Je mradi huu utapunguza adha ya maji Dar es salaam?
11 Novemba 2022Akizindua mradi wa maji pamoja na vifaa vya utafiti wa maji wilayani Kigamboni, jijini hapa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema pamoja na mabadiliko ya tabia nchi kuwa chanzo cha ukame, lakini wakazi wa mkoa wa Pwani na Morogoro ambako kuna vyanzo vya maji, wamekuwa ndicho chanzo cha uhaba wa maji kutokana na tabia zao hatarishi ikiwamo kunywesha mifugo, kuzuia maji na kutumia maji ya mto Ruvu kusafisha madini.
Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira(DAWASA) kutoa elimu kwa wananchi ili waache uharibifu huo, kuongeza uzalishaji wa maji pamoja na kugawa maji bila upendeleo wowote.
Rais Samia amezindua mradi wa maji wa Bwawa la Kidunda wenye thamani ya Shilingi milioni 329, unaotarajiwa kuanza leo na kumalizika baada ya miaka mitatu, lakini pia amezindua vifaa vya utafiti wa maji, na mabwawa ya maji yatakayosaidia kunywesha mifugo na wakazi wa jiji hilo.
Kadhalika Rais Samia amesema serikali inatimiza malengo ya kidunia ya kuhakikisha kuna uhakika wa upatikanaji wa maji nchini ifikapo 2030.
Kwa upande wake Waziri wa Maji nchini Jumaa Aweso amesema mradi huo wa maji, utahusisha visima saba vya maji, ambavyo vitazalisha lita milioni 70.
Lakini akasema Tanzania haina changamoto ya maji bali ina uhaba wa rasilimali za kuchakata maji, akaongeza kuwa, mradi huo, utatumia zaidi maji ya mvua kuzalisha na kuweka akiba kubwa ya raslimali hiyo muhimu.
Kwa nyakati tofauti, Novemba mwaka jana na Oktoba mwaka huu, Waziri Aweso amenukuliwa akisema kuwa uhaba wa maji uliopo jijini Dar es salaam, umesababishwa na kushuka kwa kina cha maji mto Ruvu, ambako kunategemewa zaidi na jiji la Dar es Salaam kama chanzo kikuu cha maji.