1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, makubaliano kati ya Israel na Lebanon mashakani?

Dotto Bulendu
19 Desemba 2025

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya tarehe ya mwisho ya utekelezaji wa usitishaji vita kati ya Israel na Lebanon, wasiwasi unaendelea kuongezeka nchini Lebanon kuhusu hatma ya makubaliano hayo.

Lebanon | Israel
Wasiwasi unaendelea kuongezeka nchini Lebanon kuhusu hatma ya makubaliano kati ya Israel na nchi hiyo kuhusu kusitisha mapiganoPicha: Mahmoud Zayyat/AFP/Getty Images

Mwisho wa juma lililopita, jeshi la Israel lilitoa onyo kwa raia wanaoishi kusini mwa Lebanon, likisema litashambulia miundombinu inayodaiwa kumilikiwa na Hezbollah katika mji wa Yanouh. Israel iliwataka wakazi wa eneo hilo kuhama mara moja kwa ajili ya usalama wao.

Hata hivyo, katika tukio lililoelezwa na vyombo vya habari vya Israel kuwa la nadra na lisilo la kawaida, jeshi la Lebanon liliomba kuruhusiwa kukagua majengo yaliyotajwa badala ya Israel kufanya mashambulizi ya angani. Israel ilikubali ombi hilo na kusitisha shambulio lililokuwa limepangwa.

Tarehe 31 Desemba mwaka huu ndiyo muda uliowekwa na Israel kwa mamlaka za Lebanon kuhakikisha kuwa Hezbollah imepokwa silaha na maghala yake yote ya silaha yameteketezwa. Jeshi la Lebanon linasema tayari limefanya oparesheni kadhaa za kulipua maghala ya silaha, ingawa waangalizi wa kimataifa wanasema ni vigumu kuthibitisha utekelezaji kamili wa hatua hizo.

Licha ya kuwepo kwa usitishaji mapigano uliopatanishwa na Marekani na Ufaransa mwezi Novemba, Israel imeendelea kushambulia maeneno nchini Lebanon karibu kila siku. Zaidi ya raia 120 wa Lebanon wameuawa tangu wakati huo, huku wanajeshi wa Israel wakiendelea kuwepo katika baadhi ya maeneo ya mpakani. Pia kuna mvutano kuhusu iwapo zoezi la kupokonya silaha linapaswa kufanyika kusini mwa Lebanon pekee au kote nchini.

Pande hasimu zinalaumiana kwa kukiuka masharti ya usitishaji vita

Israel na Lebanon zimekuwa zikilaumiana kwa kukiuka masharti ya usitishaji mapigano. Mchambuzi mkuu wa masuala ya Lebanon katika taasisi ya Crisis Group, David Wood, anasema hali hiyo imesababisha mkwamo hatari.

Marekani imekuwa mshirika wa karibu wa Israel katika kuiwekea shinikizo Lebanon, Picha: Anonymous/Middle East Images/IMAGO

"Israel inasema itaondoa wanajeshi wake Lebanon pale tu Hezbollah itakapopokonywa silaha. Hezbollah nayo inasema itafanya hivyo pale tu wanajeshi wa Israel watakapoondoka na mashambulizi kusitishwa, licha ya ukweli kwamba Israel ina nguvu kubwa ya kijeshi,” anasema Wood.

Marekani, ambayo imekuwa mshirika wa karibu wa Israel katika kuiwekea shinikizo Lebanon, imeonya kuwa itapunguza ufadhili wake kwa jeshi la Lebanon endapo halitaharakisha zoezi la kuipokonya silaha Hezbollah. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kudhoofisha zaidi uwezo wa jeshi hilo.

Mshauri mwandamizi wa Baraza la Atlantiki kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati, Nicholas Blanford, anasema mashambulizi yanayoendelea ya Israel yanahujumu juhudi za kuinyang'anya silaha Hezbollah.

Anasema kuwa iwapo Israel ingeondoa wanajeshi wake na kupunguza mashambulizi, shinikizo dhidi ya Hezbollah kuweka silaha chini lingeongezeka zaidi, badala ya hali ya sasa ambayo inaongeza mvutano na kuhatarisha uthabiti wa kisiasa wa Lebanon.

Kwa sasa, Lebanon inaonekana kunaswa kati ya masharti magumu ya kimataifa, shinikizo la kijeshi la Israel na hofu ya mgawanyiko wa ndani—hali inayotia doa mustakabali wa usitishaji huo wa mapigano. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW