Je, Marekani itaishambulia Iran?
20 Februari 2026
Vyanzo vya Marekani vimesema huenda maeneo machache ya kijeshi au ya kiserikali ya Iran yakashambuliwa hivi karibuni. Wakati huohuo vyombo vya habari vya Marekani pia vimeripoti jana kwamba rais Donald Trump anapima uwezekano wa kuruhusu mashambulizi madogo dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu, kuilazimisha ifikie makubaliano ya Nyuklia na Washington.
Jana Rais Donald Trump alisema waziwazi kwamba Iran ina muda wa siku 10 hadi 15 kufikia makubaliano na Marekani kuhusu mradi wake wa Nyuklia, vinginevyo kitatokea kile alichokiita ''Mambo mabaya kabisa'' dhidi ya nchi hiyo.
Mshauri wa kiongozi huyo wa Marekani amekadiria kuna uwezekano wa asilimia 90 wa kufanyika mashambulio ndani ya kipindi cha wiki kadhaa ikiwa mazungumzo yatashindikana.
Vyanzo vinavyofahamu kinachoendelea kuhusu mpango wa Marekani vimesema shambulio la mwanzo ikiwa litaidhinishwa huenda likafanyika ndani ya siku chache zijazo na litayalenga maeneo machache ya kijeshi au maeneo ya serikali.
Kwa mujibu wa ripoti, ikiwa bado Iran itakataa kuafikiana na mapendekezo ya Rais Trump ya kutakiwa kusitisha kabisa urutubishaji wa madini ya urani, Marekani itachukuwa hatua ya kufanya mashambulizi makubwa ambayo huenda yakalenga kuuangusha madarakani utawala wa mjini Tehran.
Taarifa zinaonesha kwamba manuari nyingine ya kijeshi ya USS Gerald R Ford kufikia siku ya Jumatano ilikuwa inakaribia kuingia Gibraltar ikitokea Karribian. Manuari hiyo imepangwa kujumuika na ile ya USS Abhraham Lincoln kwenye bahari ya karibu na Iran.
Hapo jana balozi wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, kupitia barua yake kwa baraza la usalama la Umoja huo wa Mataifa alisema nchi yake haitaki mivutano wala kuingia vitani na haitoanzisha vita vya aina yoyote.
Lakini haitokaa kimya endapo itashambuliwa. Jana pia Jamhuri hiyo ya Kiislamu iliendesha liteka zake za kila mwaka za kijeshi pamoja na Urusi huku matukio yanayofanywa na pande zote mbili Marekani na Iran yakitajwa kama ni ishara ya mataifa hayo kujiandaa kwa vita ikiwa mazungumzo ya nyuklia yatashindwa kupata mwafaka. Iran yatangaza kuufunga Mlango Bahari wa Hormuz baada ya mazungumzo na Marekani
Kadhalika Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameonya kwamba nchi yake inajiweka tayari kujibu mashambulizi ya makombora ya Iran ikiwa nchi hiyo itaamuwa kuishambulia kujibu hatua yoyote itakayochukuliwa na Marekani.
Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amewataka raia wake walioko Iran waondoke huku jeshi la Ujerumani likitangaza kuondowa wafanyakazi wake wasiokuwa na majukumu ya dharura kutoka kambi yake ya kijeshi kaskazini mwa Iraq.