Je, Mataifa ya Ghuba yatajiunga na vita vya Iran?
2 Machi 2026
Katika siku mbili zilizopita, makombora ya Iran yameripotiwa kulenga hoteli za kifahari, bandari, maeneo ya katikati ya miji, viwanja vya ndege na miundombinu ya mafuta katika baadhi ya nchi za Ghuba. Awali, Iran ilisema inalenga mali za Marekani katika eneo hilo kama sehemu ya "haki yake ya kujilinda,” kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel. Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kilitangaza kuwa kingechukulia mali zote za Marekani katika eneo hilo kuwa shabaha halali.
Makombora yalenga vituo vya kijeshi vinavyohusishwa na Marekani
Baadhi ya makombora yaliripotiwa kupiga au kulenga vituo vya kijeshi vinavyohusishwa na Marekani, ikiwemo makao ya Jeshi la Wanamaji la Marekani nchini Bahrain, huku Qatar ikisema ilizuia makombora yaliyokuwa yakielekea kambi ya anga ya Al Udeid. Kuwait nayo ilisema mashambulizi yaligonga kambi ya anga ya Ali Al-Salem ambako kuna wanajeshi wa Marekani.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema hatua ya Iran kulenga pia miji na miundombinu ya kiraia katika nchi za Ghuba ni mabadiliko makubwa. Wanasema nchi hizo ziko karibu zaidi kijiografia na Iran na hazina ulinzi mzito kama Israel, jambo linaloongeza hatari ya mashambulizi kufanikiwa.
Viongozi wa nchi za Ghuba wameonyesha mshikamano na kulaani mashambulizi hayo, wakisisitiza kuwa hawatakaa kimya huku wakilengwa. Lakini hadi sasa, hakuna dalili wazi kwamba nchi hizo zitaingia moja kwa moja vitani kwa kutumia majeshi yao.
Kwa miaka mingi, mkakati wa usalama wa nchi za Ghuba umekuwa ukitegemea uwepo wa kijeshi wa Marekani na ununuzi wa silaha za kisasa kama njia ya kuzuia mashambulizi. Wakati huo huo, katika miaka ya karibuni, baadhi ya nchi kama Saudi Arabia na Falme za Kiarabu zimejaribu kuboresha uhusiano wa kidiplomasia na Iran ili kupunguza mvutano wa kikanda.
Nchi za Ghuba zitalenga kwanza kuimarisha ulinzi wa anga
Kabla ya mashambulizi ya hivi karibuni, nchi kadhaa za Ghuba zilionya dhidi ya kampeni ya kijeshi dhidi ya Iran na hata kusema hazitaruhusu ardhi zao kutumika kufanya mashambulizi. Hata hivyo, ahadi hizo hazijazuia makombora na droni za Iran kulenga maeneo yao.
Wataalamu wanaamini kuwa hatua ya kwanza ya nchi za Ghuba itakuwa kuimarisha ulinzi wa anga na makombora, kulinda miundombinu muhimu na kuongeza usalama wa ndani. Pia zinatarajiwa kuimarisha juhudi za kidiplomasia kupitia mataifa kama Oman na Qatar ili kutafuta njia ya kupunguza mvutano.