1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je mabadiliko ya tabia nchi yamechangia mafuriko?

19 Julai 2021

Mafuriko makubwa yaliyoletwa na mvua yamesababisha athari za kutisha katika sehemu mbali mbali za Ulaya ya kati ambapo watu chungunzima wamepoteza uhai. Wanasayansi wanasema mabadiliko ya tabia nchi ndio chanzo.

Deutschland Unwetterkatastrophe | Bad Neuenahr-Ahrweiler in Rheinland-Pfalz
Picha: Ferdinand Merzbach/AFP/Getty Images

Watu wasiopungua 103 waliripotiwa kufariki na wengine chungunzima hawajulikani waliko kufikia siku ya ijumaa hapa nchini Ujerumani, Ubelgiji, Uswizi na Uholanzi baada ya vimbunga vikali vilivyoandamana na mvua kubwa iliyosababisha mito kufurika na vyanzo mbali mbali vya maji kupasua kingo zao na kusababisha mafuriko ya ghafla kwenye mitaa, na mali kuharibiwa ikiwemo magari kusombwa na majengo kuharibiwa.

Katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, Ujerumani iliwahi kushuhudia kipindi cha joto kali kabisa na ukame ikafuatiwa na kipindi cha kumwagika mvua kubwa za mawe. Lakini siku ya Jumatano na Alhamisi wiki iliyopita, hali hiyo ilifikia kiwango kingine kabisa kwa kushuhudiwa janga la mafuriko katika mikoa mbali mbali ya Magharibi mwa Ujrerumani na katika nchi jirani.

Watalaamu wanasema hali hiyo mbaya ya hewa ilikuwa huko nyuma ikitokea mara moja baada ya muda mrefu sana lakini katika miaka ijayo  ni hali inayoweza kutokea mara kwa mara na kwa nguvu kubwa, hiyo ikiwa ni dalili kwamba mabadiliko ya tabia nchi yanaanza kuathiri maisha yetu.

Afisa anayehusika na masuala ya mazingira Bernd Mehling kutoka jimbo la Magharibi mwa Ujerumani la NorthRhine Westphalia anasema kawaida hali ya hewa inayoshuhudiwa sasa ni kitu ambacho huonekana tu wakati wa msimu wa baridi kali. Akizungumza na shirika la habari la hapa Ujerumani WDR mtaalamu huyo wa mazingira anasema hali kama hii iliyoshuhudiwa, kwa ukubwa huu sio kitu cha kawaida kutokea katika kipindi cha majira ya joto.

Imekadiriwa kwamba maji yatafikia viwango ambavyo havijawahi kuonekana zaidi ya mara nne katika kipindi cha karne moja katika mji wa Hagen kwa mujibu wa msemaji wa timu inayoshushughulikia dharura wakati sehemu kadhaa za mji huo zikiripotiwa kutofikika na kujikuta imetengwa kutokana na mafuriko makubwa.

Mwananchi amepigwa butwaa ya uharibifuPicha: Wolfgang Rattay/REUTERS

James Quaas mtaalamu wa hali ya hewa kutoka chuo kikuu cha mjini Leipzig, mashariki mwa Ujerumani anasema kinachoshuhudiwa sasa ndio hali itakayokuwa ya kawaida. Anasema mabadiliko ya tabia nchi nayo sasa yanabadili tafsiri ya hali ya hewa ya kawaida iliyozoeleka na kwamba taratibu ulimwengu unaelekea kwenye utaratibu mpya wa hali ya hewa ambao unajumuisha misimu tofauti ya mvua. Lakini wanachojiuliza watu ni ikiwa mabadiliko ya tabia nchi ndiyo yaliyosababisha mafuriko kuwa makubwa kuliko kawaida?

Kimsingi ongezeko la joto husababisha matukio ya hali ya hewa ya kupita kipimo kuongezeka. Vimbunga husababishwa na ongezeko la joto duniani. Na kwa hivyo mtaalamu kutoka taasisi inayohusika na suala la mabadiliko ya tabia nchi katika chuo kikuu cha Oxford, Friederike Otto anasema mvua iliyoshuhudiwa kote barani ulaya katika kipindi cha siku chache zilizopita ni hali ya hewa mbaya ya kiwango cha juu ambayo kuongezeka kwake kunasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na itaendelea kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Shirika la kitaifa linalohusika na masuala ya hali ya hewa Ujerumani DWD limesema kwamba matukio ya mvua kubwa yameongezeka katika wakati ambapo joto nalo pia linaongezeka. Lakini limetahadharisha kwamba ongezeko hilo limekuwa kubwa zaidi wakati wa msimu wa baridi kali na hali bado haiko wazi kuhusu miezi ya msimu huu wa joto wakati ambapo vimbunga vikali kawaida hushuhudiwa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW