1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je kuna matumaini ya amani Ethiopia?

26 Oktoba 2022

Wajumbe wa AU waongoza mazungumzo ya kusaka amani Ethiopia,wakati vikosi vya serikali ya Ethiopia vikijiimarisha katika uwanja wa mapambano

Kombobild | Uhuru Kenyatta, Olusegun Obasanjo, Phumzile Mlambo-Ngcuka

Mazungumzo ya kwanza rasmi ya kutafuta amani katika mgogoro wa miaka miwili kati ya jeshi la serikali ya Ethiopia na wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF yameanza jana Jumanne. Mazungumzo hayo yanasimamiwa na Umoja wa Afrika.

Mazungumzo hayo yanafanyika nchini Afrika Kusini na yatamalizika Jumapili wiki hii.

Kinacholengwa kwenye mazungumzo hayo ni kutafuta fursa ya kumalizwa vita hivyo vilivyosababisha maelfu ya watu kuuwawa na mamilioni ya wengine kuachwa bila makaazi wakati mamia kwa maelfu wakiwa ukingoni kutumbukia kwenye baa la njaa katika nchi hiyo ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Picha: AFP via Getty Images

Msemaji wa rais Cyril Ramaphosa, Vincent Magwenya amesema Afrika Kusini ina matumaini mazungumzo hayo yatakuwa chachu ya kupatikana amani ya kudumu nchini Ethiopia.

"Afrika Kusini inawatakia wahusika kwenye mazungumzo kila la kheri na inatarajia mazungumzo yataendelea kwa njia yenye tija na kuleta matokeo ya mafanikio ambayo yatachangia amani ya kudumu kwa watu wote wa Ethiopia''

Hali ya mgogoro huo wa Ethiopia inasababisha ukosefu wa uthabiti katika eneo kubwa la upembe wa Afrika. Mazungumzo hayo ambayo yanasimamiwa na Umoja wa Afrika yalianza katika wakati ambapo serikali ya Ethiopia inaonesha imekuwa ikipiga hatua ya kujiimarisha katika uwanja wa mapambano, ikiiteka miji mingi mikubwa katika jimbo la Tigray katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Vikosi vya serikali ya Ethiopia vinaendesha operesheni yake kwa pamoja na vikosi washirika wake kutoka nchi jirani ya Eritrea.

Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Na operesheni hiyo imezusha khofu ya kusababisha madhara zaidi kwa raia hali ambayo imewafanya viongozi wa Afrika, Marekani na Umoja wa Ulaya pamoja na kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis kutowa mwito wa mapigano kusitishwa na mazungumzo yafanyike haraka.

Umoja wa Afrika umesema kwamba mwenyekiti wake Moussa Faki Mahamat ametiwa moyo na namna ambavyo pande zote zinazoshiriki mazungumzo hayo zilivyoonesha mapema dhamira ya kutaka amani.

Ujumbe wa Umoja wa Afrika kwenye mazungumzo hayo unaoongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, akisaidiwa na rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta na aliyekuwa makamu wa rais wa Afrika Kusini Phumzile Mlambo Ngcuka.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW