1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, kuiga hoja za mrengo wa kulia kunasaidia vyama vya kati?

26 Oktoba 2025

Utafiti mpya mjini Berlin wabaini vyama vya mrengo wa kati vinaruhusu siasa za mrengo mkali wa kulia kutawala mijadala kwa kurudia kauli zao, mfano ukiwa matamshi ya Kansela Merz kuhusu “mandhari ya miji” ya Ujerumani.

Ujerumani Berlin 2025 | Maandamano dhidi ya ushirikiano wa CDU na AfD
Wakosoaji wa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz wanasema anachochea misemo ya mrengo mkali wa kulia kupitia kauli zake za hivi karibuni kuhusu wahamiaji.Picha: Omer Messinger/Getty Images

Vyama vya siasa vya mrengo wa kati kushoto na kati kulia barani Ulaya vinaimarisha bila kukusudia nguvu za vyama vya siasa vya mrengo mkali wa kulia kwa kurudia hoja na misemo yao ya kisiasa, kwa mujibu wa utafiti mpya wa Kituo cha Sayansi ya Jamii cha Berlin (WZB).

Utafiti huo, uliyochapishwa mwishoni mwa Septemba katika Jarida la Utafiti wa Kisiasa la Ulaya, ulianaliza zaidi ya makala 500,000 kutoka magazeti sita ya Ujerumani katika kipindi cha miaka 26. Ulibaini kuwa si tu wanasiasa wa mrengo wa kulia wanaovuta mjadala wa kisiasa kuelekea ajenda zao, bali pia vyama vya kati kushoto vinachangia hali hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, vyama vya siasa vya mrengo wa kulia vimeendelea kupata umaarufu barani Ulaya — kama Reform UK nchini Uingereza na Alternative für Deutschland (AfD) nchini Ujerumani — licha ya juhudi za wanasiasa wa vyama vikuu vya kati kujaribu kuwavutia wapiga kura kwa sera kali zaidi dhidi ya wahamiaji.

Mamia ya waandamanaji wakiwa na mabango ya rangi wakipinga kauli ya Kansela Merz kuhusu “mandhari ya miji,” wakijikusanya chini ya miavuli kwenye mvua kubwa katika soko la Rathausmarkt, Hamburg, Oktoba 25, 2025.Picha: ABBfoto/picture alliance

Wiki hii nchini Ujerumani, mjadala mkubwa umeibuka kufuatia kauli za Kansela Friedrich Merz kuhusu "mandhari ya miji” ya Ujerumani na athari za uhamiaji, kauli ambazo wengi wameziona kuwa za kibaguzi. Baadaye, alipohojiwa kufafanua, alisisitiza msimamo wake akisema: "Waulizeni binti zenu mtajua ninachomaanisha.”

Mantiki inayojirudi

Kauli za Merz zinajirudia katika siasa za viongozi wa kati barani Ulaya. Mei mwaka huu, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema kuwa Uingereza inaweza kuwa "kisiwa cha wageni” iwapo uhamiaji hautadhibitiwa. Vivyo hivyo, mtangulizi wa Merz, Olaf Scholz, alisema mwaka 2023 kwamba "ni lazima tuchukue hatua kubwa za kuwafukuza wahamiaji haramu.”

Kauli hizi zinaashiria kuwa vyama vya kati vinaamini njia bora ya kukabiliana na kupanda kwa umaarufu wa vyama vya mrengo wa kulia ni kuiga misimamo yao mikali kuhusu wahamiaji.

Lakini kwa mujibu wa Teresa Völker, mtaalamu wa siasa katika WZB na mwandishi mwenza wa utafiti huo, mkakati huo "umekengeuka.” Anasema: "Wanasiasa wa mrengo wa kati wanapojaribu kuvutia wapiga kura kwa kauli za kupinga wahamiaji, wanaongeza nguvu kwa ajenda za vyama vya mrengo wa kulia na kuhalalisha hoja zao.”

Völker anaonya kwamba hatua kama hiyo "inaleta mawazo yaliyokuwa pembezoni hadi katikati ya mjadala wa kisiasa, na kwa kufanya hivyo, inapanua ushawishi wa siasa za mrengo mkali wa kulia.”

Kansela Merz alizusha mjadala mkubwa na ukosoaji baada ya kuwalaumu wahamiaji kwa kuongezeka kwa uhalifu mijini.Picha: Annegret Hilse/REUTERS

Uhusiano wa moja kwa moja au wa bahati?

Si wataalamu wote wanaokubaliana na matokeo hayo. Uwe Jun, mtaalamu wa siasa katika Chuo Kikuu cha Trier, anasema uhalisia wa siasa ni mgumu zaidi. "Uhusiano upo, lakini si lazima usababishwe na jambo hilo moja,” alisema. Anaeleza kuwa vyama vya kihafidhina haviwezi kupuuzia misimamo ya wanachama wao, ambao mara nyingi wanakaribiana na hoja za vyama vya mrengo wa kulia.

Jun anasema hali hii inawaweka wanasiasa kama Merz kwenye mkondo mgumu — wakijaribu kutimiza matakwa ya wapiga kura wao huku wakilaumiwa kwa kuiga siasa za mrengo wa kulia.

Utafiti mwingine wa mwaka 2022 uliofanywa na Werner Krause, Denis Cohen, na Tarik Abou-Chadi ulihitimisha kwamba mikakati ya vyama vya kati kama ile ya Merz na Starmer "haiwezi kupunguza uungwaji mkono kwa siasa za mrengo wa kulia,” bali mara nyingi "huchochea upinzani zaidi.”

Maandamano dhidi ya Kansela Merz kufuatia kauli zake kuhusu “mandhari ya miji” mjini HamburgPicha: Markus Scholz/dpa/picture alliance

Diane Bolet, mhadhiri wa tabia za kisiasa katika Chuo Kikuu cha Essex, anaongeza: "Kujaribu kuwafurahisha wafuasi wa mrengo wa kulia hakusaidii vyama vya kawaida, bali kunafanya suala la uhamiaji kuwa kuu zaidi — jambo ambalo kwa kawaida hufaidi vyama vya mrengo wa kulia.”

Ujerumani bado inachelewa kujifunza

Chama cha AfD, kilichoanzishwa mwaka 2013, ndicho chama pekee cha mrengo wa kulia kilichofanikiwa kupata uungwaji mkubwa nchini Ujerumani — tofauti na vyama kama NPD vilivyoshindwa kwa miaka mingi. Hata hivyo, wataalamu wanasema Ujerumani imeshindwa kujifunza kutokana na uzoefu wa majirani zake kama Ufaransa na Austria, ambako vyama vya mrengo wa kulia vimekuwa sehemu ya siasa kwa miongo kadhaa.

Constantin Wurthmann, mtafiti katika Kituo cha Utafiti wa Ulaya cha Mannheim, anasema tafiti kama hizi zimekuwapo kwa muda mrefu, lakini wanasiasa wamezipuuza. "Wangependa, wangejifunza kutoka nchi nyingine za Ulaya, lakini kwa sasa inaonekana hawakuwa na nia,” alisema.

Anasema kwa kurudia misemo ya siasa za mrengo wa kulia, wanasiasa kama Merz "wanazileta ajenda za chuki katikati ya mjadala wa kisiasa” na hivyo "kuhalalisha siasa za kibaguzi ambazo hapo awali zilikuwa pembezoni.”

Je, uhamiaji ni tishio kwa Ujerumani?

05:49

This browser does not support the video element.

Kwa ufupi

Utafiti wa WZB unasisitiza kwamba siasa za kati barani Ulaya zina hatari ya kujifuta nguvu zenyewe kwa kuiga hoja za mrengo mkali wa kulia. Badala ya kuwadhoofisha wapinzani wao, wanawapa uhalali na kuleta siasa za chuki ndani ya mjadala wa kawaida wa kisiasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW