Je, ni kwa kiasi gani Warepublican watabadilisha Marekani?
11 Novemba 2024Marekani imeelekea mrengo wa kulia kwa kiasi kikubwa baada ya uchaguzi, ambapo Warepublican wanaounga mkono vuguvugu la Trump la kuifanya Marekani kuwa taifa kuu tena, linalojulikana kama "Make America Great Again, au MAGA, sasa wana wingi katika Seneti na huenda pia wakadhibiti Baraza la Wawakilishi mara kura zote zitakapohesabiwa.
Soma pia: Trump afanya uchaguzi wa kwanza wa baraza la mawaziri
Vuguvugu hilo la MAGA limesema limefanikiwa kuidhibiti nchi yao tena, na tayari wakati wa kampeni walidokeza mipango mikubwa ya jinsi Warepublican wanavyokusudia kutumia mamlaka hayo. Tofauti kubwa na ushindi wa Trump katika uchaguzi wa 2016 ni kwamba safari hii amejiandaa zaidi, anasema Stormy-Annika Mildner, mkurugenzi wa taasisi ya Aspen ya nchini Ujerumani, ambayo ni taasisi huru ya utafiti wa kisera. "Amejifunza pia kuwa inaweza kuwa tatizo kwake kuwa na watu wasiokuwa waaminifu ndani ya timu yake.
Soma pia:Viongozi wa Ulaya wakutana Budapest kufuatia ushindi wa Trump Kwa hivyo, inatarajiwa kwamba safari hii watateuliwa wafuasi na waaminifu halisi wa Trump, ambao anaweza kuwategemea kwa asilimia mia moja. Kwa kubadilisha watu kwa kiasi kikubwa, hata kwenye wizara, kutakuwa na mabadiliko muhimu kwani hakutakuwepo tena na watu ambao, kama ilivyokuwa kati ya 2016 na 2020, walizuia mambo mabaya zaidi kutokea mahali fulani."
Mildner anatarajia kuwa waraka wa mkakati wa mradi wa 2025, uliyotolewa hadharani msimu wa kiangazi, utakuwa na nafasi katika ajenda mpya, huku baadhi ya wafuasi wa Trump wanaodaiwa kuhusika katika kuandaa mpango huo wakiweza kushika nyadhifa zenye ushawishi serikalini. Trump alikubali takwa muhimu kutoka Mradi 2025, akiahidi operesheni kubwa ya kuwafukuza wahamiaji, kuongeza uchimbaji wa mafuta yenye madhara kwa mazingira, na kulegeza kanuni za mazingira.
Mamlaka za shirikisho kama vile Mamlaka ya Ulinzi wa Mazingira, EPA, zitakuwa muhimu katika kusukuma mipango hii. Mandy Gunasekara, aliyekuwa mkuu wa EPA wakati wa utawala wa kwanza wa Trump, anapendekezwa kuwa kiongozi wake mpya. Inatarajiwa kwamba badala ya kuimarisha ulinzi wa mazingira, Trump atazingatia sheria kali katika maeneo mengine kama uhamiaji na uchimbaji wa mafuta.
Wachambuzi wanasubiri kwa hamu kuona nani Trump atamteua kuongoza Wizara ya Sheria, baada ya kutangaza nia ya kuitumia kwa mashtaka ya kisheria dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa. Pia, akiwa na uungwaji mkono wa Warepublican wenye wingi katika Seneti, atakuwa na uwezo wa kuteua majaji wahafidhina hadi uchaguzi wa katikati ya muhula mwaka 2026.
Profesa John Collins wa Chuo Kikuu cha George Washington aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa Trump alibadili mfumo wa mahakama za shirikisho katika muhula wake wa kwanza na sasa ana nafasi ya kuimarisha maono hayo kwa kizazi kizima.
Mildner anatabiri kuwa chama cha Republican kitajaribu kutumia fursa hii kufanya marekebisho makubwa ya serikali ndani ya mipaka ya katiba bila kuigusa katiba yenyewe, na kuongeza kuwa mabadiliko ya katiba ni mchakato mgumu ambao unaweza kuwaweka pabaya wenyewe pia ikiwa watajikuta katika upinzani.
Licha ya Ikulu, Congress, na Mahakama Kuu kuwa chini ya wahafidhina, Mildner ana imani kuwa taasisi nyingine kama vyombo vya habari zitatimiza wajibu wao wa kudhibiti mamlaka. Hata hivyo, amesema miaka hii minne itaongeza mgawanyiko wa kisiasa nchini Marekani.