Majina ya kumrithi Kansela Angela Merkel yapendekezwa
29 Desemba 2017Uchunguzi mpya wa maoni uliyotolewa na shirika la YouGov siku ya Jumatano unaonyesha kuwa asilimia 45 ya Wajerumani wangelitaka Kansela Angela Merkel asikamilishe muhula wa nne uongozini huku asilimia 36 pekee ikisema ingelitaka kumuona akikamilisha muhula mwengine.
Hata hivyo hii yote itategemea iwapo ataweza kweli kuunda serikali ya mseto, jambao ambalo linaweza kuchukua muda. Mazungumzo ya awali juu ya kuunda serikali mpya ya muungano mkuu na chama Social Democratic (SPD)yanatarajiwa kuanza tarehe 7 mwezi wa Januari, huku mazungumzo halisi yakitarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huo, hii ikimaanisha kuwa serikali mpya nchini Ujerumani huenda isiundwe hadi wakati wa kipindi cha Pasaka.
Lakini haijulikani wazi iwapo hivi ndivyo mambo yatakavyokwenda, Mazungumzo ya mwisho yaliyotarajiwa kuunda kile kilichoitwa muungano wa Jamaica jina lililotokana na rangi ya vyama hivyo kufanana na bendera ya Jamaica, vyama ambavyo ni kile cha Angela Merkel cha Christian Democratic Union (CDU), chama ndegu cha kihafidhina cha Bavaria Christian Social Union (CSU), kile cha walinzini wa mazingira cha kijani na chama cha kiliberali cha Free Democratic (FDP) — hayakufua dafu mwezi Novemba, huku vyama vingine vikikilaumu chama kinachopendelea wafanyabishara cha FDP kwa kubadili malengo yake ya kisera katika dakika za mwisho.
Mwanasiasa Daniel Günther, ndiye mtu anayeonekana kuweza kuvivaa viatu vya Merkel
Wiki hii chama cha FDP kilijibu tuhuma hizo, kupitia kiongozi wake Christian Lindner na naibu kiongozi Wolfgang Kubicki wote wakisema kuwa chama hicho hakikuweza kuingia katika mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto wakati Merkel akiwa Kansela iwapo kutakuwepo na uchaguzi mpya na pia kuhoji iwapo CDU inaweza kuendelea na Merkel kama kiongozi wake.
Lakini hata kama wakati wa Merkel umekwisha hakuna mtu aliye na uhakika nani anayeweza kuchukua nafasi yake ndani ya chama chake ambacho kinabakia kuwa chama kikubwa na muhimu nchini Ujerumani. Kwa upande wake Wolfgang Kubicki alipendekeza mwanasiasa Jens Spahn katibu mkuu katika Wizara ya fedha, mwenye umri wa miaka 37. Mwengine ni mwanasiasa aliye na miaka 44 Daniel Günther, Waziri mkuu mpya wa jimbo la Schleswig-Holstein.
Jina lengine ambalo pia limekuwa likisikika ndani ya CDU ni lile la Annegret Kramp-Karrenbauer aliye na miaka 55 aliyekipeleka chama cha Merkel katika ushindi katika jimbo dogo la Magharibi la Saarland mapema mwaka huu. Lakini kwa Merkel Mwenyewe kwa sasa yupo likizo na mumewe Joachim Sauer, Profesa wa fizikia na kemia aliyestaafu mwezi Octoba.
Merkel alikuwa na ati ati ya siku nyingi ya iwapo agombee tena ama ajiunge na mumewe katika kustaafu lakini mwishoni ilikujulikana wazi kuwa bado ana nguvu za kugombea.
Mwandishi: Amina Abubakar/DW English
Mhariri: Iddi Ssessanga