1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Je, NATO inapaswa kudungua droni za Urusi?

13 Septemba 2024

Droni na makombora yanayorushwa na Urusi kuelekea Ukraine hukiuka mara kadhaa anga ya nchi wanachama wa jumuiya ya kijeshi ya NATO.

Viongozi wa NATO kwenye mkutano wao mjini  Washington DC
Viongozi wa NATO: Kutoka kushoto ni Rais wa Marekani Joe Biden, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Katibu Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Jakub Porzycki/NurPhoto/picture alliance

Idadi ya matukio hayo imekuwa ikiongezeka katika wiki nne zilizopita. Wataalam wanapendekeza majibu kutoka kwa NATO. Lakini je, muungano huo wa kijeshi unapaswa kuchukua hatua kama hiyo?

Mapema siku ya Jumapili ya Septemba 8, ndege mbili za kivita za Romania chapa F-16 zilipaa kutoka kituo cha anga cha Borcea, mji ulio karibu na mpaka wa Ukraine. Wakazi wa mkoa huo walipewa taarifa hiyo kupitia ujumbe mfupi kwenye simu zao za mkononi.

Hatua hiyo ya dharura ilichukuliwa baada ya mfumo wa ulinzi wa anga wa Romania kugundua kuwa droni ya Urusi ilikuwa imekiuka anga yake na iliripotiwa eneo hilo kwa zaidi ya dakika 30 kabla ya kurejea kwenye anga ya Ukraine.

Soma pia: Idara ya upelelezi ya Ujerumani yaishutumu Urusi kwa hujuma dhidi ya NATO

Halikuwa tukio la kwanza la aina hiyo nchini Romania au katika eneo la pamoja la Jumuiya ya kujihami ya NATO. Siku moja tu kabla ya hapo, droni nyingine ya Urusi ilidondoka karibu na mji wa Latvia wa Rezekne, na ambayo inadhaniwa ilitokea kwenye nchi jirani ya Belarus ambaye ni mshirika wa karibu wa Urusi.

Idadi ya matukio kama hayo imekuwa ikiongezeka katika wiki nne zilizopita, huku Urusi ikionekana kuwa tayari kuchukua hatua za hatari zaidi. Jamie Shea, naibu katibu mkuu wa zamani wa  NATO  aliyekuwa akishughulikia changamotoza kiusalama katika jumuiya hiyo ameiambia DW kuwa hali inazidi kuwa mbaya, na NATO sasa inabidi ichukuwe hatua.

Shea, ambaye sasa ni mshirika mkuu katika taasisi ya Friends of Europe ya mjini Brussels, anasema kuwa muungano huo wa kijeshi unapaswa kuzipa nchi wanachama ulinzi zaidi kwa kuwa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, muungano huo uliahidi kulinda eneo zima la NATO.

Je, Urusi inaijaribu NATO?

Ndege ya kivita chapa F16 ya RomaniaPicha: U.S. Air Force/ZUMA/picture alliance

Muungano wa kijeshi wa NATO ulilaani ukiukaji wa hivi majuzi wa anga yake uliofanywa na Urusi, na kuutaja kuwa wa kutowajibika na unaoweza kusababisha hatari. Hata hivyo, katika chapisho lake kwenye mtanadao wa kijamii wa X, Naibu Katibu Mkuu wa NATO anayemaliza muda wake Mircea Geoana alidokeza kwamba muungano huo hauna taarifa zozote zinazoonyesha kuwepo kwa shambulio la makusudi la Urusi dhidi ya nchi washirika.

Wataalamu kama vile Jan Kallberg, mtafiti katika Kituo cha Uchambuzi wa Sera za Ulaya kilichopo mjini Washington, Marekani wanashuku kuwa Urusi inaweza kuwa inalenga kuyafahamu majibu ambayo NATO inaweza kuyatoa ili kupambanua kati ya kile kinachosema na kile kinachoweza kufanywa. Pia wataalamu hao wanasema huenda ikawa ni hatua ya kutaka kujaribu uwezo wa mawasiliano baina ya nchi washirika wa NATO.

Soma pia: Usalama waimarishwa katika kambi ya NATO kutokana na kitisho cha usalama

Suala hilo lilikuwa miongoni mwa mada kuu zilizojadiliwa wiki hii wakati wa mkutano wa faragha wa NATO mjini Brussels. Shinikizo linaonekana kuongezeka kwa NATO kuchukua hatua zaidi ikiwa ni pamoja na kuongeza ukaguzi na doria pamoja na kupeleka mifumo zaidi ya ulinzi wa anga katika eneo la Mashariki la muungano huo wa kijeshi.

Wengi wanajiuliza je, NATO inapaswa kudungua droni za Urusi? Katika mahojiano ya hivi majuzi na gazeti la Financial Times, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Radek Sikorski, alisema kuwa Poland, pamoja na nchi nyingine zinazopakana na Ukraine, zina "wajibu" wa kudungua makombora na droni za hata kabla ya kuingia kwenye anga yao. Lakini kufikia sasa, NATO inalipinga pendekezo hilo, ikisema kuwa linaiweka kwenye hatari ya muungano huo kuwa sehemu ya mzozo huo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW