Je mkutano wa G8 utatoa matumaini kwa Afrika?
5 Julai 2005Wakati mkutano wa viongozi wakuu wa kundi la nchi 8 tajiri duniani ukitarajiwa kufunguliwa hapo kesho huko Scotland, Uingereza imekiri kwamba huenda ikashindwa kulifikia lengo lake la kuumaliza umaskini barani Afrika.
Wakati huo huo wapinzani wa utanda wazi wanaendelea kuzusha vurugu karibu na maeneo kunako tarajiwa kufanyika mkutano huo hapo kesho.
Waziri wa fedha wa Uingereza bwana Gordon Brown amesema juhudi za nchi yake za kutaka kulisaidia bara la Afrika katika mkutano wa nchi nane tajiri duniani huenda zikakabiliwa na upinzani kutoka kwa viongozi wa nchi nyingine zilizo ndani ya kundi hilo la nchi nane tajiri duniani la G8.
Mkutano huo wa viongozi wakuu wa kundi la nchi nane tajiri duniani unafunguliwa hapo kesho huko Scotland.
Bwana Brown aliliambia shirika la BBC kwamba kile inachosema uingereza ni kwamba kinachoweza kuushawishi ulimwengu kitatokana na matokeo ya mkutano huo utakaofanyika Gleneagles Scotland.
Bwana Brown alikuwa akikumbusha yale aliyowaambia wafanya kampeini walioandaa tamasha za kuwatumbuiza walimwengu na wakati huo huo kuwahamasisha juu ya matatizo ya bara la Afrika.
Makundi mbali mbali ya muziki yaliungana hapo jumamosi iliyopita kwa lengo la kuzishinikiza nchi tajiri duniani kulisaidia bara la Afrika. Nchi hizo ni pamoja na Marekani,Canada,Ufaransa,Germany,Italy,Japan na Russia.
Uingereza iliamua kuungana na wanatamasha hao pamoja na waanaofanya maandamano katika mji mkuu wa Scotland Edinburgh kuzishinikiza nchi tajiri duniani kukubali mpango wa kuziondolea madeni nchi maskini barani Afrika,kuziongezea msaada wa maendeleo pamoja na kuweka usawa wa kibiashara .
Mwezi uliopita mawaziri wa fedha wa mataifa hayo tajiri duniani walikubaliana kuziondolea madeni nchi 18 maskini zaidi nyingi zikiwa kutoka bara la Afrika.Madeni hayo yalifikia kiasi cha dolla bilioni 40.
Hata hivyo wafanyikazi wa mashirika ya misaada wamesema hatua hiyo ya kuziondolea madeni nchi maskini imeshindwa kutatua tatizo la madeni yanayodaiwa nchi hizo na mashirika ya kibinafasi.
Pamoja na yote hayo bado haijaeleweka iwapo Uingereza itaweza kulifikia lengo lake la kuongeza mara mbili msaada wa maendeleo kwa nchi hizo maskini kutoka kiasi cha dolla bilioni 50 hadi dolla bilioni 100 kila mwaka.
Kwa upande mwengine wafanyikazi wa mashirika ya kibinafsi pamoja na wanaharakati wanaotaka kuondoshwa kwa umaskini barani Afrika wanazitaka nchi tajiri duniani kuweka usawa katika biashara.
Pamoja na hayo wanaharakati hao pia wanataka kuondolewa kwa ruzuku zinazofanya bidhaa za wakulima wa mataifa ya magharibi kuuzwa kwa bei rahisi.
Uingereza ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo wa viongozi wa mataifa tajiri duniani imetaka pia hatua za haraka zichukuliwe za kupambana na kuongezeka kwa joto duniani linalosababishwa na uchafuzi wa mazingira unaotokana na moshi wa viwandani.
Lakini hata hivyo rais Gorge W Bush wa Marekani jumatatu iliyopita amekataa kuunga mkono mpango wowote unaofanana na rasimu ya kyoto ya mwaka 1997 iliyolenga kupunguza matumizi ya hewa chafu ya Carbon.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza bwana Jack Straw hata hivyo ametabiri kwamba mkutano wa kesho utakuwa na matokeo ya kuridhisha juu ya masuala muhimu ya mabadiliko ya hali ya hewa na kumaliza umasikini Barani Afrika.
Hofu ya kuzuka ghasia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa Gleneaglea hapo kesho ,imeongezeka baada ya wapinzani wa mataifa hayo tajiri duniani G8 na wapinzani wengine wa sera za utandawazi kukabiliana na polisi katika mji wa Edinburgh na kusababisha kusimama kwa shughuli za mji.
Takriban watu kiasi cha 60 walikamatwa wakati wa pata shika hiyo huku waandamanaji 20 na polisi kadhaa wakipata majeraha madogo madogo wakati chupa zilipokuwa zinavurumishiwa polisi.
Hata hivyo Polisi wa hali juu wanaendelea na operesheni zao za kulinda usalama katika eneo hilo. kikosi hicho cha polisi kimewajumuisha zaidi ya maafisa elfu 10 kutoka nchini Uingereza.
Wageni walioalikwa kuhudhuria mkutano huo wa kila mwaka ni pamoja na viongozi wa nchi saba za Afrika,ikiwa ni Algeria,Ethiopia,Ghana,Nigeria,Senegal,Afrika Kusini na Tanzania pamoja na nchi nne zinazoinukia kuwa na nguvu kubwa kiuchumi Brazil,China,India na Mexico.