1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Je, kesi ya Machar itazidisha mgogoro Sudan Kusini?

Saleh Mwanamilongo | Isaac Mugabi
27 Septemba 2025

Aliyekuwa makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, anakabiliwa na kesi mahakamani kwa mashtaka yanayojumuisha mauaji na uhaini, hali inayochochea hofu ya kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na mzozo wa kisiasa.

Rieck Machar mjini Juba 2023
Wachambuzi wamesema kesi ya Machar yazidisha mgogoro wa kisiasa na mgawanyiko wa kikabila nchini Sudan KusiniPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Kesi ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, imefufua tena wasiwasi kuhusu amani tete ya nchi hiyo na mustakabali wa serikali ya umoja wa kitaifa. Machar, ambaye amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu Machi, alijitokeza hadharani  wiki hii (24.09.2025) katika kikao maalum cha mahakama kilichofanyika Juba, akiwa ameandamana na washtakiwa wenzake 20, akiwemo Waziri wa Petroli, Puot Kang Chol.

Machar anakabiliwa na mashtaka mazito ya mauaji, uhaini, na uhalifu dhidi ya binadamu, yanayohusishwa na mapigano yaliyotokea Nasir mapema mwaka huu, yakihusisha kundi la wanamgambo la White Army linalotawaliwa na jamii ya Nuer.

Mapema mwezi huu, Rais Salva Kiir alimsimamisha kazi Machar, akitaja sababu za usalama wa taifa. Hatua hiyo imevuruga kwa kiasi kikubwa serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018.

Wito wa uwajibikaji na uwazi

Omara Joseph, Afisa wa Utetezi na Ulinzi katika Mtandao wa Ulinzi wa Haki za Binadamu wa Sudan Kusini, aliiambia DW kwamba kifungo cha Machar kina umuhimu mkubwa.

"Hii ni ishara kuwa Sudan Kusini inaweza pia kuchukua hatua za uwajibikaji," alisema Omara, akitambua changamoto za muda mrefu za nchi hiyo katika kupata haki kupitia taasisi rasmi.

Hata hivyo, alikosoa uamuzi wa serikali wa kuzuia vyombo vya habari kufuatilia kesi hiyo, ambayo ilifanyika katika ukumbi unaotumika kwa harusi na tamasha.

"Huu ni wakati ambapo tunahitaji wadau wa kimataifa kushinikiza, kwa sababu dunia inapaswa kujua kinachoendelea katika kesi hii," aliongeza. "Kwa nini vyombo vya habari vizuiwe na kuruhusu chombo cha habari cha serikali tu?"

Shinikizo za Kisiasa?

Sudan Kusini inakabiliwa na kitisho cha kuzuka tena mapigano ya wenyewe kwa wenyewePicha: Peter Louis Gume/AFP

Waangalizi wanaonya kuwa vikwazo kama hivyo vinaweza kuimarisha mtazamo kuwa kesi hiyo ina msukumo wa kisiasa na huenda isizingatie haki. Mchakato wa kesi pia umechochea tena mvutano wa kikabila kati ya wafuasi wa Machar wa jamii ya Nuerna wale wa Kiir kutoka jamii ya Dinka.

Mwanaharakati wa mashirika ya kiraia, Tabitha Nyantin, aliiambia DW kuwa viongozi wa Sudan Kusini wanapaswa kuweka mbele umoja wa kitaifa.

"Tuna makabila mengi katika nchi hii, na viongozi wanatoka katika makundi mbalimbali ya kikabila," alisema. "Kama hawatabadilisha mtazamo wao, hatutaweza kusonga mbele kama majirani zetu wa Kenya."

Mvutano wa kikabila na madhara ya kisiasa

Uhasama kati ya Machar na Kiir ulianza tangu miaka ya 1990, wakati Machar alipoliongoza kundi lililojitenga ambalo lilishtumiwa kwa kusaliti harakati za waasi. Vikosi vyake vilihusishwa na mauaji ya Bor yaliyolenga jamii ya Dinka, jambo lililozidisha kutokuaminiana kati ya viongozi hao wawili.

Ingawa wamekuwa wakishirikiana madaraka katika serikali ya umoja wa kitaifa, wachambuzi wanasema uhusiano wao bado ni wa mvutano. Daniel Akech, mchambuzi mwandamizi kutoka asasi ya kimataifa inayoshughulikia mizozo ICG , aliliambia shirika la habari la Associated Press kuwa kesi dhidi ya Machar inaonekana kuwa "kisingizio cha mapambano ya kisiasa ya kuwania madaraka."

Kwa kuwa uchaguzi wa urais umeahirishwa mara kwa mara, kesi hiyo inatishia kuvuruga mchakato wa amani na kuleta hali ya kutokuwa na utulivu nchini kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka 2026.

Kurejea kwa Riek Machar Sudan Kusini

00:52

This browser does not support the video element.

Makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 400,000. Wakati serikali ya umoja ikiwa imesambaratika, kesi ya Machar inahatarisha mafanikio ya miaka kadhaa na kuirudisha Sudan Kusini katika mgogoro.

Kadri kesi inavyoendelea, hatari ni kubwa — si tu kwa Machar na washirika wake, bali pia kwa mustakabali wa Sudan Kusini yenyewe.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW