Je, ni kweli majeshi ya Jubaland yako ndani ya Kenya
4 Septemba 2025
Raia wa Kenya wanaoishi karibu na mpaka na Somalia wanaishi kwa hali ya wasiwasi, kufuatia kumiminika kwa wingi kwa wapiganaji wenye silaha kutoka Somalia, wanaokimbia makabiliano baina yao na serikali ya mjini Mogadishu.
Wapiganaji hao wanatokea Jubaland, jimbo la kusini mwa Somalia ambalo kwa muda mrefu limekuwa likipambana na vikosi vitiifu kwa serikali kuu. Mwezi uliopita wa Agosti vikosi vya serikali viliukomboa mji muhimu katika jimbo hilo, hali iliyowasukuma wapiganaji wa kijimbo kukimbilia katika kaunti ya Mandera kaskazini mashariki mwa Kenya.
''Hofu imetanda katika eneo hili...wakazi wengi wameamua kukimbia,''alisema Urgus Shukra, mzee wa makamo kutoka Mandera katika mahojiano ya simu na shirika la habari la AFP.
Urgus alisema kuwa wapiganaji wenye silaha kutoka Somalia wamekuwapo kwenye eneo lao kwa wiki nne sasa, na kwamba wamekita kambi katika ''maeneo muhimu sana kwa kilimo.''
''Wakati wote wanafyatua bunduki. Hata mafunzo yao wanafanyia hapo hapo,'' alisema Shukra.
Kitisho cha wapiganaji hao wa Somalia kimelalamikiwa pia na seneta wa jimbo la Mandera, Ali Ibrahim Roba, kupitia ujumbe aliouweka kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X. ''Vikosi vya Jubaland viko ndani ya mji wa Mandera. Shule zimefungwa, biashara zimepooza, na watu wamelazimika kuzihamisha familia zao kwa hofu ya kupigwa risasi au kujeruhiwa na vifaa vya miripuko.''
Ukimya wa serikali wazusha mashaka
Akizungumza na vyombo vya habari Jumatano (03.09.2025) waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen amepuuza kitisho hicho cha vikosi kutoka Somalia, akisema kimeongezwa chumvi kwa sababu za kisiasa.
''Hivi sasa hatuwezi kuthibitisha watu hao ni wa namna gani...kama ni vikosi vyenye silaha, au ni raia tu wa kawaida,'' Murkomen aliviambia vyombo vya habari nchini Kenya.
Habari za kusuasua kwa usalama jimboni Mandera zilianza kusikika mwishoni mwa mwezi Agosti. Gavana wa Mandera, Mohamed Adan Khalif alipiga la mgambo wiki iliyopita, akidokeza juu ya uwepo wa vikosi kutoka Somalia vilivyojihami kwa salaha. Kiongozi huyo alisema hali hiyo inakiuka uhuru wa kieneo wa Kenya.
''Hatuna maslahi yoyote nchini Somalia, maslahi pekee tuliyonayo kwa Somalia ni amani,'' alisema gavana Khalif, na kuongeza kuwa ikiwa watu wa Somalia watachagua vita badala ya amani, ''hatuwezi kuingilia katika mambo yao ya ndani.''
Maelfu ya wakazi wa mji wa Mandera waliandamana Jumanne, wakishiniza wapiganaji hao wageni waondoke kwenye eneo lao.
Rais William Ruto bado hajasema chochote kuhusu hali hiyo inayojiri kwenye mpaka na Somalia, na kimya chake kimekosolewa vikali na wanasiasa wa upinzani.
''Huu ni uvamizi na ukaliaji wa kimabavu,'' alisema Kalonzo Msyoka, kiongozi wa chama cha upinzani cha WPF, ambaye alimkosoa vikali Ruto kwa kutojitokeza kuzungumzia suala hilo. Tunamtaka amir mkuu wa jeshi, ambaye ni Rais William Ruto, kueleza juu ya hali hii."
Kenya inachukua tahadhari isihujumu maslahi yake
Kenya inavyo vikosi vyake vya jeshi katika jimbo la Jubaland, ikilitumia kama kama ukuta dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu wa al-Shabaab, ambalo miaka ya nyuma lilifanya mashambulizi ya kigaidi ndani ya Kenya.
Kiongozi wa jimbo la Jubaland, Ahmed Madobe ni mshirika wa kisiasa wa Kenya, ambaye anakabiliwa na shinikizo kutoka serikali kuu ya Somalia, ambayo haiutambui utawala wake.
Kuingia kwa wapiganaji wenye silaha kutoka Jubaland hivi karibuni kumeongeza dhiki ambayo imekuwepo kwa miezi kadhaa sasa katika eneo hilo la mpaka baina ya Kenya na Somalia.
Licha ya juhudi za serikali za nchi zote mbili kuimarisha mikakati, mashambulizi ya mara kwa mara, vifo vya raia na maafisa wa usalama, pamoja na changamoto za kijamii na kiuchumi, vinaendelea kuathiri maisha ya watu wanaoishi karibu na mpaka huo.
Mwezi Aprili watu watano, miongoni mwao wakiwamo maafisa wawili wa polisi waliuawa katika shambulizi la bomu kataka mji wa El- Wak katika jimbo la Mandera na ingawa hakuna upande wowote uliodai kuhusika, mara kwa mara kundi la al-Shabaab limekuwa likifanya hujuma katika eneo hilo.
Wakazi wa Mandera hawataki suluhisho la kudumu
Mashambulizi ya Aprili yalizua hofu na wasiwasi miongoni mwa wakazi wa maeneo ya mpakani na kuathiri shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi. Ingawa hali ya utulivu ilirejea baada ya serikali kuingilia kati, mkazi mmoja wa mji wa al-Wak, Yakub Mohammed, alisema wanachokitarajia ni suluhisho la kudumu.
"Tunaomba tuletewe maafisa wa usalama wa kutosha hapa El-Wak, hata wakihamisha wengine waje waishi hapa, inawezekana. Kuna wengine El-golicha, wakija kutusaidia hapa itakuwa ni sawa."
Kama Yakub Mohammed, wakazi wa eneo la mpaka kati ya Kenya na Somalia wanaamini kuwa askari wanaolihafahamu vyema eneo hilo na uhalisia wake.
''Sasa askari ametoka maeneo mengine ya Kenya, hajui eneo hili na hawezi kumtambua adui na mahali alipo. Huyo askari anaweza kutafuta maadui? Wale watu wanaoweza kuwatafuta adui ni wale wanaoishi Mandera Magharibi. Kwa hivyo serikali iwape nguvu wwnyeji,” alisema mkazi mmoja aliyezungumza na DW kwa sharti la kutotambulishwa.
Kabla ya mripuko huo, machifu watano walitekwa nyara huko Mandera na wanamgambo wa Al-Shabaab walipokuwa wakisafiri kutoka Wargadud kuelekea Elwak. Machifu hao waliachiwa huru baada ya kuzuiliwa kwa kipindi kirefu.
Serikali za Kenya na Somalia zimeanzisha mradi unaolenga kuboresha usalama katika mpaka baina wao, kwa matarajio kuwa juhudi hizi zitapelekea kuleta utulivu na kurahisisha biashara huria na uhamaji halali wa watu. Mradi huo kwa jina Daris Wacan—kwa maana "majirani wema”—unalenga kunufaisha watu 160,000 kwa kupanua upatikanaji wa maji endelevu, kuimarisha miundombinu, na kuendeleza njia za kujikimu zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi.