1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Libya ni Taifa lililosambaratika?

26 Mei 2017

Huku ikikabiliwa na changamoto za serikali nyingi, kuanguka kwa uchumi na wapiganaji wa ndani kupigania mamlaka, Je Libya ni Taifa lililosambaratika? Mkuu wa misheni ya Umoja wa Mataifa nchini Libya Martin Kobler anajibu

UN Hauptquartier: Martin Kolbler bei PK
Picha: picture-alliance/Pacific Press/A. Lohr-Jones

Kobler ambaye pia anauelewa kwa undani mzozo wa taifa hilo anazungumza na DW kuhusiana na hili.

Kabla ya uteuzi wake mnamo mwaka 2015, Kobler alishika nafasi za juu za majukumu ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Afghanistan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na baadaye alichukua majukumu ya Libya akiwa na lengo la kuzuia nchi hiyo kuja kuwa kama kile alichokiita “Syria ijayo”. Je anaamini anaweza kufikia lengo hili?

Kobler anasema, kuna nafuu kubwa sasa nchini Libya kuliko ilivyo Syria, na haijaingia katika machafuko makubwa. Anakiri kuwepo kwa serikali zinazokinzana, uhalifu mkubwa pamoja na nchi hiyo kutokuwa na serikali kuu kama ilivyo kwa mataifa mengine. Hata hivyo anasema mzozo huo hadi sasa umedhibitiwa, lakini “hatotaka kuyafanya kuwa madogo matatizo yaliyopo”. 

Kobler anasema ni vigumu kuyafanya madogo matatizo ya Libya inayokabiliwa na serikali zinazotofautiana, masuala ya kiusalama na upungufu wa nishati. Uzalishaji wa mafuta, ambao awali ulikuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi hiyo kwa sasa uko chini ya robo ya uzalishaji wa awali wa kabla ya mapinduzi.

Je, Libya ni Taifa lililovurugika?

Kobler anasema hawezi kuitambua Libya kama taifa lililovurugika. Ni taifa ambalo kulikuwa na makubaliano ya amani, ambayo yalisainiwa na Walibya wenyewe mwezi Disemba mwaka 2015, amesema.

Lakini anasema, hoja kuhusu iwapo Libya ni taifa lililosambaratika ama linalosambaratika haiwezi kuwafariji wengi nchini humo hasa kwa kuwa kuna upungufu wa huduma muhimu na machafuko ya kisiasa

Picha: Getty Images/C. McGrath

Kulingana na Umoja wa Mataifa, Libya inasalia kuwa mtoaji wa idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji wanaokimbilia Ulaya. Watu 300,000 wameyakimbia makaazi yao kutokana na machafuko nchini humo na wengine Milioni 1.3, ambao ni pamoja na wahamiaji, wakimbizi na wanaoomba hifadhi wana mahitaji makubwa ya misaada ya kibinaadamu.

Katika ziara yake nchini Libya mapema wiki hii, Kamishna mkuu wa shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR Filippo Grandi, amesema taasisi yake itaimarisha shughuli zake kama moja ya hatua za kukabiliana na hali iliyopo na kutoa mwito wa kuachiwa huru kwa wakimbizi na waomba hifadhi walioko kwenye vituo vya waliokataliwa hifadhi.

Anasema “nilishtushwa na hali mbaya ambayo wakimbizi na wahamiaji walikuwa wanakabiliwa nayo katika vituo wanavyoshikiliwa, kwa ujumla ni kutokana na kukosekana kwa rasilimali” amesema Grandi. “watoto, wanawake, na wanaume ambao tayari wameteseka sana, hawapaswi kukabiliwa tena na magumu kama hayo, ameongeza Grandi.

 Hakuna serikali kuu.

Mkataba wa amani wa Libya, uliotambulikana kama makubaliano ya kisiasa ya Libya ama Libyan political Agreement, LPA,  yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na kutiwa saini mjini Skhirat, Morrocco mnamo mwezi Disemba mwaka 2015, hadi sasa umeshindwa kutatua matatizo ya kisiasa ya nchi hiyo.
 
Kundi la kimataifa linaloangazia mizozo limesema makubaliano hayo yameunda upya zaidi badala ya kuchangia namna ya kutatua mzozo huo wa ndani, na kwamba unahitaji kuundwa upya.

Picha: AP

Miaka sita baada ya mapinduzi na kuondolewa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo hayati Muammar Gaddafi, serikali tatu tofauti katika nchi hiyo, pamoja na makundi kadhaa ya wapiganaji wa ndani wanagombania madaraka.

Umoja wa Mataifa unaiunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa. Lakini kukosa kwake uwezo wa kustawisha maisha ya watu wa Libya, kumekuwa ni chanzo cha ukosoaji hata kutoka ndani ya serikali hiyo.

Mnamo mwezi Januari mmoja wa mawaziri wakuu alijiuzulu akisema, “Sidhani kama hatujui watu wetu wanateseka na nini, lakini hatuna uwezo, na ninakiri kwamba tumeshindwa kwa sababu hatukuweza kutatua matatizo, ambayo ni mengi”

Alipoulizwa, pamoja na kushindwa kwao, Umoja wa Mataifa umeendelea kuiunga mkono serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa, Kobler ameiambia DW kwamba ni kutokana na ukosefu wa mbadala. Amesema kama unataka kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambalo tumekwishalifanya, kwa hiyo unatakiwa kuanza na hatua ya kwanza.

Mwandishi: Lilian Mtono/http://www.dw.com/en/is-libya-a-failed-state/a-38976280.
Mhariri:Josephat Charo