1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Kenya kuongeza serikali za kaunti?

15 Novemba 2022

Hoja ya kuongeza idadi ya kaunti nchini Kenya imeshang’oa nanga kwenye bunge, huku mjumbe aliyewasilisha hoja hiyo akisema inalenga kuongeza uwakilishaji kwenye uongozi na kuondoa hali ya jamii zingine kutengwa.

Kenia | Amtseinführung Präsident William Ruto
Picha: Baz Ratner/REUTERS

Mswada huo uliowasilishwa bungeni unapendekeza kuongezwa kwa kaunti tano mpya hivyo kufikisha idadi ya serikali za ugatuzi kuwa 52, kwa kuzigawanya kaunti za Baringo, Migori, Busia, Kitui, Bungoma, na Trans Nzoia.

Kitayama Marwa, mbunge wa Kuria Mashariki aliyewasilisha mswada huo, anashawishi kuwa hatua hiyo itaangazia na kukomesha hali ya jamii ndogo kutengwa kwenye baadhi ya serikali za kaunti nchini.

Mbunge wa Tiati eneo la Pokot Mashariki anaunga mkono hoja hii, ambayo itamaanisha kwamba, eneo la Tiati litaunganishwa na Baringo Kaskazini na kuwa kaunti ya Pokot Mashariki.

Akizungumza na kituo kimoja cha habari cha Kenya, mbunge huyo alitetea kwamba hatua hiyo inatoa suluhisho kwa uhasama ambao umekuwepo kwa muda mrefu kutokana na jamii nyengine kutengwa au kukosa kufikiwa na rasilimali muhimu.

Eneo hilo kame la wafugaji limekuwa na mzozo wa mipaka baina ya jamii jirani kwa miaka mingi.  

Muongozo wa kikatiba

Siku Rais Willian Ruto alipoapishwa kushikilia wadhifa urais nchini Kenya. Licha ya kupinga mabadiliko ya katiba kabla, hivi sasa wabunge wa chama chake cha UDA wanakuja na mapendekezo ya kuibadilisha katiba.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Katiba ya Kenya inatoa mwelekeo na masharti yanayopaswa kuzingatiwa katika kubadilisha mipaka ya wadi, maeneo bunge na kaunti. Kipengele cha 188 kinaipa Tume ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) mamlaka hiyo kuambatana na maswala kama vile idadi ya watu, maoni yao, tamaduni na gharama inayohusika.

Hata hivyo wako wanaolipinga pendekezo hili kwa madai kwamba jamii nyengine zitakapopewa kaunti yao, kila jamii itadai kupewa serikali yao ya ugatuzi.

Aliyekuwa mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, na ambaye ni mfuasi wa karibu wa Rais William Ruto, ni miongoni mwa wanaopinga ugatuzi huu mpya.

Gharama mpya za uendeshaji

Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kushoto), akimkabidhi rasmi nafasi mrithi wake William Ruto.Picha: Baz Ratner/REUTERS

Pendekezo hilo vilevile limeibua swala la gharama za uongozi, kwani kuongezwa kwa kaunti kutamaanisha kuundwa kwa afisi mpya na nafasi za uwakilishi kama vile za magavana, maseneta na wabunge wa kitaifa na wa kaunti.

Hili ni pendekezo la pili la kufanyia marekebisho katiba linalowasilishwa na wabunge kutoka mrengo wa chama tawala cha UDA.

Majuma mawili yaliyopita mbunge wa Fafi, Salah Yakub, alipendekeza kuondolewa kikomo kwa muda anaohudumu rais.

Hii inakwenda kinyume na juhudi za uongozi wa UDA kupinga mapendekezo yoyote ya kubadilishwa kwa katiba katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Imeandikwa na Wakio Mbogho, DW Nakuru

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW