1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, mamluki wa Kizungu wanapigana nchini Kongo?

17 Januari 2023

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo sasa inashuhudia uwepo wa mamluki kutoka nchi za Ulaya mashariki. Imeelezwa kwamba kuna mamia ya mamluki walioingia mashariki mwa nchi hiyo.

Demokratische Republik Kongo | Soldaten am Flughafen in Goma
Picha: Alain Uaykani/Xinhua/IMAGO

Mwandishi wa habari wa DW anasema karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Goma mashariki mwa Kongo kuna hoteli inayoitwa Mbiza na mara nyingi hoteli hiyo hupokea wafanyabiashara au wajumbe wa serikali kutoka mji mkuu Kinshasa. Hata hivyo tangu kipindi cha kukaribia sikukuu ya Krismasi,hoteli hiyo imejaa wanajeshi kutoka Ulaya Mashariki.Josue anaishi karibu na uwanja huo wa ndege. "Tumeshuhudia watu kadhaa katika maeneo ya uwanja wa ndege.Baadhi ya watu hao tunashuku kwamba ni Warusi,au wanaofungamana na warusi au Waromania.Lakini mpaka sasa bado hatuna taarifa zaidi.''

Mwandishi mmoja wa habari ambaye ameomba asitajwe jina kutokana na sababu za kiusalama ameeleza kwamba kuna wanajeshi wengi pengine wanafikia hata mia moja ambao ni wazungu walioko katika eneo hilo.Mwandishi huyo anasema wanajeshi hao huvaa magwanda ya kijeshi ambayo hayana bendera ya nchi yoyote na huwa na bastola kwenye mikanda yao viunoni. Kuna ulinzi mkali uliowekwa kwenye mlango wa kuingia hoteli hiyo ya Mbiza mjini Goma,na wanaolinda ni wanajeshi wa kikosi cha ulinzi cha rais wa Kongo,amesema mwandishi habari huyo. Alipoulizia ikiwa kuna nafasi kwenye hoteli hiyo alifahamishwa kwamba vyumba vyote vimeshakodishwa wageni watakaokaa kwa muda mrefu.

Wanawake wanajiunga na jeshi dhidi ya M23Picha: Benjamin Kasembe/DW

Mwanajeshi mmoja aliwaambia  hivi sasa hoteli hiyo ni makao makuu ya wazungu ingawa aligoma kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu hicho alichodokeza.Duru za kidiplomasia zimekuwa zikitowa fununu kwa wiki kadhaa kuhusu maana ya kuwepo wanajeshi hao kutoka Ulaya mashariki katika mji huo wa Goma,kiasi kilomita 30 kutoka Kusini mwa maeneo ya vita. Vita kwenye eneo hilo vilizuka mwaka jana baada ya waasi wenye asili ya Kitusti wa kundi la M23 kulidhibiti eneo kubwa la ardhi karibu na mpaka na Rwanda na Uganda.Jeshi la Kongo limekuwa likikabiliwa na hali ngumu na kupoteza wanajeshi wake wengi kwenye mapigano.

Uwepo wa mamluki hao wakizungu kutoka Ulaya mashariki kwenye hoteli ya Mbiza kumeibua tetesi kwamba serikali ya Kongo  imewaajiri mamluki wakirusi wa kampuni ya Wagner kuisadia nchi hiyo kupambana na waasi.Hata hivyo waziri wa habari na mawasiliano na msemaji wa serikali ya kongo Patrick Muyaya anasema. "Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ina haki ya kuweka ulinzi wake.Nitakupa mfano mmoja.Tuna ndege chapa Suchoi na hatuna watalaamu wa kongo  wanaoweza kuzitazama.Sasa ikiwa tunahitaji mafunzo kwa wanajeshi wetu na tukawageukia kwa mfano wanajeshi wa ufaransa ,hii haimaanishi kwamba tunaleta kundi linalokuja kuanzisha vita. Hapana.''

Mamluki wa Wagner wanaendesha harakati zao MaliPicha: Florent Vergnes/AFP

Kimsingi kundi hili la Wagner lina uzoefu katika ara la Afrika na linatazamwa kama sehemu ya jeshi la Urusi. Wapiganaji hawa wako pia kwenye mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano nchini Ukraine na wanatuhumiwa kuendesha uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu nchini humo. Barani Afrika mamluki wa Wagner wamekodiwa kusaidia kukabiliana na waasi katika nchi za Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Katika kurasa za mitandao ya kijamii zimezagaa tetesi kwamba mamluki wa kundi la Wagner sasa wako nchini Kongo.Nchi hiyo jirani na Kongo ambayo imetuhumiwa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusika kuwaunga mkono waasi wa M23 ndani ya Kongo  ina maslahi yake katika kuichafua sura ya serikali ya Kinshasa kwa kueneza tetesi hizo za uwezekano wa serikali hiyo kuwa na ushirikiano na  kundi la Wagner. 

Tuhuma hizi mara kadhaa zimekanushwa na rais wa Kongo Felix Tschisekedi.Mnamo mwezi Oktoba aliwahi kusema kwamba anafahamu umekuwa mtindo wa mamluki kutumika lakini nchi yake haihitaji kutumia mamluki.Kuanzi mwezi huu wa Januari picha zilianza kusambaa kwenye mtandao wa Tweeter zikionesha maiti ya mwanamme wakizungu akiwa amevalia sare za  kijeshi ikiwa imelala kwenye uchafu.Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na gazeti la Ujerumani la Taz (Tages Zeitung) uongozi wa M23 ulithibitisha kwamba  mzungu huyo aliuwawa katika kijiji cha Karenga Desemba 30. Ingawa mwandishi habari aliyezungumza na Dw alisisitiza kwamba wakongomani wengi hawawezi kutambua ikiwa askari wakizungu walioko nchini mwao ni warusi au ni kutoka nchi nyingine za Ulaya mashariki.Japokuwa katika mji wa Goma bado watu wanawaita askari wakizungu walioko kwenye hoteli ya Mbiza-Warusi wakiwahusika moja kwa moja na kundi la Wagner.

Inafahamika pia kwamba serikali ya Kongo imeimarisha uhusiano wake na Urusi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Hivi karibuni mnamo mwezi Agosti mwaka jana,waziri wa ulinzi wa Kongo  Gilbert Kaband alialikwa katika mkutano wa usalama mjini Moscow ambako aliisifu Urusi kwa kile alichokiita  uungaji mkono wake.Na badala yake Urusi iliahidi kulisaidia jeshi la Kongo linaloyumba kwa vifaa,silaha za kisasa za kijeshi na hasa vufaru,ndege za kivita na helikopta.Mpaka hivi karibuni ahadi hiyo ilikuwa ni viguu kutekelezwa kwasababu ya kuwepo marufu ya silaha iliyowekwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2003.

 Lakini chini ya azimio jipya lililopitishwa na baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa Desemba 20,nchi za ulimwengu hazihitaji tena kutoa taarifa kwa  Umoja wa Mataifa kuhusu biashara ya  silaha au msaada wa kijeshi waliotowa kwa serikali ya Kongo. Na siku mbili baadae mamluki wakizungu waliokuwa na hati za kusafiri za Romania walianza kuonekana wakiwasili mjini Goma.

Makala hii imetafsiriwa kutoka kwenye Kijerumani