kutoka kwa mwanzlilishi mwenza wa Umoja wa Ulaya Ufaransa, ambayo viongozi wake wanakihofia chama kinachopinga uhamiaji na National Front, au hata kutoka kwa taifa la tatu kwa nguvu katika kanda hiyo - Uingereza, ambayo imezongwa na mjadala wake juu ya iwapo ijiondowe jumla katika Umoja wa Ulaya.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na rais wa Ufaransa Francois Hollande wa Ufransa wakiwa katika mazungumzoPicha: picture-alliance/dpa/A. Jocard

Iwapo Ujerumani itafunga mipaka...

Iwapo kweli ni vitisho au la -- wakati ambapo juhudi za kuishirikisha Uturuki zikionyesha mafanikio kidogo tu ya kuwazuwia wahamiaji kufika katika fukwe za Ugiriki, maafisa wa Ujerumani na Umoja wa Ulaya wanaonya kuwa bila kuwa na punguzo kubwa katika idadi ya wahamiaji, au kubadili misimamo katika mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya ili kuipunguzia mzigo Berlin wa kuwahifadhi wakimbizi, Ujerumani huenda ikafunga mipaka yake, na hivyo kusababisha mgogoro mkubwa zaidi mwaka huu.

Wakati washirika wa Merkel katika jimbo la kusini la Bavaria wakimtaka aweke ukomo katika kuwapokea watafuta hifadhi kuelekea uchaguzi wa majimbo mwezi Machi, waziri wake wa fedha Wolfgang Schaeuble alionya kuwa ikiwa Ujerumani itafanya kile kila mmoja anachokitaraji, ndipo itakuja kubainika kuwa hilo siyo tatizo la Ujerumani tu, bali ni la Ulaya nzima.

Kansela Merkel na rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claud Juncker wamehusisha udhibiti mpya wa mipaka ya kitaifa katika mataifa ya eneo la uhuru wa kutemebea la Schengen, na kuporomoka kwa soko la pamoja, ambalo ndiyo mhimili mkuu wa kanda hiyo, na pia sarafu ya euro. Yote hayo ikiwa yatatokea yatakuwa na athari mbaya kwa sekta ya ajira na uchumi barani Ulaya.

Mataifa kama Hungary yamejizungushia senyenge kuzuwia wakimbizi.Picha: Reuters/L. Balogh

Hakuna Euro bila Schengen

Juncker alisema katika mkutano wake wa mwaka mpya na waandishi wa habari kuwa bila Schengeni....sarafu ya euro haitakuwa na maana yoyote, na kuongeza kuwa chuki za kihistoria za kitaifa zilikuwa zinaanza kuibuka upya, na kuwatuhumu viongozi wa Umoja wa Ulaya wa kizazi chake kwa kuvuruga urithi wa waanzilishi wa umoja huo, ambao ni manusura wa vita kuu vya pili vya dunia.

Merkel hajasema bado, iwapo Berlin itafuata nyayo za majirani kama vile Austria na Denmark, kuimarisha zaidi ukaguzi wa mipakani ili kuwazuwia kuingia wahamiaji wasio na vielelezo. Lakini amebainisha wazi namna Ulaya inavyoweza kuathirika. Katika mkutano wa wafanyabiashara wiki iliyopita, Merkel alisema mtu hawezi kusema ana sarafu ya pamoja bila ya kuwa na uwezo wa kuvuka mipaka kwa urahisi.

Faraghani, maafisa wa Ujerumani wako bayana zaidi. Wanasema wana muda hadi mwezi Machi au majira ya kiangazi, "kuwa na suluhisho la Ulaya, na baada ya hapo kanda ya Schengen itaporomoka," alisema afisa mmoja.

Afisa wa juu wa Umoja wa Ulaya alitoa kauli sawa na hiyo, akionya juu ya hatari kubwa ikiwa Ujerumani itaamua kufunga mipaka yake, na kusema iwapo hilo litatokea, basi hakutokuwepo tena kanda ya Schengen. Alisema ipo hatari kwamba mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa Ulaya unaofanyika mwezi Februari, ukawa ndiyo mwanzo wa mwisho.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Matumaini kwa Utruruki

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaweka matumaini yao kwa msaada kutoka kwa rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye wengi wanamuona kama dikteta. Berlin inashinikiza Umoja wa Ulaya utoe fedha zaidi kwa Uturuki, jambo ambalo Italia inalipinga. Baadhi ya Wajerumani wamefikia hatua ya kupendekeza kutumia fedha za nchi yao kuzuwia mmiminiko kutoka Uturuki.

Maafisa wa Ulaya hata hivyo wanasema ni mapema mno kuanza kutetemeka. Idadi ya wahamiaji wanaowasili imepungua mwezi huu, ambapo taarifa za Umoja wa Mataifa zimeonyesha idadi hiyo ikiwa nusu ya watu 3500 walioingia kwa siku katika mwezi wa Desemba.

Licha ya hayo, kamishna wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopoulos, aliekuwa Berlin siku ya Jumatatu, aliliambia bunge la Ulaya wiki iliyopita, kuwa hali inazidi kuwa mbaya, na kuongeza kuwa mgogoro wa wakimbizi unatishia misingi ya Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW